Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Pata mafanikio, tangaza hapa

Tangaza nasi hapa.

Tuesday, 27 August 2013

Mabadiliko CCM

Na HAMIS SHIMYE, DODOMA
HALMASHAURI Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, imefanya mabadiliko makubwa kwa lengo la kuimarisha safu ya uongozi kwa kuteua makatibu wapya 28.
Katika orodha hiyo, makatibu 25 watapangiwa kazi wilayani na watatu wameteuliwa kujaza nafasi za mikoa zilizoachwa wazi.
Mabadiliko hayo pia yatawakumba makatibu wakuu wa jumuia za Chama, ambapo tayari aliyekuwa Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Sixtus Mapunda, amependekezwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Kwa sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Martine Shigela, ambaye alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Francis Issack.
Wengine waliopendekezwa kuchukua nafasi za ukatibu mkuu kwenye jumuia hizo ni Amina Makilagi (UWT), ambaye anashika nafasi hiyo kwa sasa na Seif Shabani Mohamed atakayemrithi Khamis Suleiman Dadi.
Pamoja na mabadiliko hayo, NEC pia imemvua uanachama Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Mansoor Yussuf Himid (Kiembesamaki -CCM), kutokana na kukisaliti na kuikana Ilani ya uchaguzi.
Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema NEC imefanya mabadiliko hayo kwa lengo la kuongeza nguvu na kukiwezesha Chama kuendelea kushika dola.
Alisema baada ya uteuzi huo makatibu hao watapangiwa kazi katika wilaya mbalimbali hapo baadaye.
Aliwataja makatibu wa mikoa walioteuliwa kuwa ni pamoja na Mary Maziku, Kassim Mabrouk Mbaraka na Romuli Rojas John.
Kwa upande wa makatibu wa wilaya walioteuliwa ni Ashura Amanzi, Rukia Said Mkindu, Elias Mpanda, Jonathan Mabihya, Mulla Othaman Zuber, Jumanne Kapinga, Ali Hajai Makame, Jacob Makune, Juma Mpeli na Hawa Nanganjau.
Wengine ni Abdulrahman Shake, Subira Mohamwed Ameir, Abdalla Shaban Kazwika, Juma Bakar Nachembe, Josephat Ndulango, Rajab Uhonde, Abeid Maila, Mohamed Lawa, Mariam Sangito Kaaya na Bakar Lwasa Mfaume.
Kwa mujibu wa Nape wengine ni Julius Peter, Jumanne Kitundu Mginga, Mathias Nyombi, Agness Msuya na Mohamed Hassan Moyo.
Kuhusu makatibu wakuu wa jumuia za Chama, Nape alisema baada ya mapendekezo hayo watapelekwa kwenye mabaraza ya jumuia husika kwa ajili ya kuthibitishwa.
"Tumemaliza vizuri mkutano wetu wa Halmashauri Kuu kwa mafanikio makubwa kwani, hoja zote zilijadiliwa kwa kina na kuyapatia majibu," alisema.
Kuhusu kuvuliwa uanachama kwa Mansoor, alisema NEC imefikia hatua hiyo baada ya kujadili kwa kina tuhuma mbalimbali za mwakilishi huyo katika mkutano wake.
Alisema baada ya kupitia kwa kina tuhuma hizo, Halmashauri Kuu Taifa imebariki mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi Zanzibar ya kumvua uanachama.
Alisema kufuatia hali hiyo NEC imebariki mapendekezo hayo na kwamba, kuanzia jana Mansoor si kiongozi tena wa CCM.
Nape alisema kufuatia uamuzi huo wa halmashauri Kuu kubariki kuvuliwa uanachama, mwakilishi huyo hana nafasi ya kukata rufaa sehemu yeote katika chama.
"Huu ndio uamuzi wa mwisho na mwakilishi huyo, hana nafasi tena ya kukata rufaa juu ya uamuzi huo wa NEC,'' alisema.
Akizitaja tuhuma zake, Nape alisema Mansoor alishindwa kusimamia malengo ya CCM, kutekeleza masharti ya uanachama na kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka maadili ya viongozi. 
"Kutokana na mjadala mzito kamati Kuu imebariki mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi Zanzibar ya kumvua uanachama wa CCM na kuanzia sasa si mwanachama wa CCM wala kiongozi wa CCM" alisema Nape.

Thursday, 22 August 2013

Mtikisiko Jeshi la Polisi


NA SELINA WILSON
MAOFISA wanne wa Jeshi la Polisi, wamevuliwa madaraka na mmoja amesimamishwa kazi kutokana na kushindwa kuwajibika katika mambo ya msingi na kusababisha uhalifu kutokea.
Licha ya hao, askari watatu wamefukuzwa kazi wakituhumiwa kushirikiana na matapeli kumbambikia fuvu mfanyabiashara, mkazi wa Dumila, Samson Mwita, kwa lengo la kujipatia fedha.
Wakati hayo yakifanyika, ofisa mwingine amepandishwa cheo kwa kuanika madudu ya askari wenzake.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa mkakati wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wa kusafisha Jeshi la Polisi na kujenga nidhamu miongoni mwa askari.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya uchunguzi wa kamati ya watu watatu aliyoiunda kuchunguza matukio mbalimbali yaliyotokea hivi karibuni.
Alisema wizara inaendelea kupambana na askari wanaochafua jina la jeshi hilo na kwamba, halitamvumilia yeyote atakayebainika kwenda kinyume cha utaratibu wa kinidhamu wa jeshi hilo.
Dk. Nchimbi alisema waliofukuzwa kazi na kushitakiwa ni askari E 4344 Sajini Mohammed, E 3861 Koplo Nuran wa kituo cha polisi Dumila na Sajini Sadick Madodo wa kituo cha polisi Dakawa, mkoani Morogoro, ambao walishirikiana na matapeli Rashid Shariff na Adam Peter, kumbambikia fuvu Mwita.
Alisema Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mvomero, Inspekta Jamal Ramadhan, Mkuu wa Kituo cha Polisi Dumila, Inspekta Juma Mpamba na Mrakibu Msaidizi (ASP), Daniel Bendarugaho, wamevuliwa madaraka kutokana na tukio hilo.
Dk. Nchimbi alisema Inspekta Jamal alishindwa kuchukua hatua dhidi ya askari hao, ambao walimweleza kuna dili la kupata fedha, ambalo alikataa kushiriki lakini hakuchukua hatua dhidi ya askari na uhalifu ukafanyika.
Pia anadaiwa kushindwa kumkamata mtuhumiwa wa utapeli Adam Peter, aliyekuwa kinara wa tukio hilo. Hata hivyo, alisema kamati ya uchunguzi ilimshinikiza kumkamata.
Waziri alisema Inspekta Mpamba wa Kituo cha Dumila amechukuliwa hatua kutokana na kuonyesha udhaifu katika utendaji kazi, kwa kutosimamia kikamilifu askari wa chini yake.
Kutokana na hilo, alisema  amesababisha kutengeneza kesi ya fuvu la binadamu ili kujinufaisha kinyume cha maadili ya kazi.
Wengine waliovuliwa madaraka ni Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Arusha, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Ramadhani Giro, na Mrakibu Msaidizi (ASP), Daniel Bendarugaho, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma.
Alisema ASP Bendarugaho amevuliwa madaraka kutokana na tukio la mauaji la Desemba 25, mwaka jana, lilitokea katika kituo cha polisi Heru Ushingo, wilayani Kasulu, ambapo askari D 8622 Koplo Peter na G 1236 Konstebo Sunday, walimpiga Gasper Sigwavumba (36) na kumweka mahabusu. Alikufa siku moja baadaye.
Waziri Nchimbi alisema ASP Bendarugaho akiwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kasulu, hakuwa makini katika kusimamia upelelezi wa jalada la kesi kuhusu mauaji ya Sigwavumba, hivyo kuvuliwa madaraka. Alisema upelelezi wa tukio hilo utaanza upya.
Kuhusu Mkuu wa FFU Arusha, ASP Giro, alisema katika tukio la Mei 18, mwaka huu, askari wawili wa kituo cha Ngarenanyuki, wilayani Arumeru, walifukuzwa kazi baada ya kukiri kusafirisha bangi kwa kutumia gari la polisi namba PT 2025, aina ya Toyota Land Cruiser.
Alisema mkuu wa kikosi hicho kwenye mkoa ndiye mwenye mamlaka ya kupanga matumizi ya magari, lakini alishindwa kuyadhibiti na kusababisha litumie kusafirisha kilo 540 za bangi, zenye thamani ya sh. milioni 81 na kukamatwa mkoani Kilimanjaro.
Dk. Nchimbi alisema kutokana na hilo, ASP Giro, amevuliwa madaraka kwa kushindwa kuwasimamia ipasavyo askari na maofisa walio chini yake na kusababisha uhalifu kutokea.
Alisema ofisa aliyesimamishwa kazi ni Inspekta Isaack Manoni, ambaye ameagiza ashitakiwe kijeshi kwa tuhuma za kumtorosha askari F 1734 Koplo Edward, aliyekuwa dereva wa gari la polisi lililokamatwa na bangi.
Dk. Nchimbi alisema Inspekta Manoni alitakiwa kumpeleka askari huyo kukabidhi vifaa vya Jeshi la Polisi, lakini alizembea na kusababisha mtuhumiwa kutoroka.
Alisema Inspekta Salum Kingu, amepewa onyo kwa kuzembea katika tukio hilo, kwani alidaiwa kubaki kwenye gari umbali wa kilomita 80 kutoka nyumba ya mtuhumiwa kitendo ambacho kilichangia atoroke.
Waziri alisema Inspekta Mikidadi Galilima, naye amepewa onyo kwa kutotimiza wajibu wake katika kumshauri Mkuu wa FFU wa Arusha katika ukaguzi na usimamizi wa rasilimali za kikosi na kufichwa ukweli baada ya Koplo Edward kuiba magurudumu ya gari la polisi na kuweka ya zamani, jambo ambalo ni kosa kwa kiongozi.
Waziri Nchimbi alisema Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Francis Duma, aliyekuwa kiongozi katika tukio la kukamata gari la Jeshi la Polisi lilibeba bangi mkoani Kilimanjaro, amepandishwa cheo.
Dk. Nchimbi ameagiza askari wengine 14 walioshirikiana naye wapewe zawadi inayostahili na Mkuu wa Jeshi la Polisi Said Mwema.
0000

Jiji kuuza hisa zake UDA


Na Joseph Damas
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam, inatarajia kuuza hisa zake zilizoko katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Hatua hiyo imefikiwa jana katika kikao maalumu cha madiwani wa Jiji la Dar es Salaam na kwamba, hisa hizo zitauzwa kwa bei ya soko kulingana na mahitaji halisi.
Hata hivyo, haijaweka bayana hisa hizo zitauzwa kwa kampuni gani na kwamba, mchakato  utatangazwa na utakuwa wa wazi.
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Massaburi, alisema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao kilichoketi jana na kwamba, umelenga kuliwezesha jiji kuondokana na mvutano, ukiwemo wa madeni yanayolikabili UDA.
Alisema jiji litauza hisa zake kwa kati ya sh. 1,600 na sh. 2,600 tofauti na bei ya awali aliyouziwa mwekezaji Kampuni ya Simon Group Ltd.
Dk. Massaburi alisema iwapo Simon Group itahitaji kununua hisa hizo, italazimika kulipa tofauti ya bei ya awali.
Awali, Simon Group ilinunua hisa ndani ya UDA kwa bei chee, hivyo kuzusha mgogoro, uliomuhusisha Mwenyekiti wa UDA, Iddi Simba.
Dk. Massaburi alisema UDA  inakabiliwa na madeni makubwa, ambapo baadhi ya wadai wamefungua mashitaka mahakamani.
Alisema UDA inakabiliwa na madeni yanayofikia sh. bilioni 78 na kwamba, iwapo wahusika watashinda itakuwa mzigo mkubwa kwa jiji.
Meya huyo alisema Jiji la Dar es Salaam litakuwa na mradi mkubwa wa mabasi yaendayo haraka, hivyo UDA haitahitajika mradi huo utakapokamilika.

LAAC yabaini upotevu wa 1.2bil/- Mvomero


Na Mohammed Issa
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imegundua upotevu wa sh. bilioni 1.2 katika Halmashauri ya Mvomero, mkoani Morogoro.
Kutokana na hilo, kamati imemuita aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Sara Niluma, na aliyekuwa Mweka Hazina, Kabilile Stim, kufika mbele yake kueleza jinsi fedha hizo zilivyotumika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa LAAC, Seleman Zedi, alisema fedha hizo haijafahamika zimepelekwa wapi.
Kwa mujibu wa Zedi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alipofanya ukaguzi kwenye halmashauri hiyo, alibaini kiasi hicho cha fedha kilitumika bila kuonyeshwa zimetumikaje. Fedha hizo ni za mwaka 2011/2012.
Kutokana na upotevu wa fedha hizo, kamati imeamua kumuita Sara, ambaye amestaafu na Stim, ambaye ni Mweka Hazina wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, ili waeleze fedha hizo zilikwenda wapi.
Zedi alisema wajumbe wa kamati wamebaini kuna matumizi ya fedha yasiyofaa katika halmashauri hiyo.
Alisema fedha zilizopelekwa kwa ajili ya kinamama na vijana zilitumika vibaya na kwamba, kamati inapiga marufuku fedha hizo kutumika kwa matumizi yasiyokusudiwa.
Makamu mwenyekiti alisema kamati inamtaka mkandarasi aliyekuwa akijenga ofisi ya mkurugenzi kurudisha fedha zilizozidi.
Alisema kamati inaiomba halmashauri kuongeza uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 10.

Kamati Kuu CCM kujadili ya Bukoba


Na Theodos Mgomba, Dodoma
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, inaanza kikao leo mchana, mjini hapa, ambayo pamoja na mambo mengine itajadili suala la madiwani wanane wa Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera.
Kikao hicho kitafanyika chini ya  Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete. Kesho  Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), itaanza kikao cha siku mbili.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema ajenda kubwa ya kikao hicho itakuwa kupitia maoni ya wana-CCM kuhusu Rasimu ya Katiba mpya na suala la madiwani wa Bukoba, ambao walivuliwa uanachama na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera, ambapo Chama kimewataka waendelee na kazi.
Nape alisema awali, kamati ilitarajiwa kuanza kikao asubuhi, lakini kimeahirishwa hadi mchana kutokana na mwenyekiti wa Chama kuwa nje ya nchi.
“Ilikuwa tuanze asubuhi lakini mwenyekiti yuko Zimbabwe, katika sherehe za kuapishwa Rais Robert Mugabe, hivyo atakuja mchana ndipo tutaanza kikao,” alisema.
Alisema moja ya ajenda kubwa ni kupitia maoni ya wana-CCM kuhusu rasimu ya kwanza ya katiba, ambayo yalikusanywa kuanzia ngazi ya matawi na sasa yatapitiwa ngazi ya taifa.
Katibu huyo alisema baada ya maoni hayo kujadiliwa na Kamati Kuu, yatapelekwa NEC, ambayo itatengeneza taarifa itakayowasilishwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Tofauti yetu na wenzetu, sisi tumeshirikisha wanachama, wenzetu mmeona wanakwenda kwenye mikutano ya hadhara. Tunashukuru Jaji Warioba alisema hadharani kuwa hatapokea maoni ya mikutano ya hadhara, ambapo kwa kweli sheria ilitaka watu watumie mabaraza ya taasisi,” alisema.
Nape alisema kufanyika mikutano ya hadhara kunawapotezea wananchi muda na kuwahadaa Watanzania bila sababu.
Alisema CCM imeonyesha mfano wa jinsi ya kupata maoni kwa kushirikisha wanachama katika kujadili rasimu hiyo.
Nape alisema ajenda nyingine ni hali ya kisiasa nchini, na masuala ya utumishi, ambazo ni za kawaida ndani ya Chama.
Katika hatua nyingine, alisema CCM itazindua Baraza la Ushauri la Wazee wa Chama Jumapili wiki hii. Alisema baraza hilo litawashirikisha wenyeviti wote wastaafu wa CCM na makamu wao.

Ajali ya ndege yajeruhi saba


Na LILIAN JOEL, ARUSHA
ABIRIA saba waliokuwa wakisafiri kwa ndege ndogo kutoka Bukoba kwenda jijini Dar es Salaam, kupitia Zanzibar, wamenusurika kifo baada ya ajali kutokea.
Ndege hiyo ilianguka jana ndani ya Ziwa Manyara, baada ya kupata hitilafu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Libaratus Sabas,  alithibitisha kutokea ajali hiyo, akisema ilitokea jana mchana.
Akizungumza kwa simu, Sabas alisema majeruhi waliokolewa na boti za wavuvi na kupelekwa Hospitali ya Rufani ya Selian, jijini Arusha kwa matibabu.
Kamanda Sabas alisema alipokuwa akizungumza hakuwa na orodha ya majina ya abiria waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.
Hata hivyo, habari zilizopatikana hospitalini zinasema miongoni mwa abiria wa ndege hiyo ni wakili kutoka Kampuni ya IMMA ya jijini Dar es Salaam, Protas Ishengoma, ambaye ni miongoni mwa majeruhi wanne waliopata majeraha madogo.
Abiria mwingine ni Meeda Naburi na aliyetambulika kwa jina moja la Kashasha.
Majeruhi sita kati ya saba wa ajali hiyo walipelekwa hospitali kwa kutumia helikopta iliyokodiwa na baadhi ya mawakili wa jijini Arusha na ndugu wa majeruhi.
Akizungumza kwa simu kutoka eneo la tukio, kabla ya kusafirishwa hadi jijini Arusha kwa matibabu, Naburi alisema kabla ya ajali, rubani aliwataarifu kuwa injini moja kati ya mbili za ndege hiyo ilipata hitilafu.
Samuel Rugemalila, aliyejitambulisha kuwa ndugu wa majeruhi, akizungumza na waandishi wa habari akiwa hospitali, alisema abiria hao walikuwa wakitoka msibani Bukoba.
“Kwa mujibu wa maelezo ya majeruhi, injini moja ilipata hitilafu wakiwa umbali wa futi 21 kutoka usawa wa bahari, ndipo rubani alipofanya jitihada za kutua kwa dharura kwenye uwanja mdogo wa Manyara, kabla ya injini ya pili kuzima wakiwa futi 14 kutoka usawa wa bahari,” alisema.
Rugemalila alisema rubani alipogundua kuwa ndege isingetua salama katika uwanja huo, aliamua kutua ndani ya maji kwenye Ziwa Manyara.
“Tunamshukuru Mungu ndugu zetu wako salama licha ya kupata majeraha madogo. Kwa mujibu wa maelezo ya madaktari, maisha yao hayako hatarini,” alisema.
Ajali hiyo imetokea ikiwa ni wiki chache baada ya nyingine iliyohusisha ndege ya madaktari wasio na mipaka (Flying Doctors) kuanguka wilayani Ngorongoro.

Kikwete: Mazingira ya uwekezaji kuboreshwa


NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete, amesema serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha mazingira ya kufanyia biashara ili kutoa fursa kwa wawekezaji kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
Alisema hayo wiki hii, mjini Dar es Salaam, katika hafla maalumu ya kukabidhi tunzo kutambua mchango wa taasisi zinazohusika na shughuli za uchimbaji madini na nishati nchini.
Rais Kikwete alisema kwa muda mrefu kumekuwepo na manung’uniko kutoka kwa baadhi ya watu wanaodai rasilimali za taifa kutosaidia maendeleo ya nchi, lakini serikali imejitahidi kufanyia kazi eneo hilo na kuleta mabadiliko.
Alisema moja ya hatua zilizochukuliwa na serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji ni kusimamia amani na ustawi wa nchi, unaotoa fursa kwa wawekezaji kuendesha shughuli zao kwa mafanikio.
Kuhusu tunzo hizo, alisema zimebuniwa maalumu kwa ajili ya kuzihamasisha kampuni zinazohusika na sekta hizo kuongeza ushiriki katika maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema kampuni za uchimbaji madini na zile za nishati zimeongeza ushiriki katika maendeleo ya huduma mbalimbali za kijamii.
Profesa Muhongo alisema tunzo hizo zilizohusisha vyeti na ngao maalumu ni kielelezo cha ushiriki wa kampuni hizo katika maendeleo ya jamii kupitia miradi ya miundombinu, kuchangia huduma za afya, elimu, maji, ajira na uwezeshaji.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alisema kampuni 14 zilihusishwa kwenye mchakato wa kuwapata washindi, ambao ni kampuni zinazojitoa zaidi kwenye huduma mbalimbali za kijamii.
Maswi alisema baada ya tunzo hizo kuzinduliwa na Rais Kikwete mwaka jana, liliundwa jopo la majaji saba waliozunguka kwenye maeneo mbalimbali na hatimaye kuwapata washindi.
Washindi wa jumla wa kwa kampuni zenye mtaji mkubwa ni mgodi wa almasi wa Williamsons na migodi ya dhahabu ya Geita (GGM) na Bulyanhulu.
Kwa upande wa kampuni zenye mtaji wa kati, washindi wa jumla ni Kiwanda cha Saruji Mbeya, Tanzanite One na Kiwanda cha Saruji cha Twiga.

Trafiki bandia apanda kizimbani


NA SYLVIA SEBASTIAN, DSJ
MKAZI wa Kimara, Dar es Salaam, James Hassan, aliyekuwa akishikiliwa polisi, akituhumiwa kujifanya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, amepandishwa kizimbani kujibu mashitaka hayo.
Hassan (45), alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, akikabiliwa na mashitaka mawili ya kujifanya mtumishi wa umma na kukutwa na sare za Jeshi la Polisi.
Wakili wa Serikali Nassoro Katuga, alimsomea mshitakiwa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakamani hiyo, Joyce Minde.
Katuga alidai Agosti 14, mwaka huu, eneo la Kinyerezi, Mnara wa Voda, mshitakiwa kwa njia ya udanganyifu alijitambulisha kwa Inspekta wa Polisi Gabriel Chiguma, kuwa ni askari wa usalama barabarani.
Katika shitaka la pili, Hassan anadaiwa siku hiyo, kwa njia ya udanganyifu, alikutwa akiwa na sare za polisi, ambazo ni kofia, jaketi na mkanda.
Mshitakiwa alikana mashitaka, ambapo Katuga alidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Hassan aliomba dhamana, ambapo Hakimu Joyce, alitaja masharti kuwa, awe na wadhamini wawili wenye makazi ya kudumu, watakaotia saini dhamana ya maandishi ya sh. milioni saba.
Mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo, hivyo alipelekwa rumande. Kesi itatajwa Septemba 5, mwaka huu.

Wednesday, 21 August 2013

Wabunge waibua madudu Ardhi


NA KHADIJA MUSSA
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali imegundua madudu katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambapo viwanja 7,800 nchini havina wamiliki.
Kati ya viwanja hivyo, 160 vyenye thamani ya sh. milioni 500 viko Dar es Salaam.
Kutokana na hilo, kamati hiyo imemuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu katika wizara hiyo ili kujua undani wa viwanja hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe, alisema viwanja hivyo wamiliki wake hawajulikani licha ya kuweko katika orodha ya wizara.
Zitto alisema sababu nyingine ya kuomba ukaguzi maalumu ni kutofikiwa malengo yaliyowekwa na serikali ya kukusanya sh. bilioni 99 katika bajeti ya mwaka 2012/2013, ambapo zilikusanywa sh. bilioni 20 tu.
“Baada ya wizara kuona imeshindwa kufikia malengo katika ukusanyaji fedha, iliamua kuongeza kodi na bei ya viwanja jambo ambalo liliwaongezea wananchi mzigo,” alisema.
Kutokana na hilo, alisema kamati imeiagiza wizara kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kuanzisha mfumo wa kidijitali utakaowezesha hati zote kutolewa kama zilivyo leseni za udereva.
Zitto alisema kamati ina imani kupitia mfumo huo, ambao kila mmiliki atatambulika kupitia namba ya mlipakodi utawezesha kuondoa migogoro ya ardhi iliyoko sasa, ikiwemo ya hati tatu kutolewa kwa kiwanja kimoja.
Katika hatua nyingine, kamati imetaka maelezo kutoka Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, kutokana na kutotumika mfumo wa kielektroniki wa utoaji wa risiti za malipo yanayotokana na makosa ya madereva wa magari.
Imekiagiza kikosi hicho kuwasilisha taarifa mbele ya kikao cha kamati kitakachofanyika Septemba 10, mwaka huu, mjini Dodoma.
Zitto alisema muda umepita tangu mfumo huo uanzishwe na vifaa vya utekelezaji wa kazi kununuliwa na serikali, lakini askari wa kikosi hicho wanatumia mfumo wa kizamani kutoa stakabadhi.
Alisema kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kama mfumo huo ungetumika ungeiwezesha serikali kuingiza sh. bilioni 55, tofauti na ilivyo sasa ambapo wanakusanya sh. bilioni 15 kwa mwaka.

Kituo cha Ubungo ‘kuzaa’ viwili


NA SELINA WILSON
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kujenga vituo viwili vya mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani, inayokadiriwa kugharimu sh. bilioni 40.
Ujenzi wa vituo hivyo, unafuatia kubadilishwa kwa matumizi ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo, ambacho kinafanyiwa ukarabati kwa ajili ya mabasi yaendayo haraka.
Msemaji wa Jiji Gaston Makwembe, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mjini Dar es Salaam.
Makwembe, alisema vituo hivyo vitajengwa katika maeneo ya Mbezi Luis na Boko Basihaya, ambapo vitatoa huduma kwa kanda.
Alisema kituo cha Boko Basihaya, kitahuduma wasafiri wanaokwenda mikoa ya kanda ya Kaskazini na cha Mbezi Luis kitahudumia wasafiri wanaoelekea mikoa ya kanda ya Kati, Nyanda za juu.
Kwa upande wa abiria wanaokwenda mikoa ya Kusini watajengewa kituo cha mabasi katika eneo la Kongowe baada ya kukamilishwa kwa awamu ya kwanza ya vituo vya Mbezi Luis na Boko Basihaya.
Alisema kwa sasa wapo katika mchakato wa kufanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kupata gharama halizi za utekelezaji wake  na kubaini vyanzo vya fedha.
Makwembe, alisema Halmashauri ya Jiji imepanga kushirikiana na taasisi mbalimbali za fedha na wawekezaji wanao onyesha nia ya kushirikiana katika ujenzi wa vituo hivyo.
Kwa upande wake Meneja wa Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo, Juma Idd, alisema wakati wa maandalizi ya ujenzi wa vituo hivyo, kituo hicho bado kitaendelea kutoa huduma kwa wasafiri wa mikoani na nchi jirani.
Akizungumzia ukarabati wa kituo hicho kwa ajili ya kuhudumia mabasi yaendayo haraka, Iddi alisema eneo hilo pia litajengwa maduka makubwa na hoteli.

Watuhumiwa mauji ya Msuya kizimbani


NA MWANDISHI WETU, MOSHI
WATU watatu wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na shitaka la kumuua mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya (43).
Washitakiwa hao ni Sharifu Mohammed mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Mpungi, mkazi wa Kijiji cha Songambele na Musa Mangu mkazi wa Shagarai kwa Mrefu, mkoani Arusha.
Mohammed na wenzake walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, mbele ya Hakimu Mkazi Munga Sabuni.
Wakili wa Serikali Stella Majaliwa, alidai kuwa washitakiwa hao walimuua Msuya kwa kukusudia.
Hata hivyo, washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Kwa upande wake wakili wa utetezi Lucie Paul, alidai mahakamani hapo kuwa wateja wake walikamatwa Agosti 12, mwaka huu, wamekaa rumande bila ya kupewa fursa ya kuwasiliana na ndugu zao au wakili, jambo ambalo si haki.
Msuya aliuawa Agosti 7, mwaka huu, saa 6.30 mchana, kwa kupigwa risasi kando ya barabara kuu ya Arusha – Moshi, katika eneo la Mjohoroni, wilayani Hai, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Kesi hiyo itatajwa Septemba 4, mwaka huu.

Waliojitoa NSSF walipwa mafao


NA MWANDISHI WETU
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umelipa mafao yenye thamani ya sh. bilioni 199 kwa wanachama wake mwaka uliopita wa fedha.
Asilimia 70 ya fedha hizo, imeelezwa kuwa  zimelipwa kwa wanachama waliojitoa.
Pia, thamani ya NSSF imeendelea kupanda na kufikia trilioni 2.6 na pia, inawekeza sh.bilioni 950 kila mwaka.
Hayo yalisemwa na Meneja Kiongozi, Idara ya Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa NSSF, Eunice Chiume, alipozungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jana.
Alisema fedha hizo zimelipwa kwa ajili ya mafao mbalimbali kwa wanachama wake ikiwemo wanaojitoa kwa sababu mbali mbali ikiwemo kuacha kazi.
Alipoulizwa kuhusu watu kujitoa, alisema hali hiyo inatokana na uelewa duni juu ya hifadhi ya jamii kuhusiana na suala ambalo ni changamoto kubwa kwa taifa.
“Wengi hawana uelewa juu ya hifadhi ya jamii, mwanachama hata akiacha kazi eneo moja, anaweza kuendelea kuwa mwanachama na akahama na namba yake anapoajiriwa mahali pengine,” alisema.
Hata hivyo, alisema NSSF hakuna changamoto yoyote kwa lakini kwa taifa ni tatizo kubwa kwa sababu, wote wanajitoa ndio hao watakaokuja kuhitaji pensheni ya uzeeni, ambayo imeanza kuzungumzwa itolewe kwa wazee wote hata wasiojiwekea akiba.
“Yaani kitakachotokea ni kwamba, wanaojitoa sasa, wakizeeka itabidi kodi na michango ya wengine, itumike kuwalipa mafao, jambo ambalo ni mzigo mkubwa,”alisema.
Akizungumzia kuhusu uwekezaji, Eunice alisema NSSF kwa mwaka huu wa fedha, inatarajia kuwekeza sh. bilioni 951 .4.
Alisema sawa na ongezeko la asilimia 21 ikilinganishwa na mwaka uliopita wa fedha, ambapo iliwekeza sh. bilioni 751.4.
Kwa mujibu wa Eunice, NSSF imekuwa ikiwekeza kwenye miradi mikubwa hapa nchini na mingi ni ya serikali na urejeshaji wake ni wa uhakika.
Alitoa mfano wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambapo serikali imeshaanza kurejesha sh. bilioni 14 kwa mujibu wa mkataba wa mkopo wa bilioni 232.
NSSF kwa mwaka huu, inatarajia kukusanya sh. bilioni 181.1 kutoka kwenye vitega uchumi vyake na inatarajia kulipa sh. bilioni 5.19 kwa ajili ya mafao ya matibabu kwa wanachama wake.

Kero za muungano zaanza kutatuliwa


NA MWANDISHI WETU
KAMATI ya pamoja ya kushughulikia kero za muungano, imefanikiwa kuzipatia ufumbuzi baadhi.
Moja kati ya hoja hizo ni Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu kutofanya kazi Zanzibar kutokana na sheria hiyo kutokuwa suala la Muungano.
Msemaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais Siglinda Chipungaupi, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jana, kuhusu mafanikio ya ofisi hiyo.
Siglinda, alisema sheria hiyo imefanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwemo namba 8 ya 2006 na kuondoa upungufu uliokuwepo na sasa inafanya kazi pande zote mbili.
Alisema hoja nyingine ni ushiriki wa Zanzibar katika Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo nafasi ya Zanzibar kuwasilisha miradi ya maendeleo ya kiuchumi kwa ajili ya kuijumuisha katika miradi ya kikanda ya EAC.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, SMZ iliwasilisha miradi tisa katika miradi ya Tanzania itakayoombewa ufadhili chini ya EAC.
Alisema Wizara ya Afrika Mashariki inaendelea kufuatilia miradi hiyo kwa kushirikiana na sekta husika.
Hoja nyingine iliyopatiwa ufumbuzi ni ya mgawanyo wa mapato yatokanayo na misaada kutoka nje.

Tuesday, 20 August 2013

Mgambo watibua mambo Amana



Na Mwandishi Wetu
TAKRIBAN sh. 700,000 zinazokusanywa kwa mwezi na mgambo katika Hospitali ya Amana, wilayani Ilala, Dar es Salaam, zikidaiwa kuwa ushuru wa maegesho ya pikipiki, hazijulikani zinakokwenda.
Licha ya mgambo kukusanya fedha hizo, si uongozi wa hospitali au Manispaa ya Ilala ulioeleza kuutambua ushuru huo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hospitalini hapo, umebaini mgambo hukusanya fedha hizo bila kutoa stakabadhi, zaidi ya kuorodhesha namba za usajili wa pikipiki kwenye karatasi.
Mgambo hao hutoza sh. 500 kwa kila pikipiki inayoingia hospitalini  hapo, wakidai ni maelekezo kutoka kwa wakubwa wao, ambao hata hivyo, hawakuwa tayari kuwataja.
Ofisa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema manispaa haina taarifa za kutozwa ushuru huo.
“Hilo silifahamu, naahidi kulifuatilia na kutoa taarifa sahihi,” alisema.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Meshack Shimwela, alisema uongozi wa hospitali hauhusiki na tozo hiyo na hauifahamu.
Alisema iwapo kuna utaratibu huo, wanaokusanya ushuru wanafanya hivyo kwa utashi wao bila uongozi wa hospitali kujua.
“Vyombo vyote vya moto vinatakiwa kuingia na kutoka bila kulipia, kama kuna mtu anawatoza watu ushuru, uongozi wa hospitali hauhusiki na  haufaidiki na chochote,” alisema.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Asha Mahita, alisema utaratibu huo hauruhusiwi na haupo kisheria.
Alisema inawezekana wanaotoza fedha hizo wanafanya hivyo kwa maslahi binafsi, na kwamba mtu yeyote hatakiwi kulipia ushuru wa chombo cha usafiri anapoingia hospitalini na kama atalipishwa  apatiwe risiti.
“Hilo ni tatizo haiwezekani mtu alipie huduma bila ya kupewa risiti, kwani sheria ndivyo inavyoelekeza,” alisema.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa nyakati tofauti wiki iliyopita umebaini kati ya saa 12 asubuhi hadi saa sita mchana, takriban pikipiki 56 huingia hospitalini hapo.
Kwa idadi hiyo, sh. 28,000 hukusanywa asubuhi kwa siku, licha ya zingine zinazoingia mchana na jioni. Kwa utaratibu huo, kwa wiki kuna uwezekano wa kukusanywa sh. 196,000 na kwa mwezi sh. 784,000.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia utozwaji ushuru huo, walisema wanashangazwa na kuhoji iwapo upo kisheria, kwani hospitali zingine hawatozwi.
“Hili tunalofanyiwa ni dhuluma na wizi, wanachukua fedha bila  kutoa stakabadhi, wakati utaratibu wa serikali unaelekeza kila anayelipia huduma apewe stakabadhi.
“Magari yanaingia na kutoka bila kulipa hata senti tano, kwa nini ushuru huu uwe ni kwa pikipiki tu, na ukitoka ukaingia tena unalipa,” alisema dereva wa pikipiki Yussuf Makame, mkazi wa Vingunguti.
Issa Saidi, mkazi wa Kigamboni, alisema mgambo wamekuwa wakiwatoza ushuru bila kuwapatia risiti, hiyo kuna shaka kuwa fedha hizo wanazitumia kwa maslahi binafsi.

Dk. Sheni abadili muundo wa Baraza la Mawaziri



Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Dk. Ali Mohammed Sheni, amefanya marekebisho katika muundo na majukumu ya baadhi ya wizara za serikali yake.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, ilisema kwa marekebisho hayo baadhi ya shughuli za wizara zimeunganishwa na kuundwa wizara mpya, na baadhi zimehamishiwa wizara nyingine.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilieleza marekebisho hayo hayakuongeza idadi ya wizara ambapo serikali ya Zanzibar itaendelea kubaki na wizara 16.
Kutokana na marekebisho hayo, shughuli za Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, zimeondolewa katika ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kuundwa wizara mpya.
Shughuli za utawala bora zimeondolewa kutoka Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuhamishiwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, huku shughuli za kazi zikiunganishwa na shughuli za utumishi na kuundwa wizara mpya.
Aidha shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika zimeondolewa kutoka Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika na kuunganishwa na shughuli za Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto.
Shughuli za Tume ya Mipango zimeondolewa kutoka Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na kuhamishiwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na Idara ya Uratibu wa shughuli za SMZ  Dar es Salaam, imeondolewa kutoka Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo na kuhamishiwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais.
Wizara mpya zilizoundwa kufuatia marekebisho hayo ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Wizara ya Fedha, na Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto.
Kutokana na kuundwa kwa Wizara hizo mpya, Rais Dk. Sheni  amefanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri na Watendaji Wakuu wa Wizara kwa kuwabadilisha wizara baadhi ya mawaziri, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu.
Katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora anakuwa Dk. Mwinyihaji  Makame, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora anakuwa Salum Maulid Salum, na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora ni Said Abdulla Natepe.
Katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ anakuwa Haji Omar Kheri, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ ni Joseph Abdalla Meza, wakati Naibu Katibu Mkuu (Tawala za Mikoa) ni Mwinyiussi A. Hassan na Naibu Katibu Mkuu (Idara Maalum za SMZ) ni CDR Julius Nalimy Maziku.
Katika Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa umma ni Haroun Ali Suleiman na Katibu Mkuu  Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma ni Fatma Gharib Bilal, na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Yakout Hassan Yakout.
Katika wizara ya fedha, waziri ni Omar Yussuf Mzee, Katibu Mkuu ni Khamis Mussa Omar, na Naibu Katibu Mkuu ni Juma Ameir Khalid.
Katika Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Waziri ni Zainab Omar Mohammed, Katibu Mkuu wake ni Asha Ali Abdulla na Naibu Katibu Mkuu (Uwezeshaji na Ushirika) ni Ali Khamis Juma na Naibu Katibu Mkuu (Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto) ni Msham Abdulla Khamis.
Viongozi hao waliapishwa jana jioni Ikulu mjini Zanzibar katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali.
00000

Warioba: Hatuhitaji malumbano


Na Hamis Shimye
MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, amesema tume haiko katika malumbano na wanasiasa dhidi ya Rasimu ya Katiba.
Amesema tume iko kwa ajili ya kupata muafaka wa mambo yanayotakiwa yawemo ndani ya katiba mpya.
Jaji Warioba amesema anashangazwa na mikutano ya hadhara inayofanywa na baadhi ya vyama vya siasa, ikidaiwa kuwa ni mabaraza ya katiba, kwa kuwa huu si muda wa kupokea maoni yao.
Alisema hayo jana, alipofungua mkutano wa kitaifa wa baraza la katiba la tasnia ya habari ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Katika mkutano huo, Jaji Warioba alikuwa mgeni rasmi. Aliwataka waandishi wa habari kuijadili kwa umakini na kupendekeza mambo mazuri kwa maslahi ya wananchi.
Alisema waandishi wanapochangia katika rasimu hiyo, wajadili mambo muhimu kuhusu taifa, kwa kuwa kutasaidia kupatikana rasimu bora ya habari itakayolinda maslahi ya taifa.
“Hatupokei maoni, muda wa kupokea maoni ulishakwisha na tume kufanya kazi ya kuchambua maoni hayo, sasa tuna rasimu na kinachotakiwa ni kuijadili kwa kujenga muafaka na si malumbano,’’ alisema.
Alisema waandishi wanapaswa kuchangia kwa umakini ili kusaidia kupatikana katiba bora, kwa kuwa hiyo ndiyo fursa yao na wasingoje kulalamika baadaye.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, rasimu ina mambo mengi ya kujadiliwa, kama vile ardhi, elimu na uchumi, ambayo yanamgusa moja kwa moja mwananchi wa kipato cha chini, ambaye katiba mpya itakuwa mkombozi wake.
Alisema katiba ni jambo la msingi na si la mifarakano, kwa kuwa jamii yote inataka katiba mpya, hivyo waache watu wasikilizwe ili kupatikana kwa mawazo ya pamoja.
Mwenyekiti huyo alisema vyombo vya habari vinapaswa kuwa makini na kuhakikisha habari zinalenga kuielimisha jamii kuhusu rasimu iliyopo na kuachana na habari za kujadili sehemu ndogo ya mgawanyo wa madaraka.

Serikali kuwasilisha taarifa Fao la Kujitoa


Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, inatarajia kupokea taarifa ya serikali kuhusu hatua iliyofikiwa katika marekebisho ya sheria ya Fao la Kujitoa wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jenista Mhagama, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jana, ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam.
Alisema kamati itapokea taarifa ya serikali mjini Dodoma kupitia Wizara ya Kazi na Ajira na kuangalia ni hatua gani iliyofikiwa katika kurekebisha sheria ya mafao ya uzeeni.
Hatua hiyo ilitokana na hoja binafsi iliyowasilishwa na mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jafo, kulitaka Bunge liazimie kuitaka serikali iruhusu fao la kujitoa liendelee.
Awali, kabla ya kuwasilishwa kwa hoja hiyo katika mkutano wa Bunge Novemba, mwaka jana, wafanyakazi na baadhi ya wabunge walilalamikia Sheria ya mwaka 2012 iliyozuia wafanyakazi kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Jenista alisema kazi nyingine inayoendelea kufanywa na kamati ni kupitia muswada wa sheria ya Mfuko wa Akiba ya  Wafanyakazi Serikalini (GEPF).
Alisema muswada huo utakapowasilishwa bungeni utawezesha mfuko huo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, kama ilivyo kwa mifuko mingine, hivyo kuongeza tija.

Tisa wajeruhiwa msafara wa Mwenge



Na Theodos Mgomba, Dodoma
WATU tisa wamejeruhiwa, akiwemo Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Juma Ally Simai (32), baada ya msafara wao kupata ajali katika kijiji cha Fufu, wilayani Chamwino.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Susan Kaganda, alisema jana kuwa, ajali hiyo ilitokea saa 3.30 asubuhi, wakati msafara ukitoka Chamwino kwenda wilayani Mpwapwa.
Alisema Simai amelazwa katika hospitali ya rufani ya mkoa wa Dodoma kwa matibabu.
Susan alisema baada ya msafara kufika katika kijiji hicho, moja ya gari lilifunga breki ghafla, ndipo magari manne yaliyokuwa nyuma yalipogongana.
Aliwataja majeruhi wengine waliolazwa katika hospitali hiyo kuwa, Charles Mamba (39), diwani wa Ipagala, Manispaa ya Dodoma, Dativa Kimolo (46), ambaye ni Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Dodoma na Amina Mgeni (36), muuguzi wa kituo cha afya Makole, Manispaa ya Dodoma.
Wengine waliotibiwa na kuruhusiwa ni Jackline Magoti (39), Richard Mahelela (51), Jumanne Ngede (58), Zaituni Varinoi (43) na Gandula Chimponda (40).
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Zainab Chaula, alisema amepokea majeruhi tisa na hadi jana mchana Simai alikuwa bado amelazwa.
Alisema hali yake inaendelea vizuri na anatarajiwa kuruhusiwa endapo ataendelea hivyo.

UDSM kutoa Shahada ya Sayansi ya Hali ya Hewa


NA RACHEL KYALA
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), imefanikisha kuanzisha kozi ya Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Hali ya Hewa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agness Kijazi, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam.
Dk. Agness alisema mchango wa TMA katika kufanikisha uanzishwaji wa shahada hiyo ni kushiriki katika uandaaji wa mitaala ya kufundishia na kutoa wataalamu wa kufundisha kozi mbalimbali chuoni hapo.
Alisema mamlaka itatoa nafasi ya mafunzo ya vitendo kwa wanachuo, ikiwemo kufanya mazoezi ya kazi kwa mwaka mmoja kwa wahitimu, na kuhakikisha Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), linatambua uanzishwaji wa kozi hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema kuanzishwa kwa mafunzo hayo nchini ni moja ya utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete, na fursa kwa idadi kubwa ya Watanzania, wageni na wafanyakazi wa mamlaka kujiunga na masomo katika taaluma ya hali ya hewa kwa gharama nafuu.
“Kwa upande wa mamlaka, mafunzo hayo yatasaidia kuokoa gharama kubwa ya kati ya sh. milioni 15 na sh. milioni 25 kwa mwaka iliyokuwa ikitumika kusomesha mtaalamu mmoja nje ya nchi, sasa itagharimu sh. milioni moja tu kwa mwaka,” alisema.
Dk. Agness alitoa wito kwa wanafunzi, hususan wa kike kufanya vyema kwenye masomo ya Fizikia na Hesabu ili kukidhi vigezo vya kujiunga na masomo hayo.
Alisema hivi sasa mamlaka ina idadi ndogo ya wafanyakazi wanawake, ambao ni 125  ikilinganishwa na wanaume 449.
Wakati huo huo, alisema TMA imepanua wigo wa ushirikiano na vyombo vya habari, hususan redio za kijamii ili kutoa taarifa za hali ya hewa kwa wakati, zikiwemo za kila siku, za msimu na za tahadhari ya majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi.
Dk. Agness alisema mamlaka imeboresha viwango vya utoaji  taarifa za hali ya hewa kwa asilimia 80, ambapo imezindua njia kadhaa za usambazaji habari, ikiwemo mitandao ya simu za mkononi kwa makundi maalumu, wakiwemo wakulima na wavuvi.
Naye mtaalamu wa hali ya hewa wa mamlaka hiyo, Ladislaus Chang’a, alisema idadi ya watu wanaotumia utabiri wa hali ya hewa kwenye shughuli mbalimbali, hususan wakulima inaongezeka kila mwaka.
Kutokana na hilo, alisema watapata taarifa kutoka serikali za mitaa, kupitia kwa maofisa ugani, ambao watawashauri namna ya kuzitumia ili kuleta kilimo chenye tija.

UDSM kutoa Shahada ya Sayansi ya Hali ya Hewa


NA RACHEL KYALA
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), imefanikisha kuanzisha kozi ya Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Hali ya Hewa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agness Kijazi, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam.
Dk. Agness alisema mchango wa TMA katika kufanikisha uanzishwaji wa shahada hiyo ni kushiriki katika uandaaji wa mitaala ya kufundishia na kutoa wataalamu wa kufundisha kozi mbalimbali chuoni hapo.
Alisema mamlaka itatoa nafasi ya mafunzo ya vitendo kwa wanachuo, ikiwemo kufanya mazoezi ya kazi kwa mwaka mmoja kwa wahitimu, na kuhakikisha Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), linatambua uanzishwaji wa kozi hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema kuanzishwa kwa mafunzo hayo nchini ni moja ya utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete, na fursa kwa idadi kubwa ya Watanzania, wageni na wafanyakazi wa mamlaka kujiunga na masomo katika taaluma ya hali ya hewa kwa gharama nafuu.
“Kwa upande wa mamlaka, mafunzo hayo yatasaidia kuokoa gharama kubwa ya kati ya sh. milioni 15 na sh. milioni 25 kwa mwaka iliyokuwa ikitumika kusomesha mtaalamu mmoja nje ya nchi, sasa itagharimu sh. milioni moja tu kwa mwaka,” alisema.
Dk. Agness alitoa wito kwa wanafunzi, hususan wa kike kufanya vyema kwenye masomo ya Fizikia na Hesabu ili kukidhi vigezo vya kujiunga na masomo hayo.
Alisema hivi sasa mamlaka ina idadi ndogo ya wafanyakazi wanawake, ambao ni 125  ikilinganishwa na wanaume 449.
Wakati huo huo, alisema TMA imepanua wigo wa ushirikiano na vyombo vya habari, hususan redio za kijamii ili kutoa taarifa za hali ya hewa kwa wakati, zikiwemo za kila siku, za msimu na za tahadhari ya majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi.
Dk. Agness alisema mamlaka imeboresha viwango vya utoaji  taarifa za hali ya hewa kwa asilimia 80, ambapo imezindua njia kadhaa za usambazaji habari, ikiwemo mitandao ya simu za mkononi kwa makundi maalumu, wakiwemo wakulima na wavuvi.
Naye mtaalamu wa hali ya hewa wa mamlaka hiyo, Ladislaus Chang’a, alisema idadi ya watu wanaotumia utabiri wa hali ya hewa kwenye shughuli mbalimbali, hususan wakulima inaongezeka kila mwaka.
Kutokana na hilo, alisema watapata taarifa kutoka serikali za mitaa, kupitia kwa maofisa ugani, ambao watawashauri namna ya kuzitumia ili kuleta kilimo chenye tija.

Exim yaadhimisha miaka 16 ya huduma



Mwandishi Wetu
BENKI ya Exim Tanzania imetimiza miaka 16 katika utoaji  huduma za kibenki, ikijivunia mkakati utakaoifanya kuwa bora zaidi nchini katika miaka michache ijayo.
Ilianza kutoa huduma za kibenki nchini Agosti 15, 1997, kwa kuwa na tawi moja jijini Dar es Salaam, ambapo sasa inayo 25 nchini
.
Akizungumza katika maadhimisho yaliyofanyika makao makuu ya benki hiyo, jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu, Dinesh Arora, alisema imejikita katika utoaji huduma za kibenki za kipekee.
Kwa mujibu wa Arora, benki hiyo imeorodheshwa kwenye tunzo za benki bora Afrika, zilizofanyika jijini Marrakesh, Morocco.
“Tutaendelea na jitihada za kutoa huduma. Mafanikio haya katika kipindi hiki yametokana na dhamira yetu ya kutoa huduma za kibenki za kipekee, zitokanazo na wafanyakazi makini na wateja waaminifu,’’ alisema.
Ofisa huyo alisema benki hiyo inaamini ugunduzi ni maisha, hivyo wateja watarajie huduma bora.
Naye Meneja wa Huduma kwa Wateja, Frank Matoro, alisema  maadhimisho hayo yatakuwa chachu ya kuendelea kutoa huduma bora, kwa kuwa kipaumbele cha Exim ni utoaji huduma bora kwa wateja.
Alisema hilo ndilo limeifanya benki kuanzisha huduma ya mawasiliano kwa wateja kupitia mtandao.

Tunu: Wasichana wawezeshwe


Na Mwandishi Wetu
MKE wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda, amesema kuna haja ya kuweka juhudi za makusudi za kuwawezesha wasichana kuhudhuria masomo kila siku.
Amesema kukosekana vifaa vya kujisitiri wakati wa hedhi miongoni mwa wasichana ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wakose masomo kati ya siku 30 na 70 kwa mwaka, jambo linalochangia kudorora kwa elimu miongoni mwao.
Tunu alisema hayo jana, alipozindua mradi wa ‘Hakuna wasichoweza’ katika Shule ya Msingi Chilongola, iliyoko Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara.
Mradi huo unafadhiliwa na Taasisi ya T-MARC, inayojihusisha na masuala ya afya na maendeleo, ukilenga kuwafikia wasichana 10,000 wa Manispaa ya Mtwara Mikindani na Wilaya ya Mtwara Vijijini.
“Wasichana wengi wanapokuwa katika siku zao hushindwa kuhudhuria masomo kati ya siku tatu na saba kwa mwezi, au siku kati ya 30 na 70 kwa mwaka.
“Hii husababishwa na kukosa nyenzo za uhakika za kujisitiri wakiwa shuleni. Wengi wao huamua kubaki nyumbani hadi mizunguko yao itakapokwisha ili kuepuka kuaibika,” alisema.
Alisema usiri na ufahamu mdogo wa jamii kuhusu masuala ya hedhi na changamoto wanazopata wasichana katika kipindi hicho ni tatizo kubwa.
“Wengi wetu katika jamii inayotuzunguka bado tunalichukulia suala la hedhi kuwa la aibu na la siri kubwa, hivyo matatizo yanayotokana na hali hii ya kawaida hubaki bila kushughulikiwa, kwani kila mtu anaona aibu kusema wazi kuwa kuna tatizo,” alisema.
Aliongeza: “Kwa kuwa hedhi haichagui siku maalumu, inawezekana siku hizo zikawa za mitihani au za masomo muhimu. Matokeo yake ni wasichana kukosa vipindi na walimu  hawavirudii.”
Tunu alisema sababu nyingine ni kukosekana majisafi na huduma safi za vyoo, ikiwemo milango ili kulinda heshima ya mtumiaji.
Alisema shule nyingi hazina vyoo vya kutosheleza idadi ya wanafunzi na vichache vilivyopo mara nyingi havina milango, maji na sabuni. Pia alisema hakuna elimu ya kutosha miongoni mwa wasichana walio kwenye umri wa kubalehe.

Jalini kinga badala ya tiba –Dk. Sheni


Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imetoa wito kwa wataalamu wa afya kutoka China, kuangalia kwa kina suala la kinga ya maradhi badala ya tiba wanapokuwa nchini.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni, alitoa rai hiyo alipozungumza na timu ya wataalamu 25 wa afya kutoka Jamhuri ya Watu wa China, waliomtembelea Ikulu, juzi.
Wataalamu hao, wakiwemo madaktari bingwa waliwasili nchini Juni, mwaka huu, na wanatarajiwa kukaa nchini kwa miaka miwili. Wanatoka jimbo la Jiangsu na wamekuwa wanakwenda Zanzibar kufanya kazi tangu mwaka 1964.
“Msijishughulishe tu kutoa huduma za tiba, badala yake muangalie pia suala la kinga ambalo ni muhimu katika kuimarisha afya za wananchi,” alisema.
Dk. Sheni alivitaka vyombo vya habari, vikiwemo vya serikali kuelimisha jamii kuhusu kinga ya maradhi.
Alisema wataalamu hao wana umuhimu wa kipekee, kwa kuwa licha ya kutoa tiba pia wanatekeleza mipango maalumu ya kusimamia ujenzi wa kituo cha uchunguzi wa maradhi ya njia ya chakula katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, Unguja.
Pia ujenzi wa kituo cha kuhudumia wagonjwa waliopata ajali katika hospitali ya Abdalla Mzee Pemba.
“Vituo hivyo ni vipaumbele kwetu kwa kuwa vitapunguza gharama kwa serikali ya kuwapeleka wagonjwa nje ya Zanzibar kwa matibabu, wakati mwingine hata kwa uchunguzi,” alisema.
Dk. Sheni alisema hivi sasa wagonjwa wengi wenye matatizo ya njia ya chakula hulazimika kupelekwa Dar es Salaam au hata nje ya nchi, hivyo kukamilika kwa kituo hicho kutakuwa faraja kwa serikali na wananchi.
Kuhusu kituo cha watu wanaopata ajali cha Pemba, alisema ni muhimu kwa kuwa zimekuwepo ajali nyingi, hususan wakati wa msimu wa uchumaji karafuu.
Dk. Sheni aliwahakikishia wataalamu hao kuwa serikali itafanya kila jitihada ili kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi.
Kwa upande wao, wataalamu hao walisema wamejizatiti katika kuwahudumia wananchi ili kutoa mchango wao ipasavyo katika kuimarisha afya nchini.
Kiongozi wa wataalamu hao, Dk. Lui Ya Ping, alisema watafanya kazi kwa bidii ili kutimiza wajibu wao.
Alisema mpango kazi wao umewasilishwa kwa Wizara ya Afya, hospitali na kwa viongozi wao walioko China.
Dk. Lui alisema ujumbe kutoka Idara ya Afya ya Jimbo la Jiangsu utawasili nchini Novemba, mwaka huu, kuangalia utekelezaji wa ujenzi wa vituo vilivyoelezwa katika mpango huo.

Wednesday, 14 August 2013

WALINZI wakiwadhibiti wafuasi wa Katibu wa Jumuia za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda  kuingia wodini kumuona kiongozi wao alipokuwa akisomewa shitaka la uchochezi katika wodi ya Kitengo cha Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alikolazwa.

Nape: Madiwani Bukoba bado halali


NA SELINA WILSON
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema bado kinawatambua madiwani wanane wa Manispaa ya Bukoba, waliotangazwa kuvuliwa uanachama.
Kwa mujibu wa Chama, uamuzi wa kuwavua uanachama hauna baraka za vikao vya ngazi ya juu vya CCM.
Chama kimewataka madiwani hao waendelee kufanya kazi na kwamba, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, itakutana Agosti 23, mwaka huu, mjini Dodoma, kujadili suala hilo na mambo mengine.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera, kutangaza kuwavua uanachama madiwani hao.
Madiwani waliovuliwa uanachama ni Yusuph Ngaiza wa kata ya Kashai, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba, na Samwel Ruangisa wa kata ya Kitendagulo, aliyewahi kuwa meya na mkuu wa kwanza wa mkoa wa Kagera.
Wengine ni Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Deusdedith Mutakyawa (Nyanga), Richard Gaspal (Miembeni), Naibu Meya Alexander Ngalinda (Buhembe),  Dauda Kalumuna (Ijuganyondo) na Robert Katunzi (Hamugembe).
Nape alisema kwa mujibu wa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM walio kwenye vyombo vya dola, hususan wabunge na madiwani, uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Mkoa si wa mwisho.
“Uamuzi huo unapaswa kupata baraka za Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, ndipo utekelezwe, na hilo ni kwa mujibu wa Mwongozo wa CCM ulitolewa Juni 22, mwaka 2010,” alisema.
Alisema mwongozo huo umeelekeza uamuzi wowote wa adhabu unaogusa viongozi wa CCM wenye madaraka kwenye serikali, wakiwemo wabunge na madiwani ni lazima upitishwe na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama.
Nape alisema madiwani waliosimamishwa bado ni halali wa CCM, na wanapaswa kuendelea na kazi kama kawaida wakisubiri kikao cha Kamati Kuu.
Aliwataka wananchi wa Manispaa ya Bukoba na kata husika, wanachama na viongozi wa CCM kuwa watulivu katika kipindi ambacho suala hilo linashughulikiwa na vikao vya kitaifa.
Kwa mujibu wa Nape, wamepokea barua za madiwani hao za kukata rufani kupinga uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Mkoa kwa msingi wa madai ya kukiukwa utaratibu katika kufikia uamuzi huo.
Madiwani hao walikata rufani kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kupinga uamuzi huo, muda mfupi baada ya kutangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera, Avelin Mushi.
Katika barua ya rufani, ambayo Uhuru ina nakala yake, madiwani hao wanasema wanapinga kuvuliwa uanachama na kuondolewa nyadhifa zao kwa kuwa utaratibu haukufuatwa.
“Sisi madiwani wanane wa CCM kwa pamoja tunapinga uamuzi uliofikiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya mkoa kwa sababu kanuni, utaratibu na katiba ya Chama  havikufuatwa.
“Kwa hali hiyo, tunaleta malalamiko yetu mbele yako ili uliangalie suala hilo kwa umakini kwa maslahi ya Chama chetu, serikali, wanachama na wananchi waliotupa dhamana ya nafasi hizi,” ilieleza barua hiyo iliyowasilishwa kwa Kinana.
Juzi Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Kagera, katika kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Chama mkoani humo, Costancia Buhiye, kilipitisha uamuzi wa kuwafutia dhamana ya uanachama na kuwaondolea nyadhifa zao madiwani hao.
Kwa mujibu wa Mushi, hatua hiyo ilitokana na kupuuza ushauri uliotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Mushi, alisema uamuzi huo unatokana na Chama kujali maslahi ya wananchi, tofauti na ya watu binafsi na kwamba, ulitokana na mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa  hiyo, Dk. Anatoli Amani.
Rais Kikwete akiwa ziarani mkoani Kagera hivi karibuni, alitoa agizo kwa wana-CCM hao kutoendelea na mgogoro huo. Mushi alisema vikao vya Chama vimekuwa vikifanyika kwa kufuata kanuni na utaratibu.
Hata hivyo, alisema licha ya kuitwa kwenye vikao hivyo, wanachama hao wamekuwa wakikaidi, na  wakionywa kuhusu kuihujumu serikali ya CCM kwa kushirikiana na madiwani wa kambi ya upinzani kwa kutotekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi.
Katika mgogoro ndani ya manispaa, Kagasheki anapinga ujenzi wa soko jipya mjini Bukoba akidai haukufuata uamuzi wa vikao vya baraza la madiwani wakati Dk. Amani akisisitiza ujenzi umepitishwa na vikao vya baraza.
Mgogoro huo uliibuka baada ya uongozi wa manispaa kutangaza utekelezaji wa miradi mbalimbali, ukiwemo wa ujenzi wa soko jipya na la kisasa na upimaji wa viwanja 5,000.
Uamuzi huo wa kutimuliwa kwa madiwani wanane ulipokelewa kwa hisia tofauti na wananchi wa manispaa hiyo wakiwemo wanachama wa CCM ambao baadhi yao waliungana  na madiwani hao kusikitikia uamuzi huo.

Ponda asomewa shitaka kitandani


NA KHADIJA MUSSA
KATIBU wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, amesomewa shitaka la kuwahamasisha wafuasi wake kutenda makosa.
Ponda (54), alisomewa shitaka hilo jana katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu ya Muhimbili (MOI), alikolazwa akitibiwa jeraha analodai ni la risasi, lililoko bega la kulia.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Tumaini Kweka, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hellen Riwa, alimsomea shitaka hilo saa 10.15 jioni.
Kweka alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Juni 2 na Agosti 11, mwaka huu, katika maeneo mbalimbali nchini.
Alidai kwa wadhifa wake, Ponda aliwahamasisha wafuasi wake kufanya vurugu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Ponda alikana shitaka na kesi iliahirishwa hadi Agosti 28, mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.
Mshitakiwa ameendelea kuwa chini ya ulinzi hospitali hapo, baada ya kunyimwa dhamana kutokana na sababu za kiusalama.
Kwa upande wake, wakili Juma Nassor, anayemwakilisha Ponda, hakuwepo wakati shitaka hilo likisomwa.
Hata hiyo, ilielezwa wanatarajia kuwasilisha pingamizi mahakamani kutaka kesi hiyo ifutwe wakidai hati ya mashitaka ina kasoro kisheria.
Miongoni mwa kasoro hizo inadaiwa ni kufunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  Kisutu, ambayo haina uwezo wa kusikiliza shitaka hilo linalodaiwa kutendwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Licha ya kuwepo ulinzi mkali katika maeneo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wafuasi wa Ponda walifurika na kusababisha usumbufu kwa watu wengine, wakiwemo waliokwenda kupata huduma ya tiba na kuona wagonjwa.
Mmoja wa madaktari katika hospitali hiyo kubwa nchini, ambaye hakutaka kutaja jina, alikaririwa akisema ni vyema Ponda akahamishiwa hospitali nyingine ili kupunguza msongamano usio wa lazima Muhimbili.
Alisema jeraha la Ponda linaweza kuendelea kutibiwa katika hospitali zingine zilizoko jijini Dar es Salaam na si lazima Muhimbili.
Ponda alipokewa MOI Agosti 11, mwaka huu, saa 7.30 mchana, akitokea MNH.
Inadaiwa kiongozi huyo alijeruhiwa mwishoni mwa wiki iliyopita akiwa mkoani Morogoro, baada ya kumaliza kuhutubia kongamano la baraza la Idd el Fitri, lililoandaliwa na taasisi hiyo.

Polisi wanasa shehena ya bangi


 NA LILIAN JOEL, ARUSHA

POLISI Mkoani hapa wamekamata shehena ya maguni 352 ya bangi yaliyokuwa yakisafirishwa kwa ajili ya kuingia katika soko la ndani na nje ya nchi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Lebaratus Sabas, aliwaambia waandishi wa habari Jijini Arusha jana kuwa, shehena hiyo ilikamatwa baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Kamanda Sabas, alisema katika tukio hilo, watu watano wanawashikiliwa kwa kosa la kukutwa wakiisafirisha.
Aliwataja watuhumiwa kuwa ni Thomas Lesime (60), Esuphat Daudi, Atumii Daud, Lemali Saitoti na Lomayan Thomas, wote wakazi wa Kijiji cha Kisimiri Juu, wilayani Arumeru.
Hata hivyo, alisema tayari wameshateketeza magunia 225 na magunia 127 yameachwa kwa ajili ya kutumika kama kielelezo mahakamani.
Wilaya ya Arumeru ni miongoni mwa wilaya maarufu nchini kwa kilimo cha bangi, huku Kijiji cha Kisimiri Juu kikiongoza.
Kilimo cha zao hilo kimeendelea kushika kasi kutokana na kipato kizuri na cha uhakika wanachopata wahusika wa biashara hiyo haramu.
Imeelezwa kuwa kilimo hicho huendeshwa chini ya ufadhili wa wafanyabiashara wakubwa wakiwemo kutoka nje ya nchi.
Wafanyabiashara hao, hulipia gharama za kutunza shamba na uvunaji kama njia ya kuwahamasisha wakulima kuendelea na kilimo hicho haramu.

Walioachana na mihadarati watinga Ikulu


Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete ameiagiza Wizara  ya Afya kupitia kitengo cha magonjwa ya akili,  na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, kushirikiana na Kituo cha Ushauri Nasaha cha Pili Misana Foundation.
Alisema lengo ni kutaka kuona kituo hicho  kinawasaidia waathirika wengi zaidi wa dawa hizo.
Aliyasema hayo juzi Ikulu, Dar es Salaam, alipokutana na vijana walioachana na matumizi ya dawa za kulevya ambao wamepata ushauri nasaha na usaidizi kutoka katika kituo cha Pili Misana, kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam.
“Jamii lazima ishiriki katika utatuzi wa jambo hili ni tatizo kubwa na linamgusa kila mtu na inabidi wote tushiriki katika kulipiga vita,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo, alimpongeza Pili Misana na Zacharia Hans Pope, ambaye ndiye mfadhili wa kituo hicho ambacho tayari vijana 203 wamepatiwa huduma ya ushauri nasaha na wameachana na matumizi ya dawa za kulevya na kurudi katika shughuli za maendeleo.
Rais Kikwete, alisema tatizo la dawa za kulevya ni la muda mrefu, lakini awali lilikuwa halisikiki kwa sababu jitihada za kuzuia dawa hizo zilikuwa hazitangazwi wala kufuatiliwa.
Vijana 35 walioacha matumizi ya dawa hizo, walikwenda Ikulu wakiwa wametoka katika shughuli za kitaaluma, elimu na kijamii na wana umri tofauti kati ya miaka 14 mpaka 53.
Alisema serikali inafanya jitihada kubwa za kuwasaidia vijana mbalimbali na itaendelea kutoa msaada huo, huku juhudi za kupambana na dawa hizo zikiendelea.
Naye mfadhili wa kituo hicho, Zacharia Hans Pope, alitoa wito kwa jamii, kushiriki kwa kuwa karibu zaidi na vijana walioathirika ili kusaidia mapambano ya dawa hizo.

Waliojenga katikati ya makaburi wabomolewa


Na Frank Kibiki, Iringa
WATU waliovamia na kujenga nyumba katikati ya makaburi ya Mtwivila, Manispaa ya Iringa, wamebomolewa nyumba hizo.
Kazi hiyo ilifanywa jana na Halmashauri ya Manispaa hiyo, kwa madia kuwa nyumba hizo zimejengwa kinyume cha sheria.
Uhuru, lilishuhudia operesheni ya kubomoa nyumba hizo ambayo ilitekelezwa na askari mgambo wa Manispaa hiyo.
Meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi, alisema ni makosa kuvamia sehemu ya makaburi na kujenga nyumba, jambo ambalo kamwe hawataliacha liendelee.
“Ni kosa kujenga katikati ya makaburi, imebidi tuendeshe operesheni ya kubomoa nyumba hizi, kwa sababu hawa watu walivamia eneo hili la makaburi na kujenga nyumba zao tena bila woga wowote,” alisema Mwamwindi.
Akisimamia operesheni hiyo, Mwanasheria  wa Manispaa ya Iringa Innocent Kihaga,  alisema wamelazimika kuvunja nyumba hizo baada ya kubaini kuwaa zimejengwa maeneo ambayo si rasmi na bila kuwepo kibali cha mipango miji.
Hata hivyo, mwanasheria huyo alisema  wametoa muda wa siku 30 kwa mmiliki wa nyumba moja, ambayo tayari imekamilika, kubomoa na kuondoka eneo hilo.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Theresia Mahongo,  alisema manispaa haitakubali kuona watu wanajenga nyumba kiholela na kuwataka waheshimu sheria zilizopo.
Aliwataka wote waliojenga nyumba kwenye maeneo ambayo hawajaruhusiwa wabomowe kwa hiyari.

Tume yatoa ukomo wa muda wa maoni


NA MWANDISHI WETU
TUME ya Mabadiliko ya Katiba, imezitaka asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofana, kuwasilisha maoni yao kabla ya muda wa mwisho uliowekwa.
Makundi hayo ni yale yaliyounda Mabaraza ya Katiba kwa wanachama wake kwa ajili ya kuijadili na kuitolea maoni Rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya iliyotolewa na Tume.
Kwa mujibu wa Tume hiyo, mwisho wa kuwasilisha maoni ni Agosti 31, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa jana kwa Vyombo vya habari na Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid, ilisema ukomo wa tarehe ya kuwasilisha maoni kwa mujibu wa mwongozo wa Uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana ulianza kutumika Juni Mosi, mwaka huu.
Assaa, alisema Tume haitaongeza muda wa kupokea maoni kwa makundi hayo kwa kuwa baada ya tarehe iliyotajwa, Tume itakuwa na kazi ya kuyapitia na kuyachambua maoni hayo kwa ajili ya kuiboresha Rasimu.
Katibu huyo alizitaka kuwasilisha maoni yao moja kwa moja katika ofisi za Tume zilizopo Jijini Dar es Salaam, Mtaa wa Ohio au ofisi ndogo ya Zanzibar, Mtaa wa Kikwajuni Gofu, katika Jengo la Mfuko wa Barabara.
“Kwa mujibu wa Aya Na. 4.0 ya Mwongozo, Asasi, Taasisi na Makundi ya watu wenye Malengo yanayofanana, yanatakiwa kuwasilisha kwa Tume maoni hayo kwa njia ya randama, barua, andiko au muhtasari wa makubaliano,” alisema Assaa.
Aidha, alisema wanaweza kutuma kwa njia ya barua pepe; katibu@katiba.go.tz au anuani za posta za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, S.L.P 1681 Dar es Salaam pamoja na ile ya S.L.P 2775 Zanzibar.
Hata hivyo, aliyataka makundi hayo kuzingatia tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maoni iliyopangwa naTume.

Friday, 9 August 2013


RAIS Jakaya Kikwete, akitoka katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, jana, baaada ya
kuwajulia hali raia wawili wa Uingereza waliomwagiwa tindikali mjini Zanzibar na kulazwa hospitalini hapo.(Picha na Freddy Maro).

Watalii wamwagiwa tindikali Zanzibar




Na waandishi wetu
WATALII wawili raia wa Uingereza, wamejeruhiwa baada ya watu wasiojulikana kuwamwagia tindikali wakiwa matembezini eneo la Shangani, mjini Unguja, Zanzibar.
Habari za kuaminika zinasema watalii hao walikuwa wanakwenda kula katika hoteli ya Pagoda, na walipatwa na mkasa huo saa moja usiku.
Tukio hilo ni mwendelezo wa matukio kadhaa ya watu kumwagiwa tindikali, wakiwemo viongozi wa dini na wafanyabiashara.
Watalii hao, Katie Gee na Kristie Trup, wana umri wa miaka 18, ambao ni walimu wa kujitolea katika Kituo Maalumu cha Sober House, kinachowasaidia waathirika wa dawa za kulevya.
Katie na Kristie waliwasili Zanzibar wiki mbili zilizopita kupitia Shirika lisilo la Kiserikali la Art In Tanzania.
Rais Jakaya Kikwete,  amewatembelea watalii hao katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam, ambako walipelekwa baada ya tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna wa Jeshi la Polisi Mussa Ali Mussa, alisema wameanza uchunguzi ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa.
“Tumeanza uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwahoji watu mbalimbali, wakiwemo wanaotembeza watalii Zanzibar,’’ alisema.
Alisema ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote, yakiwemo ya Mji Mkongwe, hususan wakati huu, ambao waumini wa dini ya Kiislamu wanasherehekea sikukuu ya Idd el Fitri.
Kamishna Mussa alisema wamefungua vituo vidogo vya polisi kwenye maeneo yote yatakayokuwa na mikusanyiko na askari wameongezwa kulinda usalama mitaani.

CCM YAONYA, YALAANI
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimelaani tukio hilo, ambalo kimesema imepokea taarifa zake kwa masikitiko.
Imesema walimu hao walikuwa msaada mkubwa kwa taifa, kutokana na kujitolea kufundisha Shule ya Mtakatifu Monica, katika Kanisa la Anglikana, Zanzibar.
Taarifa ya Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Itikadi na Uenezi, Zanzibar, Waride Bakari Jabu, alisema unyama huo kamwe haupaswi kufumbiwa macho, kwani ni kinyume cha haki za binadamu.
“CCM inalaani unyama huu na vitendo vya watu kumwagiwa tindikali, tunavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina, kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wote,’’ alisema.
Waride, katika taarifa kwa vyombo vya habari jana, alisema mfululizo wa matukio ya watu kumwagiwa tindikali ni jambo la hatari.

SANYA: NI UNYAMA
Mbunge wa Mji Mkongwe, Muhammad Ibrahimu Sanya, alisema tukio hilo ni la kinyama na halipaswi kufumbiwa macho.
Ameliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha linakuwa makini na watu wanaoendesha unyama huo, na kuchukua hatua kwa wakati stahili.
“Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi haraka na lihakikishe waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria. Ni tukio la kijinga na la kinyama, binadamu hawezi kufanya hivi kwa mwenzake,” alisema.
Sanya alisema hilo ni tukio la utovu wa nidhamu na kwamba, matukio ya aina hiyo hayapaswi kufumbiwa macho, kwani yanalipaka tope taifa.
HOFU YATANDA
Tukio hilo limeanza kuwatisha wadau wa utalii, wakihofia kupungua kwa watalii.
Ofisa wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, ambaye hakupenda kuandikwa jina gazetini, alisema tukio hilo linaweza kuzorotesha maendeleo, hususan katika sekta ya utalii.
Alisema linaweza pia kuwatisha raia wa Uingereza, ambao wanaweza kusitisha kutembelea Zanzibar.
Zanzibar hupokea watalii wengi kutoka nchi za Ulaya, ikiwemo Uingereza na Italia.
Tukio hilo ni la tatu katika kipindi cha miezi mitatu, ambapo Mei 23, mwaka huu, Sheha wa Shehia ya Tomondo, Zanzibar, Mohammed Omar Said, alimwagiwa tindikali na watu wasiofahamika.
Julai 14, mwaka huu, Sheikh wa Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, Said Makamba, alimwagiwa tindikali.
Mmoja wa wamiliki wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad, alimwagiwa tindikali Julai 19, mwaka huu, eneo la Msasani, Dar es Salaam.


Mhadhiri UDSM auawa kwa risasi



NA KHADIJA MUSSA
MHADHIRI Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shule ya Uhandisi, Patrick Rweyongeza, ameuawa kwa kupigwa risasi na majambazi.
Tukio hilo ni mfululizo wa matukio ya ujambazi wa kutumia pikipiki, maarufu bodaboda, ambayo yameanza kushika kasi jijini Dar es Salaam.
Rweyongeza aliuawa juzi, saa tano asubuhi, eneo la Magomeni TANESCO, alipokuwa akitoka benki. Inadaiwa majambazi hayo yalipora sh. milioni 5.5.
Mhadhiri huyo inaelezwa alikuwa ndani ya gari na alikuwa anakwenda eneo lake la ujenzi.
Kwa mujibu wa taarifa, majambazi hayo yalimfuata yakiwa kwenye pikipiki na kumfyatulia risasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alithibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa, uchunguzi unaendelea.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa chuo hicho, Dk. Mohamed Bakary, ameviomba vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika katika tukio hilo.
Rweyongeza aliajiriwa UDSM Machi, 2008. Masomo yake ya chuo kikuu aliyapata chuoni hapo alikojiunga 2002 na kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Uhandisi Majengo mwaka 2007.
Mwaka 2010 Rweyongeza alijiunga na Chuo Kikuu cha Glasgow, nchini Scotland, ambako mwaka 2011 alihitimu Shahada ya Uzamili ya Uhandisi Majengo na Mitambo.

Serikali yatahadharishwa


SERIKALI imetahadharishwa kuweka mipaka na ukomo wa uwezo wa kampuni binafsi za ulinzi, kwenye eneo la ulinzi na usalama wa taifa katika katiba mpya.
Hatua hiyo imeelezwa itasaidia kudhibiti ulinzi na usalama wa taifa, badala ya sasa ambapo kila kampuni inajiimarisha kwa kadri ya uwezo wake, zingine zikifanya kazi nchi nzima kama vile jeshi.
Hayo yalijitokeza katika mjadala wa Rasimu ya Katiba mpya unaoendelea mjini Kibaha.
Akichangia katika sura ya 15 ya rasimu hiyo inayozungumzia ulinzi na usalama katika Jamhuri ya Muungano, mjumbe wa baraza kutoka kata ya Visiga, Dk. Eliud Eseko, alitaka katiba itamke wazi kuhusu mipaka ya kampuni hizo.
Dk. Eseko alisema ibara ya 220 ya rasimu hiyo inazungumzia taasisi za ulinzi na usalama wa taifa, hivyo pia izungumzie kampuni binafsi za ulinzi na ziwekewe mipaka.
“Kampuni hizi zinaweza kufanya kazi kwa kuwekewa masharti ya ukubwa wake ama zipangiwe mikoa au kanda ili zisiwe kubwa zikaenea nchi nzima,” alisema.
Alisema baadhi ya kampuni hizo zinaongozwa na askari wastaafu wenye uwezo mkubwa, hivyo ikitokea mambo yakaenda ovyo, zinaweza kuleta changamoto kwa majeshi nchini.
“Wasiwasi wangu ni kuwa, mtu aliyepata mafunzo jeshini na kuwa mtaalamu wa mabomu, sasa anaongoza mtandao wa walinzi binafsi nchi nzima, akiamua kuasi itakuwa kazi kubwa, hivyo nashauri kampuni hizo zibanwe zisiwe na ukubwa huo,” alisema.
Naye Tatu Jamadi, akiwasilisha maoni ya kundi E, alitaka Jeshi la Magereza na Uhamiaji, yawe katika orodha ya taasisi za ulinzi na usalama wa taifa, kwani taasisi hizo hazikutajwa.
Katika ibara hiyo, taasisi zilizotajwa ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa.

Umri wa kustaafu majaji wapingwa



UMRI wa miaka 70 wa kustaafu jaji mkuu na majaji wa mahakama ya juu uliopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba mpya umepingwa, na kupendekezwa uwe miaka 65.
Hoja hiyo ilitolewa na mjumbe wa Baraza la Katiba kutoka kata ya Maili Moja, Andrew Lugano, wakati akichangia mjadala wa Rasimu ya Katiba mjini Kibaha.
Alisema ibara ya 155 ya rasimu, imeweka miaka 70, lakini anapendekeza iwe miaka 65, kwani mtu anakuwa amezeeka na anapaswa kupumzika.
“Hata katika vitabu mbalimbali, vikiwemo vya maandiko matakatifu, umri wa kuishi duniani ni miaka 70, hivyo akistaafu miaka 65 anapata miaka mitano ya kula pensheni,” alisema.
Naye Alex Warioba, alitaka kiongozwe kifungu kwamba, miaka miwili kabla ya kustaafu wasipewe kesi ili wapate muda wa kumalizia za nyuma.
Alisema uzoefu unaonyesha kuna kesi nyingi zinachelewa kumalizika kutokana na majaji kustaafu, hivyo hukabidhiwa kwa mwingine jambo ambalo linachelewesha utoaji haki.
Ibara ya 155, kifungu cha kwanza inasema Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu watashika madaraka mpaka watakapofikisha miaka 70, isipokuwa kama watajiuzulu au kuvuliwa wadhifa kwa mujibu wa katiba.


Atakayefukuzwa kupoteza ubunge


SUALA la wabunge wanaotimuliwa na vyama vyao limechukua nafasi kubwa katika mjadala wa Rasimu ya Katiba Mpya, mjini Kibaha, huku wengi wakipendekeza wabunge hao wapoteze ubunge.
Wakichangia ibara ya 123 ya rasimu hiyo, wajumbe wa Baraza la Katiba la Halmashauri ya Mji wa Kibaha, walisema mbunge aliyedhaminiwa na chama akifukuzwa na kuvuliwa uanachama, ubunge wake nao unapaswa kukoma.
Mjumbe kutoka kata ya Kongowe, Slom Bagumesh, alisema hatua hiyo itasaidia kujenga nidhamu kwa wabunge wanaotokana na vyama, lakini wakiendelea na ubunge haitakuwa sawa.
“Hivi mtu aliyepeperusha bendera ya chama fulani, anakwenda bungeni badala ya kutetea wananchi anakitukana chama kilichompeleka pale, akifukuzwa hakuna sababu ya kubaki na ubunge,” alisema.
Mjumbe mwingine kutoka kata ya Tumbi, Rajabu Makala, alisema kifungu cha pili cha ibara ya 123, kinapaswa kuboreshwa badala ya kubaki na ubunge, kitamke atakuwa amepoteza ubunge, mbunge atakayefukuzwa na chama chake.
Alisema wabunge wanaotokana na vyama wanapaswa kuheshimu katiba na kanuni za vyama vyao, na endapo akizivunja na akifukuzwa na kuvuliwa uanachama apoteze ubunge.
“Tunasema huyo abaki na ubunge atakuwa anamwakilisha nani, kama waliompeleka wamemtimua inabidi ufanyike uchaguzi mdogo,” alisema.
Mjumbe mwingine alisema kifungu cha tatu cha ibara hiyo, ambacho kinatamka mbunge akijiondoa mwenyewe kwenye chama, atapoteza sifa ya kuwa mbunge, kiondolewe na kibaki kifungu cha pili.
Wajumbe wengine walitaka katiba ieleze endapo ataondolewa kwa mizengwe aweze kwenda kupinga mahakamani.
Hata hivyo, mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema kifungu hicho kiliwekwa kutokana na maoni ya wananchi kwamba, ili kukwepa gharama za uchaguzi mdogo, pasiwe na uchaguzi wa mara kwa mara.
Alisema kama maoni ya kutaka uchaguzi mdogo urejeshwe yatajitokeza, tume itachukua maoni ya wengi.
Wajumbe wengine waliunga mkono rasimu hiyo kwamba, endapo mbunge atakoma ubunge kutokana na kifo au sababu yoyote, chama chake kiteue mtu aliyefuata katika orodha ya kura za ndani ya chama isipokuwa kwa mbunge huru uchaguzi ufanyike.

Wataka Kiswahili kitumike kimataifa


WAJUMBE wa Baraza la Katiba  la Halmashauri ya Kibaha, wametaka lugha ya Kiswahili itumike katika mawasiliano rasmi ya kitaifa na kimataifa.
Wakichangia mjadala wa katiba mpya mjini Kibaha, pia walitaka Kiswahili kitumike kama lugha rasmi ya kufundishia kuanzia darasa la kwanza hadi vyuoni.
Akichangia katika sura ya kwanza, ibara ya nne ya rasimu hiyo, Selina Wilson, kutoka kata ya Maili Moja, hilo litawezesha kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.
“Hakuna taifa lililopiga hatua kiuchumi kwa kutumia lugha za kigeni, inabidi Kiswahili kiwe lugha rasmi ya kufundishia na mawasiliano ya kitaifa na kimataifa.
“Vijana wa Kitanzania wamekuwa wakibuni teknolojia mbalimbali, lakini kutokana na matumizi ya Kingereza inabidi zipewe majina kwa lugha hiyo,” alisema.
Alisema ni wakati sasa katiba itamke wazi ili kuhakikisha Kiswahili kinachukua nafasi yake, kwani ni moja kati ya tunu za taifa.
Mjumbe mwingine, Issa Mkuwili, kutoka kata ya Mkuza, alisema Kiswahili kimeshaanza kutumiwa na mataifa mbalimbali lakini Watanzania wanarudi nyuma katika kukiendeleza.
Mwenyekiti wa kundi la sita la kukusanya maoni ya rasimu hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema Kiswahili kinatumiwa kibiashara na kinawaingizia fedha nyingi wajanja kutoka Kenya na Uganda.
Alisema watu wa mataifa mengi duniani, yakiwemo ya Ulaya, wanapenda kujifunza Kiswahili na kinazungumzwa na mataifa mengi, hivyo kinaweza kutumika kimataifa.
“Unapokwenda nchi za Ulaya utakuta walimu wa Kiswahili wengi wanatoka Kenya, hata mabalozi wanapokuja nchini wanakwenda chuo kikuu kujifunza Kiswahili, utakuta mwongozaji wao ametoka Uganda,” alisema.

Thursday, 1 August 2013

Dk. Mwakyembe afichua ufisadi mpya bandarini


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
SERIKALI imetoa miezi mitatu kwa matrekta yaliyoingizwa nchini kwa ajili ya utekelezaji mpango wa Kilimo Kwanza na sasa yanabeba makontena katika Bandari ya Dar es Salaam, yawe yameondolewa.
Imeelezwa serikali ilifuta ushuru wa zana za kilimo, yakiwemo matrekta chini ya mpango wa Kilimo Kwanza, lakini mengi yameishia kufanya shughuli nyingine nje ya sekta ya kilimo.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alitoa agizo hilo jana, wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya kilimo (Nane Nane), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, katika viwanja vya John Mwakangale, vilivyoko jijini Mbeya.
Dk. Mwakyembe alisema agizo hilo linatakiwa liwe limetekelezwa ifikapo Oktoba 30, mwaka huu, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaokaidi.
“Hili hatuwezi kulivumilia, linavunja malengo ya serikali ya kujitosheleza katika kilimo. Matrekta mengi nimeyaona bandarini Dar es Salaam, yakitumika kubeba mizigo, yakiwemo makontena, hivyo natoa miezi mitatu yote yawe yameondolewa,” alisema.
Alisema matrekta hayo na yanayoendelea kuwepo barabarani katika maeneo mbalimbali mijini, ifikapo Oktoba 30, mwaka huu, yasiwepo.
Dk. Mwakyembe alisema atazungumza na uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na Jeshi la Polisi ili kupiga marufuku matrekta mijini, badala yake yawe mashambani kulima na kubeba mizigo.
Katika hatua nyingine, waziri alizitaka halmashauri kuondoa mambo madogo madogo yanayowakatisha tamaa wakulima.
Aliyataja mambo hayo kuwa, kodi za kukera, ambazo zinaendelea kutozwa kwa wakulima wanaotoa mazao ama shambani kwenda nyumbani au gulioni.
Dk. Mwakyembe alisema halmashauri zina wataalamu wenye ujuzi mbalimbali, lakini wanashindwa kutumia weledi na elimu yao kubuni vyanzo vipya vya mapato, ambavyo havitawakera wananchi.
Katika hatua nyingine, aliwataka wakulima wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kujiunga katika ushirika na kuviimarisha vyama vilivyoko kwa kununua hisa, kuweka akiba na amana ili kupata mitaji ya kilimo.
Alisema ushirika imara utawasaidia wanachama kupata mitaji, pembejeo za kilimo, zana bora na kutafuta masoko ya mazao ya wanachama.
TAFUTENI MASOKO NJE
Wakati huo huo, Theodos Mgomba, anaripoti kutoka Dodoma kuwa, serikali imewataka wataalamu kufikisha kwa wakulima ubunifu na majibu ya utafiti wa kilimo, badala ya kufanya hivyo kwenye maonyesho tu.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alisema hayo jana, alipofungua maonyesho ya Nane Nane katika viwanja vya Nzuguni, mjini Dodoma.
Chiza alisema kuna utaalamu wa aina mbalimbali, ukiwemo wa nyenzo za kilimo unaoonyeshwa kwenye maonyesho, lakini hali za wakulima hazibadiliki.
Alisema jambo hilo linatoa sura kuwa, matokeo ya utafiti hayawafikii wakulima ili kuboresha kilimo.
Waziri alisema hakuna sababu ya kuendelea kuweka vikwazo katika biashara za mazao ya chakula. Alisema hivi sasa kuna ongezeko la chakula kutoka nchini kuuzwa nje na watu wa nchi jirani.
“Sioni sababu ya kuweka vikwazo katika biashara ya chakula, unapokwenda Sudan kuna chakula kingi kinachotoka nchini, lakini wanaokiuza huko si Watanzania,” alisema.
Alisema wakati umefika kwa Watanzania kutafuta masoko nje ya nchini na kuuza mazao yao.
Kuhusu ajira kwa vijana, alisema hakuna sababu ya wao kulalamikia ukosefu wa ajira, wakati ardhi kwa ajili ya kilimo ipo ya kutosha.
Chiza alisema hakuna sababu ya vijana kuandamana barabarani kudai ajira, huku wakiacha kilimo kama kazi ya wazee au watu ambao hawana elimu.
“Nitafurahi kama kuna vijana wataandamana na kuja kwangu kuomba ardhi kwa ajili ya kuanzisha kilimo kama ajira kwao,” alisema.

Mchumba wa Slaa alikoroga


NA FURAHA OMARY
JOSEPHINE Slaa Mushumbusi, mchumba wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, ametoa kioja mahakamani, alipokuwa akimtambua mshitakiwa.
Josephine alitoa kioja hicho jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alipokuwa akimtambua mshitakiwa katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomuhusu akiwa mlalamikaji.
Mwanamama huyo aliyehojiwa na wakili iwapo anamtambua mshitakiwa, alikiri kumtambua lakini aliishia kumuonyesha mtu mwingine asiyehusika.
Wakili alimtaka kumtambua mshitakiwa aliyemvamia na kumpora mali zake, kwenye makutano ya SUMA JKT, katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Josephine aliyefuatana mahakamani na Dk. Slaa, alipanda kwenye kizimba mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Riwa, kutoa ushahidi. Washitakiwa katika kesi hiyo ni Getisi Mturi, Gake Mwita, Salum Mpanda na Charles Chasens.
Mturi na wenzake wanadaiwa Julai 13, 2011, katika eneo la SUMA JKT, walimvamia Josephine na kumpora vitu mbalimbali, na kabla ya uhalifu huo, walimtishia kwa bastola.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Leonard Chalo, kutoa ushahidi, Josephine alidai Julai 13, mwaka 2011, saa mbili asubuhi, aliingia ofisini kwake kwenye jengo la Mawasiliano Tower.
Josephine alidai alitoka ofisini  saa 11 jioni na kuanza safari ya kurejea nyumbani kwake Boko, akiendesha gari lenye namba ya usajili T 932 ASH, aina ya Toyota Harrier.
Alidai akiwa kwenye foleni eneo la tukio, aliona mtu akipita upande wa kushoto. Alidai kupitia kioo kidogo cha pembeni mwa gari lake, alimuona mtu huyo akivunja kioo cha gari lake.
“Nilimuona vizuri mtu huyo tangu alipotembea kwenda nyuma ya gari, ambako ghafla alianza kuvunja dirisha,” alidai.
Josephine alidai alitahamaki na kwamba, alisikia milio ya risasi,  hivyo alitafuta njia ya kujiokoa kwa kuondoa gari eneo hilo na kwenda kwenye geti, jirani na SUMA JKT.
“Nilikatisha barabara upande wa pili, ambako niligundua kuna mtu mwingine, nako kulikuwa na risasi zikilia.
“Kabla sijafika nilikotarajia kwenda, gari lilipinduka katikati ya mtaro, nilijaribu kufungua mlango ili nikimbie lakini nilikutana na mtu akiwa na bastola, hivyo sikufanikiwa kukimbia,” alidai.
Shahidi huyo alidai alimuona mtu huyo kwa sura, kwa kuwa walisimama wote kwa takriban dakika nane.
Wakili Chalo alimtaka Josephine kuangalia watu walioko mahakamani iwapo atamuona mtu huyo na kumtambua.  Sehemu hiyo ilikuwa ifuatavyo:
Josephine: Mheshimiwa naweza kumshika mkono iwapo nikimuona?
Hakimu: Ndiyo.
Josephine: Mheshimiwa naomba watu wote wasimame ili niweze kuwaona vizuri, kwani kipindi hicho nakumbuka alikuwa na uso mpana, lakini ni kama amebadilika, kwani hata mimi nilivyokuwa wakati huo si sawa na sasa.
Hakimu: Naomba wote msimame, isipokuwa mimi.
Watu wote waliokuwamo katika chumba cha mahakama walisimama, wakiwemo mawakili.
Josephine: Mheshimiwa huyu hapa, huku akimshika.
Aliyeguswa na Josephine alisogea mbele ya hakimu na kueleza kuwa, hahusiki na kesi hiyo, kwani yuko hapo akisubiri kudhaminiwa.
Mtuhumiwa: Mheshimiwa naomba tu nidhaminiwe, mimi sihusiki, wakati hayo yanatokea nilikuwa Malawi. Hili ni ‘gundu’. Mheshimiwa naomba nidhaminiwe kama barua moja haijahakikiwa, nidhaminiwe vivyo hivyo.
Kutokana na tukio hilo, waliokuwamo mahakamani waliangua vicheko, huku Josephine akisisitiza anakumbuka mtu huyo alikuwa sawa na huyo aliyekuwamo mahakamani.
Akiendelea na ushahidi, Josephine alidai anakumbuka waliomvamia walikuwa si chini ya sita na kwamba, walimwibia vitu mbalimbali, ikiwemo pochi, kamera, simu mbili, kadi za benki na leseni ya udereva. Alidai watuhumiwa waliondoka na pikipiki.
Alidai wakati wa tukio hilo alikuwa mjamzito, hivyo alikwenda hospitali ya Mwananyamala kuangalia afya yake.
Mwanamama huyo alidai kati ya saa sita au saba usiku wa siku ya tukio, alipigiwa simu na askari kutoka kituo cha polisi Chang’ombe na kutakuwa kwenda kufuata mali zake.
Alidai aliipata pochi, kadi za simu na leseni. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Agosti 7, mwaka hu

Wanaharakati wa kisheria wampeleka Pinda kortini


NA FURAHA OMARY
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kimefungua kesi dhidi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
LHRC na TLS wanapinga kauli ya waziri mkuu aliyoitoa bungeni, kuruhusu polisi kuwapiga raia wanaokaidi amri halali ya Jeshi la Polisi.
Mlalamikiwa mwingine katika kesi hiyo iliyofunguliwa jana, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Kesi hiyo
imesajiliwa na kupewa namba 24 ya mwaka 2013.
Akizungumzia hatua hiyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alisema hakuna mahakama yenye uwezo wa kusikiliza shauri linalohusu jambo lililotamkwa na mbunge ndani ya Bunge.
Dk. Kashilillah alisema ibara ya 102 ya Katiba ya Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania, imeeleza wazi kwamba, mbunge hatashitakiwa kwa jambo lolote alilosema au nyaraka alizotoa ndani ya Bunge.
Alisema ibara ya 100 inalitaka Bunge litunge sheria na kuweka utaratibu wa kusimamia haki na sheria, na imeweka mipaka ya kumfanya mbunge awe huru kuchangia mijadala ndani ya Bunge.
Dk. Kashilillah alisema Kanuni ya Bunge ya 71 imetoa nafasi kwa mwananchi, mbunge au taasisi ambayo haijaridhika na matamshi ya mbunge ndani ya Bunge, kuandika malalamiko kwa msimamizi mkuu wa bunge ambaye ni spika.
Alisema spika akipokea malalamiko, huyafanyia kazi na kutoa taarifa bungeni, hivyo waliomshitaki waziri mkuu walipaswa kumuandikia malalamiko yao spika.
Kwa mujibu wa hati ya madai, waombaji wanadai Mei 20, mwaka huu, Waziri Mkuu Pinda akiwa bungeni, alitoa kauli kuruhusu askari wa Jeshi la Polisi kuwapiga raia ambao hawatatii amri yao kunapokuwa na vurugu, jambo ambalo wanadai ni kinyume cha Katiba.
Hati hiyo ilinukuu kauli inayodaiwa kutolewa na Pinda:
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu kwa sababu hakuna namna nyingine, eeh maana tumechoka sasa.”
Wanadai kwa mujibu wa utekelezaji wa sheria za jinai, kauli inayotolewa na kiongozi kama vile waziri mkuu inaonekana kuwa amri inayopaswa kutekelezwa na vyombo vya dola, kama polisi.
Kupitia hati hiyo, wanadai kwa uelewa wao, polisi watadhani ni amri halali iliyotolewa na kiongozi na kusababisha waendelee kuwatesa na kuwapiga wananchi wasio na hatia kinyume cha haki iliyowekwa kwenye sheria.
Wanadai kauli hiyo inahatarisha haki ya kuishi, inadhalilisha utu wa mtu, inaunga mkono matumizi mabaya ya utekelezaji wa sheria na inasababisha ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa.
Inadaiwa kuwa Waziri Mkuu Pinda alivunja ibara ya 100 ya Katiba inayompa kinga mbunge anapotoa jambo lolote bungeni, kwa kuwa yeye hakuzungumza bungeni kama mbunge bali alikuwa anatoa msimamo wa serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi wa Uboreshaji na Utetezi wa LHRC, Harold Sungusia, alisema wameungwa mkono na wananchi zaidi ya 2,019.
Alisema wananchi hao wametia saini hati ya kutoridhishwa na kauli ya waziri mkuu na wanatarajia kuwa na jopo la wanasheria wasiopungua 20 katika kesi hiyo.
Naye Mkurugenzi wa kituo hicho, Hellen Kijo- Bisimba alisema kwa kushirikiana na TLS, wananchi na taasisi mbalimbali wameamua kumshitaki waziri mkuu kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria.

Mashahidi kesi ya vigogo TBA kufikia 13


NA FURAHA OMARY
UPANDE wa Jamhuri katika kesi inayowakabili waliokuwa vigogo wawili wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), umeieleza mahakama kuwa unatarajia kuita mashahidi 13 na vielelezo 20, wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo.
Washitakiwa katika kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambayo imepangwa kuanza kusikilizwa Agosti 7, mwaka huu, ni  waliokuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala huo, Makumba Kimweri na Msanifu Mkuu wake, Richard Maliyaga.
Kimweri na Maliyaga wanakabiliwa na mashitaka matano ya matumizi mabaya ya ofisi katika utoaji kibali cha ujenzi wa jengo la ghorofa 15 kiwanja namba 45 mtaa wa Chimara.
Mwendesha Mashitaka kutoka Taasisi ya  Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai, alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, baada ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali.
Akiwasomea maelezo ya awali, Swai alidai Kimweri alikuwa na wadhifa huo TBA kuanzia mwaka 2002 hadi 2010 na Maliyaga aliajiriwa mwaka 2002 akiwa msanifu mkuu.
Alidai kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na TBA, ambapo hadi mwaka 2006 kilikuwa hakijaendelezwa ambapo wakala huo chini ya Sheria ya Ununuzi wa Umma iliwaalika wanaotaka kuwekeza kuwasilisha andiko la awali kwa ajili ya kuendelezaji.
Swai alidai kampuni nane ziliwasilisha maandiko ya awali ambazo zilifunguliwa katika hafla ya ufunguzi iliyofanyika Februari 19, 2006. Alidai Bodi ya Zabuni ilikutana katika mwaka wa fedha 2006/2007 kikao kilichofanyika Septemba 29, 2006 ilipendekeza wawekezaji saba ikiwemo Royale Orchard Inn Ltd.
Ilidaiwa Februari, 2007 timu ya tathmini ilikaa na kufanya tathmini kuhusu viwanja vinane kwa ajili ya kuviendeeleza ambavyo ni vya TBA, vikiwemo namba 45 na 46.
Mwendesha mashitaka huyo alidai katika ripoti hiyo walitoa mapendekezo kuhusu kampuni saba kuwasilisha taarifa zake kwa kuwa miongoni mwa kampuni za awali zilizopita ikiwemo Royale.
Alidai timu ilipitia tena na kutoa mapendekezo na kuwapitisha Royale na M/s Msasani Slipway Ltd. Ilidaiwa Kaimu Katibu wa Bodi ya Zabuni D. M. Makolo alielekeza ziliamuriwe kampuni mbili kuendelea kutoa taarifa zao na kuwasilisha mbele ya Menejimenti ya TBA na timu ya makubaliano.
Swai alidai Machi 22, 2007, Makolo aliandika barua kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu kumwita mkurugenzi mtendaji wa kampuni zilizoshinda kwa makubaliano.
Alidai Agosti 6, mwaka 2007, mikataba miwili kwa ajili ya viwanja viwili wahusuika walitia saini ambapo kwa upande wa serikali watamiliki asilimia 25 na mwekezaji asilimia 75 katika jengo la ghorofa 18. Alidai TBA ilitoa vibali vilivyotiwa saini na Maliyaga, kikiwemo za kuongeza kutoka ghorofa 15 hadi 18.
Mwendesha mashitaka huyo alidai eneo hilo lilikuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa ghorofa tatu hadi sita na kwa makazi, na kwamba washitakiwa walitoa kibali kwa mwekezaji bila ya kupata idhini kutoka kwa mamlaka husika.
Washitakiwa hao walikubali majina yao, vyeo na kutia saini hati za kuruhusu kujenga wakati mengine yote walikataa.

Watu binafsi vinara wa wizi wa umeme


NA KHADIJA MUSSA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema kuwa, watu binafsi ndiyo wanaongoza kwa wizi wa nishati hiyo, huku wakiwa wadaiwa sugu wa shirika hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Mawasiliano wa Shirika hilo, Badra Masoud, alisema watu binafsi ndiyo wanaongoza kwa kuwa wadaiwa sugu ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo serikali ndiyo iliyokuwa ikiongoza.
Badra alisema kuwa baada ya serikali kuweka vipaumbele likiwemo suala la umeme iliamua kulipa madeni yote, hivyo kwa sasa deni kubwa limebaki kwa watu binafsi.
Alisema mbali na watu binafsi kuwa wadaiwa sugu, pia ndio wanaoongoza kwa wizi wa nishati hiyo ya umeme na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watendaji wanapokwenda kusoma mita.
“Baadhi ya watu wamekuwa wakiwatishia watendaji wa shirika letu kwa ama kukataa kuwafungulia nyumba zao au wakati mwingine kuwafungulia mbwa,” alisema Badra.
Katika hatua nyingine, meneja huyo alisema hali ya ukata wa bajeti unaolikabili shirika hilo, ni miongoni mwa changamoto inayolifanya kushindwa kufikisha huduma hiyo katika baadhi ya maeneo nchini.
Alisema changamoto hiyo inatokana na ongezeko kubwa la watu waliojitokeza kuomba kuunganishiwa huduma hiyo kwa mwaka huu, hasa baada ya serikali kupunguza gharama za kuunganishiwa umeme.
Gharama za kuunganishiwa umeme kwa wateja walioko kwenye umbali usiozidi mita 30 (single phase) ambao hawahitaji nguzo ni sh. 177,000 kwa wateja wa vijijini na mijini  sh. 320,960, ambapo awali ilikuwa sh. 455,108 bila kujali mteja aliko.
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/2013 bungeni Dodoma, Julai 28, mwaka jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja wa mijini.
Pia, Profesa Muhongo alisema serikali imeshusha gharama za uunganishwaji wa umeme kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo moja katika maeneo ya vijijini kwa sh. 337,740 na mijini sh. 515,618 badala ya sh. 1,351,884 zilizokuwa zikilipwa awali.
Alisema kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini watalipa sh. 454,654 na mijini sh. 696,670 badala ya sh. milioni 2.001.
Badra alisema gharama hizo zilizoanza kutumika kuanzia Januari mosi, mwaka huu, zimesaidia kuongeza idadi kubwa ya wateja, hali inayofanya kamouni kutokuwa na bajeti ya kutosha kufikisha umeme katika baadhi ya maeneo.
Alisema shirika hilo lilikuwa na lengo la kuunganisha umeme kwa wateja 150,000, ambapo hadi sasa wamepokea maombi 112,000, huku kati yao 80,000 tayari wakiwa wameunganishiwa.
Kwa mujibu wa Badra, idadi ya waliotuma maombi ni kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hivyo wanatarajia kuvuka lengo walilojiwekea, kwani hali hiyo haijawahi kutokea katika miezi ya hivi karibuni kupokea maombi mengi kiasi hicho.

China yakabidhi dawa za malaria za bil. 2/-


NA RACHEL KYALA.
SERIKALI ya China imeipatia Tanzania msaada wa dawa za kutibu malaria zenye gharama ya takriban sh. bilioni mbili.
Msaada huo wa dawa aina ya Artemisinin iliyogunduliwa nchini China, ulikabidhiwa jana kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi mjini Dar es Salaa
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Balozi wa China hapa nchini, Lu Youging, alisema kuwa, dawa hizo zinafaa kwa matumizi ya binadamu na kwamba hazina madhara.
“Sisi kama marafiki wa karibu wa Tanzania hatufurahi kuona malaria ikiendelea kuwa tatizo kwa Watanzania, hivyo tutatoa ushirikiano kadri tuwezavyo ili kutokomeza ugonjwa huo,” alisema Youging.
Balozi huyo alisema kuwa China ilikuwa miongoni mwa nchi nyingi duniani zilizokuwa zikiathiriwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa huo, lakini hivi sasa umetokomeza.
Akizungumza wakati akipokea msaada huo, Dk. Mwinyi alisema kuwa uhusiano katika sekta ya afya baina ya nchi hizi mbili umedumu kwa miaka mingi, ambapo China imekuwa ikileta madaktari mara kwa mara kuja kufanya kazi hapa nchini.
“Tayari imeshaleta makundi zaidi ya 24 ya matibabu kuja kufanya kazi na kwa sasa kuna madaktari zaidi ya 2,000 wanaofanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini,” aliongeza.
Waziri huyo alisema baadhi ya misaada iliyotolewa na nchi hiyo kwa Tanzania licha ya msaada huo ni ujenzi wa hospitali ya moyo na kuchukua wataalamu wa afya wa hapa nchini kwenda kupatiwa mafunzo nchini humo.
Waziri huyo aliishukuru serikali ya China kwa msaada huo na kuongeza tangu ilipoanza kuisaidia Tanzania dawa za malaria, takwimu zinaonyesha vifo dhidi ya ugonjwa huo vimepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi asilimia 10 mwaka jana na maambukizi yakipungua kwa asilimia 50.