Na Joseph Damas
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam, inatarajia kuuza hisa zake zilizoko katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Hatua hiyo imefikiwa jana katika kikao maalumu cha madiwani wa Jiji la Dar es Salaam na kwamba, hisa hizo zitauzwa kwa bei ya soko kulingana na mahitaji halisi.
Hata hivyo, haijaweka bayana hisa hizo zitauzwa kwa kampuni gani na kwamba, mchakato utatangazwa na utakuwa wa wazi.
Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Massaburi, alisema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao kilichoketi jana na kwamba, umelenga kuliwezesha jiji kuondokana na mvutano, ukiwemo wa madeni yanayolikabili UDA.
Alisema jiji litauza hisa zake kwa kati ya sh. 1,600 na sh. 2,600 tofauti na bei ya awali aliyouziwa mwekezaji Kampuni ya Simon Group Ltd.
Dk. Massaburi alisema iwapo Simon Group itahitaji kununua hisa hizo, italazimika kulipa tofauti ya bei ya awali.
Awali, Simon Group ilinunua hisa ndani ya UDA kwa bei chee, hivyo kuzusha mgogoro, uliomuhusisha Mwenyekiti wa UDA, Iddi Simba.
Dk. Massaburi alisema UDA inakabiliwa na madeni makubwa, ambapo baadhi ya wadai wamefungua mashitaka mahakamani.
Alisema UDA inakabiliwa na madeni yanayofikia sh. bilioni 78 na kwamba, iwapo wahusika watashinda itakuwa mzigo mkubwa kwa jiji.
Meya huyo alisema Jiji la Dar es Salaam litakuwa na mradi mkubwa wa mabasi yaendayo haraka, hivyo UDA haitahitajika mradi huo utakapokamilika.
Thursday, 22 August 2013
Jiji kuuza hisa zake UDA
09:59
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru