Thursday 22 August 2013

Ajali ya ndege yajeruhi saba


Na LILIAN JOEL, ARUSHA
ABIRIA saba waliokuwa wakisafiri kwa ndege ndogo kutoka Bukoba kwenda jijini Dar es Salaam, kupitia Zanzibar, wamenusurika kifo baada ya ajali kutokea.
Ndege hiyo ilianguka jana ndani ya Ziwa Manyara, baada ya kupata hitilafu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Libaratus Sabas,  alithibitisha kutokea ajali hiyo, akisema ilitokea jana mchana.
Akizungumza kwa simu, Sabas alisema majeruhi waliokolewa na boti za wavuvi na kupelekwa Hospitali ya Rufani ya Selian, jijini Arusha kwa matibabu.
Kamanda Sabas alisema alipokuwa akizungumza hakuwa na orodha ya majina ya abiria waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.
Hata hivyo, habari zilizopatikana hospitalini zinasema miongoni mwa abiria wa ndege hiyo ni wakili kutoka Kampuni ya IMMA ya jijini Dar es Salaam, Protas Ishengoma, ambaye ni miongoni mwa majeruhi wanne waliopata majeraha madogo.
Abiria mwingine ni Meeda Naburi na aliyetambulika kwa jina moja la Kashasha.
Majeruhi sita kati ya saba wa ajali hiyo walipelekwa hospitali kwa kutumia helikopta iliyokodiwa na baadhi ya mawakili wa jijini Arusha na ndugu wa majeruhi.
Akizungumza kwa simu kutoka eneo la tukio, kabla ya kusafirishwa hadi jijini Arusha kwa matibabu, Naburi alisema kabla ya ajali, rubani aliwataarifu kuwa injini moja kati ya mbili za ndege hiyo ilipata hitilafu.
Samuel Rugemalila, aliyejitambulisha kuwa ndugu wa majeruhi, akizungumza na waandishi wa habari akiwa hospitali, alisema abiria hao walikuwa wakitoka msibani Bukoba.
“Kwa mujibu wa maelezo ya majeruhi, injini moja ilipata hitilafu wakiwa umbali wa futi 21 kutoka usawa wa bahari, ndipo rubani alipofanya jitihada za kutua kwa dharura kwenye uwanja mdogo wa Manyara, kabla ya injini ya pili kuzima wakiwa futi 14 kutoka usawa wa bahari,” alisema.
Rugemalila alisema rubani alipogundua kuwa ndege isingetua salama katika uwanja huo, aliamua kutua ndani ya maji kwenye Ziwa Manyara.
“Tunamshukuru Mungu ndugu zetu wako salama licha ya kupata majeraha madogo. Kwa mujibu wa maelezo ya madaktari, maisha yao hayako hatarini,” alisema.
Ajali hiyo imetokea ikiwa ni wiki chache baada ya nyingine iliyohusisha ndege ya madaktari wasio na mipaka (Flying Doctors) kuanguka wilayani Ngorongoro.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru