Tuesday, 20 August 2013

Mgambo watibua mambo Amana



Na Mwandishi Wetu
TAKRIBAN sh. 700,000 zinazokusanywa kwa mwezi na mgambo katika Hospitali ya Amana, wilayani Ilala, Dar es Salaam, zikidaiwa kuwa ushuru wa maegesho ya pikipiki, hazijulikani zinakokwenda.
Licha ya mgambo kukusanya fedha hizo, si uongozi wa hospitali au Manispaa ya Ilala ulioeleza kuutambua ushuru huo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hospitalini hapo, umebaini mgambo hukusanya fedha hizo bila kutoa stakabadhi, zaidi ya kuorodhesha namba za usajili wa pikipiki kwenye karatasi.
Mgambo hao hutoza sh. 500 kwa kila pikipiki inayoingia hospitalini  hapo, wakidai ni maelekezo kutoka kwa wakubwa wao, ambao hata hivyo, hawakuwa tayari kuwataja.
Ofisa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema manispaa haina taarifa za kutozwa ushuru huo.
“Hilo silifahamu, naahidi kulifuatilia na kutoa taarifa sahihi,” alisema.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Meshack Shimwela, alisema uongozi wa hospitali hauhusiki na tozo hiyo na hauifahamu.
Alisema iwapo kuna utaratibu huo, wanaokusanya ushuru wanafanya hivyo kwa utashi wao bila uongozi wa hospitali kujua.
“Vyombo vyote vya moto vinatakiwa kuingia na kutoka bila kulipia, kama kuna mtu anawatoza watu ushuru, uongozi wa hospitali hauhusiki na  haufaidiki na chochote,” alisema.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Asha Mahita, alisema utaratibu huo hauruhusiwi na haupo kisheria.
Alisema inawezekana wanaotoza fedha hizo wanafanya hivyo kwa maslahi binafsi, na kwamba mtu yeyote hatakiwi kulipia ushuru wa chombo cha usafiri anapoingia hospitalini na kama atalipishwa  apatiwe risiti.
“Hilo ni tatizo haiwezekani mtu alipie huduma bila ya kupewa risiti, kwani sheria ndivyo inavyoelekeza,” alisema.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa nyakati tofauti wiki iliyopita umebaini kati ya saa 12 asubuhi hadi saa sita mchana, takriban pikipiki 56 huingia hospitalini hapo.
Kwa idadi hiyo, sh. 28,000 hukusanywa asubuhi kwa siku, licha ya zingine zinazoingia mchana na jioni. Kwa utaratibu huo, kwa wiki kuna uwezekano wa kukusanywa sh. 196,000 na kwa mwezi sh. 784,000.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia utozwaji ushuru huo, walisema wanashangazwa na kuhoji iwapo upo kisheria, kwani hospitali zingine hawatozwi.
“Hili tunalofanyiwa ni dhuluma na wizi, wanachukua fedha bila  kutoa stakabadhi, wakati utaratibu wa serikali unaelekeza kila anayelipia huduma apewe stakabadhi.
“Magari yanaingia na kutoka bila kulipa hata senti tano, kwa nini ushuru huu uwe ni kwa pikipiki tu, na ukitoka ukaingia tena unalipa,” alisema dereva wa pikipiki Yussuf Makame, mkazi wa Vingunguti.
Issa Saidi, mkazi wa Kigamboni, alisema mgambo wamekuwa wakiwatoza ushuru bila kuwapatia risiti, hiyo kuna shaka kuwa fedha hizo wanazitumia kwa maslahi binafsi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru