Friday, 27 June 2014

Viwango vya askari akiumia kazini vyatajwa


KIWANGO cha juu cha fidia kwa polisi aliyepoteza maisha akiwa kazini ni sh. milioni 15 wakati kiwango cha fidia kwa aliyeumia kazini ni kati ya sh. milioni moja na milioni tano.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Perreira Ame Silima, alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Saidi Zuberi (Fuoni-CCM), aliyetaka kujua viwango vya fidia kwa polisi wanaopoteza maisha wakiwa kazini na wanaoumia.
Hata hivyo, Silima alisema viwango vinavyotolewa kwa polisi walioumia kazini hutegemea kiwango cha maumivu.
Naibu Waziri alisema pia kuwa likizo za uzazi na ugonjwa kwa watumishi wa Jeshi la Polisi hazina tofauti na watumishi wengine wa serikali.
Alisema sheria ya likizo ya uzazi kwa polisi wanaume wakati wake zao wanapojifungua, bado haijaanza kufanyakazi katika jeshi hilo na wizara yake inaendelea kulishughulikia suala hilo.
Akijibu swali la msingi la Jaku Hashim Ayoub (Kuteuliwa),  Silima alisema serikali huwalipa fidia askari wanaofariki wakiwa kazini kwa mujibu wa kanuni za fidia za askari polisi na magereza za mwaka 2010 iliyotangazwa kwenye gazeti la serikali GN. 270 ya 30/07/ 2010.
Alisema pia kuwa likizo za askari polisi zipo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za ajira ya polisi. Alisema utaratibu huo unazingatia masharti ya ajira ya askari, ambapo hupewa likizo ya siku 84 kwa kipindi cha miaka mitatu, sawa na siku 28 kwa kila mwaka.


"Hivyo si kweli kwamba taratibu za likizo za uzazi na za mwaka zinapingana na misingi ya haki za wafanyakazi. Lakini katika maboresho yanayoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi, taratibu mbalimbali zitaangaliwa upya, ikiwemo likizo," alisema.


Katika swali lake, Jaku alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia askari polisi wanapoumia kazini na pia katika kuangalia upya haki ya likizo ya uzazi na likizo ya mwaka oli zilingane na misingi ya haki za wafanyakazi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru