Thursday 22 August 2013

Mtikisiko Jeshi la Polisi


NA SELINA WILSON
MAOFISA wanne wa Jeshi la Polisi, wamevuliwa madaraka na mmoja amesimamishwa kazi kutokana na kushindwa kuwajibika katika mambo ya msingi na kusababisha uhalifu kutokea.
Licha ya hao, askari watatu wamefukuzwa kazi wakituhumiwa kushirikiana na matapeli kumbambikia fuvu mfanyabiashara, mkazi wa Dumila, Samson Mwita, kwa lengo la kujipatia fedha.
Wakati hayo yakifanyika, ofisa mwingine amepandishwa cheo kwa kuanika madudu ya askari wenzake.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa mkakati wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wa kusafisha Jeshi la Polisi na kujenga nidhamu miongoni mwa askari.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya uchunguzi wa kamati ya watu watatu aliyoiunda kuchunguza matukio mbalimbali yaliyotokea hivi karibuni.
Alisema wizara inaendelea kupambana na askari wanaochafua jina la jeshi hilo na kwamba, halitamvumilia yeyote atakayebainika kwenda kinyume cha utaratibu wa kinidhamu wa jeshi hilo.
Dk. Nchimbi alisema waliofukuzwa kazi na kushitakiwa ni askari E 4344 Sajini Mohammed, E 3861 Koplo Nuran wa kituo cha polisi Dumila na Sajini Sadick Madodo wa kituo cha polisi Dakawa, mkoani Morogoro, ambao walishirikiana na matapeli Rashid Shariff na Adam Peter, kumbambikia fuvu Mwita.
Alisema Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mvomero, Inspekta Jamal Ramadhan, Mkuu wa Kituo cha Polisi Dumila, Inspekta Juma Mpamba na Mrakibu Msaidizi (ASP), Daniel Bendarugaho, wamevuliwa madaraka kutokana na tukio hilo.
Dk. Nchimbi alisema Inspekta Jamal alishindwa kuchukua hatua dhidi ya askari hao, ambao walimweleza kuna dili la kupata fedha, ambalo alikataa kushiriki lakini hakuchukua hatua dhidi ya askari na uhalifu ukafanyika.
Pia anadaiwa kushindwa kumkamata mtuhumiwa wa utapeli Adam Peter, aliyekuwa kinara wa tukio hilo. Hata hivyo, alisema kamati ya uchunguzi ilimshinikiza kumkamata.
Waziri alisema Inspekta Mpamba wa Kituo cha Dumila amechukuliwa hatua kutokana na kuonyesha udhaifu katika utendaji kazi, kwa kutosimamia kikamilifu askari wa chini yake.
Kutokana na hilo, alisema  amesababisha kutengeneza kesi ya fuvu la binadamu ili kujinufaisha kinyume cha maadili ya kazi.
Wengine waliovuliwa madaraka ni Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Arusha, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Ramadhani Giro, na Mrakibu Msaidizi (ASP), Daniel Bendarugaho, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma.
Alisema ASP Bendarugaho amevuliwa madaraka kutokana na tukio la mauaji la Desemba 25, mwaka jana, lilitokea katika kituo cha polisi Heru Ushingo, wilayani Kasulu, ambapo askari D 8622 Koplo Peter na G 1236 Konstebo Sunday, walimpiga Gasper Sigwavumba (36) na kumweka mahabusu. Alikufa siku moja baadaye.
Waziri Nchimbi alisema ASP Bendarugaho akiwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kasulu, hakuwa makini katika kusimamia upelelezi wa jalada la kesi kuhusu mauaji ya Sigwavumba, hivyo kuvuliwa madaraka. Alisema upelelezi wa tukio hilo utaanza upya.
Kuhusu Mkuu wa FFU Arusha, ASP Giro, alisema katika tukio la Mei 18, mwaka huu, askari wawili wa kituo cha Ngarenanyuki, wilayani Arumeru, walifukuzwa kazi baada ya kukiri kusafirisha bangi kwa kutumia gari la polisi namba PT 2025, aina ya Toyota Land Cruiser.
Alisema mkuu wa kikosi hicho kwenye mkoa ndiye mwenye mamlaka ya kupanga matumizi ya magari, lakini alishindwa kuyadhibiti na kusababisha litumie kusafirisha kilo 540 za bangi, zenye thamani ya sh. milioni 81 na kukamatwa mkoani Kilimanjaro.
Dk. Nchimbi alisema kutokana na hilo, ASP Giro, amevuliwa madaraka kwa kushindwa kuwasimamia ipasavyo askari na maofisa walio chini yake na kusababisha uhalifu kutokea.
Alisema ofisa aliyesimamishwa kazi ni Inspekta Isaack Manoni, ambaye ameagiza ashitakiwe kijeshi kwa tuhuma za kumtorosha askari F 1734 Koplo Edward, aliyekuwa dereva wa gari la polisi lililokamatwa na bangi.
Dk. Nchimbi alisema Inspekta Manoni alitakiwa kumpeleka askari huyo kukabidhi vifaa vya Jeshi la Polisi, lakini alizembea na kusababisha mtuhumiwa kutoroka.
Alisema Inspekta Salum Kingu, amepewa onyo kwa kuzembea katika tukio hilo, kwani alidaiwa kubaki kwenye gari umbali wa kilomita 80 kutoka nyumba ya mtuhumiwa kitendo ambacho kilichangia atoroke.
Waziri alisema Inspekta Mikidadi Galilima, naye amepewa onyo kwa kutotimiza wajibu wake katika kumshauri Mkuu wa FFU wa Arusha katika ukaguzi na usimamizi wa rasilimali za kikosi na kufichwa ukweli baada ya Koplo Edward kuiba magurudumu ya gari la polisi na kuweka ya zamani, jambo ambalo ni kosa kwa kiongozi.
Waziri Nchimbi alisema Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Francis Duma, aliyekuwa kiongozi katika tukio la kukamata gari la Jeshi la Polisi lilibeba bangi mkoani Kilimanjaro, amepandishwa cheo.
Dk. Nchimbi ameagiza askari wengine 14 walioshirikiana naye wapewe zawadi inayostahili na Mkuu wa Jeshi la Polisi Said Mwema.
0000

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru