Monday, 27 October 2014

CCM: Ndoa ya wapinzani ‘feki’



  •  Yasema kuing’oa madarakani ni ndoto za alinacha
  •  Viongozi wa vyama vilivyoungana kila mmoja anatafuta ulaji
  •  Mangula awaonya viongozi wa wilaya kutowagawa wanachama

NA SELINA WILSON
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema  hakitishiwi nyau kuungana kwa vyama vinne vya upinzani kwa lengo la kuking’oa madarakani.

 Kimesema muungano huo wa wapinzani si halali na ni sawa na ndoa ya mkeka.
Pia kimesema ni ndoto za alinacha kwa wanandoa hao wa msimu, ambao kila mmoja anatafuta ulaji, kuing’oa CCM, ambayo imesimamia maendeleo ya nchi pamoja na kuifanya kuwa na amani na mshikamano.
Kauli hiyo imetolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara, Philip Mangula, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ndoa hiyo ya wapinzani.
Ndoa hiyo ilifungwa juzi katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, na viongozi wa vyama hivyo, Freeman Mbowe (CHADEMA), James Mbatia (NCCR-MAGEUZI), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Emmanuel Makaidi (NLD).
Kwa mujibu wa viongozi hao, makubaliano hayo yanalenga kuhakikisha wanaing’oa CCM madarakani katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na ule wa rais na wabunge. Pia kuungana na kuhamasisha wananchi kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.
Hata hivyo, habari za kuaminika zinasema kuwa, vyama hivyo vimejificha chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ili kukwepa mawimbi makali kutokana na vyote kukabiliwa na migogoro mizito inayohatarisha uhai wake.
Mangula alisema takwimu zinaonyesha kuwa wapinzani hawana uwezo wa kuing’oa CCM, kwani wamekuwa wakipata asilimia 61 hadi 89 katika uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani na kuwaachia wapinzani asilimia chache.
Pia alisema Watanzania wamekuwa wakipigia kura CCM kutokana na kuvutiwa na sera zake za maendeleo, amani na mshikamano, tofauti na wapinzani ambao wamekuwa wakipiga kelele bila kuonyesha uwajibikaji kwa vitendo.
“Kwa takwimu hizo, maana yake CCM ikipata asilimia 89 ya kura, vyama vyote vya upinzani vinagawana asilimia ndogo, hivyo ndoa yao ni kama ya mkeka na hakuna uhusiano wowote wa kuishinda CCM,” alisema.
Alitoa mfano wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi, ambao CCM ilishinda kwa asilimia 80, mwaka 2000 asilimia 87 na mwaka 2005 ilishinda kwa asilimia  89 katika kura za wabunge.
Kwa upande wa kura za Rais, mwaka 1995 ilishinda kwa asilimia 61.8, 2000 ilishinda kwa asilimia 71 na mwaka 2005 CCM ilishinda kwa asilimia 80.2 huku vyama vyote vikigawana asilimia 38 mpaka 20.
“Kutokana na hali hiyo, nawatakia kila kheri na kwamba wakikosa mgombea katika uchaguzi mkuu wa mwakani, CCM inaweza kuwakopesha kwa kuwa inao wengi,” alisema.
Mangula alisema muungano huo wa wapinzani hautapunguza idadi ya mashina wala matawi ya CCM, hivyo ndoto zao kushika dola hazitatimia.
Chini ya ndoa hiyo ya mkeka, viongozi hao walisema watasimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi wa mwakani na katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa Desemba 14, mwaka huu, pia vitaungana.
Muungano huo wa vyama vinne vya upinzani chini ya UKAWA, ulianzia katika Bunge Maalumu la Katiba, ambapo baadae walisusia vikao hivyo na hatimaye Bunge liliendelea na kupata theluthi mbili za wajumbe kwa Bara na Zanzibar na Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi kupatikana kwa kishindo.
Mangula aonya
Katika hatua nyingine, Mangula amewaonya viongozi wa CCM wa ngazi za wilaya kutowagawa wanachama kwa lengo la kuimarisha makundi yao, badala yake waimarishe kundi moja la CCM.
Alisema viongozi wa Chama katika wilaya na mikoa, wakiwemo wabunge na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), wanapaswa kuhakikisha Chama kinafanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa. 
Mangula alisema yapo maeneo wabunge na wajumbe wa NEC wanavutana kwa lengo la kupanga safu, jambo ambalo alisema kamwe  halitavumiliwa na watakaobainika wataadhibiwa.
“Wakati huu ni wa kuimarisha kundi moja la CCM ili iweze kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani, lakini si muda wa kuimarisha kundi la mtu fulani,” alisema.
Mangula alisema uzoefu unaonyesha kwamba maeneo ambayo CCM ilishindwa katika uchaguzi, sababu zilitokana na makundi ndani ya Chama, hivyo aliwaonya viongozi hao kuwaachia wanachama waamue.
Alisema amekuwa akifanya ziara na kufuatilia maendeleo ya Chama katika maeneo mbalimbali nchini, lakini yapo maeneo ambayo viongozi hawaelewani kwa sababu ya makundi yasio na tija kwa Chama.
Mangula alisema CCM inafuatilia kwa kina maelekezo yake wa viongozi wa mikoa, wilaya, kata, matawi na mashina na yeyote atakayebainika kuvuruga uchaguzi huo kwa sababu za kuimarisha kundi lake, Chama kitamchukulia hatua.
Akizungumzia mkakati wa Chama katika uchaguzi huo, Mangula alisema CCM ina mtandao wa uongozi hadi ngazi ya tawi, ambao unajisimamia katika mipango yao.
“Tutashinda uchaguzi wa serikali za mitaa na kwamba hakuna kiongozi wa kitaifa atakayekwenda kufanya kampeni kwenye uchaguzi huo. Katika vijiji na mitaa, CCM ina viongozi wanaoaminika kwa wananchi na ndio watakaofanya kampeni,” alisema.
00000

000000

00000

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru