Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, inatarajia kupokea taarifa ya serikali kuhusu hatua iliyofikiwa katika marekebisho ya sheria ya Fao la Kujitoa wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jenista Mhagama, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jana, ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam.
Alisema kamati itapokea taarifa ya serikali mjini Dodoma kupitia Wizara ya Kazi na Ajira na kuangalia ni hatua gani iliyofikiwa katika kurekebisha sheria ya mafao ya uzeeni.
Hatua hiyo ilitokana na hoja binafsi iliyowasilishwa na mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jafo, kulitaka Bunge liazimie kuitaka serikali iruhusu fao la kujitoa liendelee.
Awali, kabla ya kuwasilishwa kwa hoja hiyo katika mkutano wa Bunge Novemba, mwaka jana, wafanyakazi na baadhi ya wabunge walilalamikia Sheria ya mwaka 2012 iliyozuia wafanyakazi kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Jenista alisema kazi nyingine inayoendelea kufanywa na kamati ni kupitia muswada wa sheria ya Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini (GEPF).
Alisema muswada huo utakapowasilishwa bungeni utawezesha mfuko huo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, kama ilivyo kwa mifuko mingine, hivyo kuongeza tija.
Tuesday, 20 August 2013
Serikali kuwasilisha taarifa Fao la Kujitoa
09:01
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru