Monday, 9 March 2015

Vigogo wa Escrow wapumulia mashine

Kama unahitaji kutangaza biashara yako kupitia tovuti hii, wasiliana na idara ya masoko au fika ofisini kwetu mtaa wa Lumumba, mkabala na Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
***   ***   ***  ***   ***  ***   ***   ***   ***


.... Wapumulia mashine

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

LICHA ya kuanza kuhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma na mamlaka zingine za uchunguzi, hali bado ngumu kwa watendaji wa umma waliohusika kwenye kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Tangu kuibuliwa kwa kashfa hiyo, mawaziri wawili Profesa Anna Tibaijuka (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini) wameshajiuzulu kwenye nafasi hizo.
Pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, naye ameachia ngazi kutokana na kuhusishwa kwenye kashfa hiyo huku Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakim Maswi, akisimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi yake.
Hata hivyo, kuna watendaji wengine wa ngazi za juu, ambao kwa sasa wanahojiwa na Baraza la Maadili kuhusiana na kashfa hiyo, ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeendelea kuwakalia kooni kikiibana serikali kutaka hatua zaidi zichukuliwe.
Tayari kwa upande wake, CCM imewasimamisha Andrew Chenge, William Ngeleja na Profesa Tibaijuka kuhudhuria vikao vya maamuzi ndani ya Chama. Chenge na Ngeleja ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na Tibaijuka ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema juzi kuwa ni muhimu kwa watendaji wote wanaohusika kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yao.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Dodoma, Kinana alisema atamshauri Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kwa kuwa si vyema kwa watumishi wa serikali kuendelea kuwepo maofisini wakati wanakabiliwa na tuhuma nzito.
Alisema ili uchunguzi unaoendelea kwa sasa uwe na mantiki, ni vyema watumishi hao wakaziacha ofisi kwa sasa na kukaa kando ili uchunguzi uendelee.

“Namshauri Balozi Sefue kuwa hata kama watumishi hao bado wanahojiwa, ni vyema wakae kando hadi hapo tuhuma dhidi yao zitakapobainika kama ni kweli au hapana.

“Sina madaraka ya kumuamrisha Katibu Mkuu Kiongozi kwani mwenye madaraka hayo ni Rais Jakaya Kikwete. Ndani ya CCM tumechukua hatua na tunaendelea, tumewasimamisha viongozi wanaotajwa kuhusika na tukikamilisha uchunguzi wetu tutaona njia sahihi ya kuchukua,” alisema Kinana.

Kinana aliongeza kuwa kashfa ya Escrow inahusisha fedha za Watanzania na kwamba, kibaya zaidi kumeibuka vikundi vya kuanza kuwatetea wahusika.

“Hawa watu kukiwa na firigisi za kuku wanaanza kula wao, kukiwa na kuku kapikwa wao ni wa kwanza kula hii si sawa,” alisema Kinana na kuongeza: “Kuwachekea wezi na kuwatetea ni tabia mbaya, ambayo imeaanza kujitokeza huku mtu wa kawaida akiiba kuku tu anafungwa.”

Alionya tabia ya watumishi kuwa watukufu badala ya kutanguliza maslahi ya kuwahudumia watanzania na kushangazwa na maofisa watendaji wa kata kutaka kuitwa waheshimiwa, wakati zamani walikuwa wakiitana kwa majina na si cheo.

Wafadhili waitosa Ukawa
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnaye, alifichua siri ya kundi linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kujipanga kususia kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Aliueleza umma huo kuwa, viongozi wa Ukawa walipewa fedha na wafadhili kwa ajili ya kuendesha harakati wakati wa mchakato wa Katiba. Alisema harakati hizo zilianza wakati wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya kukusanya maoni ya wananchi na baadaye kwenye Bunge Maalumu.
Hata hivyo, alisema wakati wanapewa fedha hizo, waliaminiwa kuwa zitatumika vizuri, lakini hadi wanasusia vikao vya Bunge, walikosa hoja na maelezo sahihi ya matumizi ya fedha hizo.
“Mtakumbuka Ukawa waliposusia Bunge la Katiba na hasa baada ya kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa, walisema watapita nchi nzima kuwahamasisha wananchi kupiga kura ya hapana, lakini sasa wameibuka na kutangaza kususia bila kutoa sababu za msingi.
“Sasa mchezo uko hivi. Baada ya Ukawa kukaa, wakagundua hawana uwezo wa kuwashawishi wananchi waikatae Katiba Inayopendekezwa. Pili wakaamua wapeleke hoja ya kupinga Katiba hata kama hawatafanikiwa kuizuia mtaani. Hivyo wakaamua kwenda kuzisaka hizo pesa.
“Walipofikisha madai yao huko kwa watoa pesa, wakatakiwa kupeleka maelezo ya matumizi ya fedha za awali, ambayo hawana na wamebanwa waseme mpango wa kuzuia Katiba Inayopendekezwa, wakajaribu kudanganya lakini mwisho wa siku wakagonga ukuta,” alisema Nape na kusababisha uwanja mzima kulipuka.
Alisema Ukawa wamegoma kushiriki mchakato huo si kwa kuwa Katiba Inayopendekezwa ina kasoro, la hasha bali wanafanyia kazi matumbo yao na si maslahi ya Watanzania.
Hata hivyo, Nape alisema kwa sasa vigogo wa Ukawa wanaendelea kujitahidi kubembeleza wafadhili hao kuwapa fedha kwa ajili ya uchaguzi na pindi majadiliano yakikamilika, ataweka mambo hadharani.
Alisema pamoja na kuendelea kuzungusha bakuli, bado Ukawa wana hali ngumu kutokana na fedha walizopewa awali kutumika vibaya kwa maslahi ya wachache.

Vigogo wenye nafasi nyingi
Wakati huo huo, CCM imewataka wanachama wake, ambao hawana muda wa kuzitumikia nafasi walizoomba ndani ya Chama kwa kuwa na majukumu mengine, ni vyema wakaziachia.
Agizo hilo limetolewa na Kinana, alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu mkoa wa Dodoma, juzi, katika ukumbi wa White House.
Alisema kuna baadhi ya makada wa CCM wana nyadhifa zaidi ya moja ndani na nje ya Chama, jambo ambalo linawafanya kutokuwa na nafasi ya kuwatumikia wananchi ipasavyo.
Alisema inawezekana mtu mmoja akawa waziri na wakati huo huo akawa mjumbe wa NEC na pia mjumbe wa kamati ya siasa, wakati si mara zote anaweza kuwepo kwenye kila kikao.
Kinana alisema CCM inaangalia utaratibu wa utoaji wa nyadhifa hizo ili kuepuka mtu mmoja kujilimbikizia nafasi.

“Kama wewe ni mjuumbe wa kamati kuu, basi achia vyeo vingine na wenzako waweze kuwatumikia wananchi, sio kila sehemu wewe upo hii si sahihi,” alisema na kuongeza:

“Na ukiona mtu wa aina hiyo ujue kuwa anataka kujilinda kutoka nafasi moja kwenda katika nafasi nyingine na si vinginevyo.”

Aidha, alisema CCM ni chama bora chenye kila utaratibu unaotakiwa ndani ya chama, lakini wanokiaharibu ni viongozi wenyewe.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru