Thursday, 1 August 2013

Wanaharakati wa kisheria wampeleka Pinda kortini


NA FURAHA OMARY
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kimefungua kesi dhidi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
LHRC na TLS wanapinga kauli ya waziri mkuu aliyoitoa bungeni, kuruhusu polisi kuwapiga raia wanaokaidi amri halali ya Jeshi la Polisi.
Mlalamikiwa mwingine katika kesi hiyo iliyofunguliwa jana, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Kesi hiyo
imesajiliwa na kupewa namba 24 ya mwaka 2013.
Akizungumzia hatua hiyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alisema hakuna mahakama yenye uwezo wa kusikiliza shauri linalohusu jambo lililotamkwa na mbunge ndani ya Bunge.
Dk. Kashilillah alisema ibara ya 102 ya Katiba ya Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania, imeeleza wazi kwamba, mbunge hatashitakiwa kwa jambo lolote alilosema au nyaraka alizotoa ndani ya Bunge.
Alisema ibara ya 100 inalitaka Bunge litunge sheria na kuweka utaratibu wa kusimamia haki na sheria, na imeweka mipaka ya kumfanya mbunge awe huru kuchangia mijadala ndani ya Bunge.
Dk. Kashilillah alisema Kanuni ya Bunge ya 71 imetoa nafasi kwa mwananchi, mbunge au taasisi ambayo haijaridhika na matamshi ya mbunge ndani ya Bunge, kuandika malalamiko kwa msimamizi mkuu wa bunge ambaye ni spika.
Alisema spika akipokea malalamiko, huyafanyia kazi na kutoa taarifa bungeni, hivyo waliomshitaki waziri mkuu walipaswa kumuandikia malalamiko yao spika.
Kwa mujibu wa hati ya madai, waombaji wanadai Mei 20, mwaka huu, Waziri Mkuu Pinda akiwa bungeni, alitoa kauli kuruhusu askari wa Jeshi la Polisi kuwapiga raia ambao hawatatii amri yao kunapokuwa na vurugu, jambo ambalo wanadai ni kinyume cha Katiba.
Hati hiyo ilinukuu kauli inayodaiwa kutolewa na Pinda:
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu kwa sababu hakuna namna nyingine, eeh maana tumechoka sasa.”
Wanadai kwa mujibu wa utekelezaji wa sheria za jinai, kauli inayotolewa na kiongozi kama vile waziri mkuu inaonekana kuwa amri inayopaswa kutekelezwa na vyombo vya dola, kama polisi.
Kupitia hati hiyo, wanadai kwa uelewa wao, polisi watadhani ni amri halali iliyotolewa na kiongozi na kusababisha waendelee kuwatesa na kuwapiga wananchi wasio na hatia kinyume cha haki iliyowekwa kwenye sheria.
Wanadai kauli hiyo inahatarisha haki ya kuishi, inadhalilisha utu wa mtu, inaunga mkono matumizi mabaya ya utekelezaji wa sheria na inasababisha ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa.
Inadaiwa kuwa Waziri Mkuu Pinda alivunja ibara ya 100 ya Katiba inayompa kinga mbunge anapotoa jambo lolote bungeni, kwa kuwa yeye hakuzungumza bungeni kama mbunge bali alikuwa anatoa msimamo wa serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi wa Uboreshaji na Utetezi wa LHRC, Harold Sungusia, alisema wameungwa mkono na wananchi zaidi ya 2,019.
Alisema wananchi hao wametia saini hati ya kutoridhishwa na kauli ya waziri mkuu na wanatarajia kuwa na jopo la wanasheria wasiopungua 20 katika kesi hiyo.
Naye Mkurugenzi wa kituo hicho, Hellen Kijo- Bisimba alisema kwa kushirikiana na TLS, wananchi na taasisi mbalimbali wameamua kumshitaki waziri mkuu kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru