Thursday, 1 August 2013

Sheikh Ponda sasa asakwa


Na Mohammed Issa
POLISI Zanzibar imesema mtu yeyote mwenye taarifa za alipo Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, aziwasilishe Polisi ili aweze kukamatwa.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar Musha Ali Mussa, alisema wanaendelea kumtafuta Sheikh Ponda na kama kuna mtu anataarifa zake aseme, ili aweze kukamatwa.
AIisema wanaendelea kumsaka ili wamuhoji kwa kudaiwa kufanya mihadhara yenye uchochezi.
“CD zake alizokuwa akitoa mihadhara tunazo, tunaendelea kumsaka kwa udi na uvumba na tukimtia mikononi tutamuhoji na kama itaonekana anapaswa kufikishwa mahakamani tutafanya hivyo,” alisema Kamishana huyo.
Sheikh Ponda, inadaiwa alifika visiwani humo na kufanya mihadhara ya kidini katika misikiti kadhaa ya Unguja, yenye kuashiria uvunjifu wa amani.
Taarifa iliyotolewa juzi na Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, ilivitaka vyombo vya dola kumchukulia hatua za kisheria Sheikh Ponda, kutokana na kauli za kichochezi, zinazolenga kuwagawa Wazanzibar.
Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu, alisema Sheikh Ponda alikuwa akifanya mihadhara huko Unguja, yenye mwelekeo wa kujenga chuki na uhasama.
Inadaiwa katika mihadhara yake aliyoifanya Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja na katika msikiti wa Kwarara, mjini humo, aliwahamasisha Wazanzibar kuandamana kuishinikiza serikali kuwaachia masheikh sita wa Jumuia ya Uamsho.
Katika kanda tatu za zenye hotuba ya mihadhara yake, inamnukuu akiwashawishi Wazanzibar kuandamana kama wanavyofanya wananchi wa Misri.
Pia, Sheikh Ponda, anadaiwa kupandikiza chuki miongoni mwa wananchi.
Inadawa kuwa alilenga kuhamasisha pia wafanye uasi kwa lengo la kulipiza visasi, na aliwataka waingie barabarani kwa maandamano.
Hivi sasa, Sheikh Ponda anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja, kufuatia hukumu iliyotolewa hivi karibuni na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Moja ya masharti aliyopewa ni kutotenda kosa katika kipindi chote anachotumikia kifungo hicho.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru