Tuesday, 21 April 2015

Mamia wauaga mwili wa DC Kyerwa


 NA REHEMA MAIGALA
RAIS  Jakaya Kikwete, ameongoza mamia ya waombelezaji kuuaga mwili wa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Luteni Kanali (mstaafu) Benedict Kitenga.
Mwili wa Kanali Kitenga uliagwa jana katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, ambapo viongozi mbalimbali wakiwemo wa CCM na serikali walihudhuria.
Kabla ya kufariki dunia, Kanali Kitenga alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akipatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na shinikizo la damu.
Anatarajiwa kuzikwa leo katika Makaburi ya Kola, manispaa ya Morogoro.
Kanali Kitenga alizaliwa Juni 15, 1953 katika kijiji cha Shungu wilayani Kilombero, Morogoro. Alitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka 36 kabla ya kustaafu rasmi Juni 30, 2008.
Mara baada ya kustaafu utumishi ndani ya JWTZ, Rais Kikwete alimteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara na baadaye Kyerwa, ambapo hadi anakutwa na umauti alikuwa akiingoza.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongella, alisema Tanzania imempoteza mtu muhimu na aliyekuwa mstari wa mbele kuhakikisha taifa linasonga mbele.
“Hili ni pigo kubwa tulilopata kwa mzee wetu. Tutamkumbuka daima kwa umakini wake katika shughuli zake za kila siku,” alisema Mongella.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, alieleza kushitushwa kwake na kifo cha  Kanali Kitenga na kusema alikuwa kiongozi mhamasishaji wa maendeleo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru