Tuesday 20 August 2013

Tunu: Wasichana wawezeshwe


Na Mwandishi Wetu
MKE wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda, amesema kuna haja ya kuweka juhudi za makusudi za kuwawezesha wasichana kuhudhuria masomo kila siku.
Amesema kukosekana vifaa vya kujisitiri wakati wa hedhi miongoni mwa wasichana ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wakose masomo kati ya siku 30 na 70 kwa mwaka, jambo linalochangia kudorora kwa elimu miongoni mwao.
Tunu alisema hayo jana, alipozindua mradi wa ‘Hakuna wasichoweza’ katika Shule ya Msingi Chilongola, iliyoko Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara.
Mradi huo unafadhiliwa na Taasisi ya T-MARC, inayojihusisha na masuala ya afya na maendeleo, ukilenga kuwafikia wasichana 10,000 wa Manispaa ya Mtwara Mikindani na Wilaya ya Mtwara Vijijini.
“Wasichana wengi wanapokuwa katika siku zao hushindwa kuhudhuria masomo kati ya siku tatu na saba kwa mwezi, au siku kati ya 30 na 70 kwa mwaka.
“Hii husababishwa na kukosa nyenzo za uhakika za kujisitiri wakiwa shuleni. Wengi wao huamua kubaki nyumbani hadi mizunguko yao itakapokwisha ili kuepuka kuaibika,” alisema.
Alisema usiri na ufahamu mdogo wa jamii kuhusu masuala ya hedhi na changamoto wanazopata wasichana katika kipindi hicho ni tatizo kubwa.
“Wengi wetu katika jamii inayotuzunguka bado tunalichukulia suala la hedhi kuwa la aibu na la siri kubwa, hivyo matatizo yanayotokana na hali hii ya kawaida hubaki bila kushughulikiwa, kwani kila mtu anaona aibu kusema wazi kuwa kuna tatizo,” alisema.
Aliongeza: “Kwa kuwa hedhi haichagui siku maalumu, inawezekana siku hizo zikawa za mitihani au za masomo muhimu. Matokeo yake ni wasichana kukosa vipindi na walimu  hawavirudii.”
Tunu alisema sababu nyingine ni kukosekana majisafi na huduma safi za vyoo, ikiwemo milango ili kulinda heshima ya mtumiaji.
Alisema shule nyingi hazina vyoo vya kutosheleza idadi ya wanafunzi na vichache vilivyopo mara nyingi havina milango, maji na sabuni. Pia alisema hakuna elimu ya kutosha miongoni mwa wasichana walio kwenye umri wa kubalehe.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru