Thursday 1 August 2013

Watu binafsi vinara wa wizi wa umeme


NA KHADIJA MUSSA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema kuwa, watu binafsi ndiyo wanaongoza kwa wizi wa nishati hiyo, huku wakiwa wadaiwa sugu wa shirika hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Mawasiliano wa Shirika hilo, Badra Masoud, alisema watu binafsi ndiyo wanaongoza kwa kuwa wadaiwa sugu ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo serikali ndiyo iliyokuwa ikiongoza.
Badra alisema kuwa baada ya serikali kuweka vipaumbele likiwemo suala la umeme iliamua kulipa madeni yote, hivyo kwa sasa deni kubwa limebaki kwa watu binafsi.
Alisema mbali na watu binafsi kuwa wadaiwa sugu, pia ndio wanaoongoza kwa wizi wa nishati hiyo ya umeme na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watendaji wanapokwenda kusoma mita.
“Baadhi ya watu wamekuwa wakiwatishia watendaji wa shirika letu kwa ama kukataa kuwafungulia nyumba zao au wakati mwingine kuwafungulia mbwa,” alisema Badra.
Katika hatua nyingine, meneja huyo alisema hali ya ukata wa bajeti unaolikabili shirika hilo, ni miongoni mwa changamoto inayolifanya kushindwa kufikisha huduma hiyo katika baadhi ya maeneo nchini.
Alisema changamoto hiyo inatokana na ongezeko kubwa la watu waliojitokeza kuomba kuunganishiwa huduma hiyo kwa mwaka huu, hasa baada ya serikali kupunguza gharama za kuunganishiwa umeme.
Gharama za kuunganishiwa umeme kwa wateja walioko kwenye umbali usiozidi mita 30 (single phase) ambao hawahitaji nguzo ni sh. 177,000 kwa wateja wa vijijini na mijini  sh. 320,960, ambapo awali ilikuwa sh. 455,108 bila kujali mteja aliko.
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/2013 bungeni Dodoma, Julai 28, mwaka jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja wa mijini.
Pia, Profesa Muhongo alisema serikali imeshusha gharama za uunganishwaji wa umeme kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo moja katika maeneo ya vijijini kwa sh. 337,740 na mijini sh. 515,618 badala ya sh. 1,351,884 zilizokuwa zikilipwa awali.
Alisema kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini watalipa sh. 454,654 na mijini sh. 696,670 badala ya sh. milioni 2.001.
Badra alisema gharama hizo zilizoanza kutumika kuanzia Januari mosi, mwaka huu, zimesaidia kuongeza idadi kubwa ya wateja, hali inayofanya kamouni kutokuwa na bajeti ya kutosha kufikisha umeme katika baadhi ya maeneo.
Alisema shirika hilo lilikuwa na lengo la kuunganisha umeme kwa wateja 150,000, ambapo hadi sasa wamepokea maombi 112,000, huku kati yao 80,000 tayari wakiwa wameunganishiwa.
Kwa mujibu wa Badra, idadi ya waliotuma maombi ni kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hivyo wanatarajia kuvuka lengo walilojiwekea, kwani hali hiyo haijawahi kutokea katika miezi ya hivi karibuni kupokea maombi mengi kiasi hicho.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru