Thursday 13 November 2014

Serikali kulipa deni la watumishi wa umma


WATUMISHI wa Umma wanaidai serikali zaidi ya sh. bilioni nane, ikiwa ni malimbikizo ya madeni.
Hata hivyo, serikali imesema kiasi hicho ni kidogo ikilinganishwa na madai yaliyokuwepo awali, ambapo watumishi walikuwa wakiidai serikali fedha nyingi.
Hayo yameelezwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani, ambapo alisema jitihada zinaendelea kufanywa ili kumaliza deni hilo.
Alikuwa akijibu swali la Masoud Abdalla Salim (Mtambile- CUF), ambaye alitaka kufahamu kuhusiana na malimbikizo na madeni ya askari.
Salim alisema serikali inaweza kuwaepusha askari na watumishi wa umma na vitendo vya rushwa kwa kuwalipa madeni.
ìWaziri umesema kuna wimbo wa maadili wa askari ambao wanatakiwa kuimba kila siku, wimbo huo utaimbwa na utaendelea kuimbwa kila siku, suala hapo ni madeni na mishahara ambayo askari wanaidai serikali,î alisema.
Celina alisema asilimia kubwa ya madeni tayari yamelipwa, ambapo alisema kwa sasa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inadaiwa sh. milioni 800.
Hata hivyo, alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu, deni hilo litakuwa limelipwa.
Awali, Mwanahamisi Kassim (Viti Maalumu-CCM), alihoji sababu zinazochukuliwa na serikali baada ya kuwafukuza kazi askari waliotiwa hatiani kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Naibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, alikiri kuwa baadhi ya askari kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuwa, hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Kwa kipindi cha Januari mwaka jana na Septemba, mwaka huu, askari 54 walituhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, kati yao 19 walifikishwa mahakamani na 34 hatua mbalimbali za kinidhamu, ikiwemo kufukuzwa kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi.

1 comments:

  1. Hongela selikari kwa kujalibu kumaliza madeni ya wafanyakaz

    ReplyDelete