Wednesday 26 June 2013

Kampuni 34 zapigwe ‘stop’ kushiriki zabuni za umma


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), imezifungia kampuni 34 kwa mwaka mmoja, kutoshiriki zabuni za manunuzi ya umma kwa tuhuma za kufanya udanganyifu.
Zinadaiwa kutotekeleza mikataba yao kwa wakati na kufanya malipo hewa.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Jaji Thomas Mihayo, aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua warsha ya siku tatu ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, ya kuwajengea uwezo wa kusimamia sheria za ununuzi katika sekta ya umma ya mwaka 2011.
Jaji Mihayo, alisema kati ya hizo, kampuni 24 zilifungiwa kwa kushindwa kutekeleza mikataba na taasisi za umma na nane zilifungiwa kwa ajili ya kulipa malipo kwa kazi ambazo hazikufanyika.
Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Nyegezi J.J. Construction Limited, Muson Engineering Limited na Jossam and Company Ltd.
Alisema zingine tatu zinaendelea kufungiwa mapka hapo zitakaporejesha fedha walizolipwa.
Alizitaja kuwa ni pamoja na kampuni ya Man-Ncheye-Pa-Co, Ltd ya Bunda, Tengo Construction Limited ya Morogoro na Icon Engineers ya Mwanza.
Jaji Mihayo alitoa wito kwa wakurugenzi kutoa taarifa kwa kampuni zilizojiingiza katika udanganyifu au kushindwa kutekeleza mikataba ili nazo zifungiwe.
Alisema ni vyema kusimamia na kuiheshimu sheria ya manunuzi ya umma, ili kulinda fedha za serikali zinazotumika katika ununuzi wa vifaa mbalimbali.
Alisema kwa mujibu wa ripoti ya utendaji ya mwaka 2011/2012 ya PPRA imebaini zaidi ya sh. trillion 4.3 zilitumiwa na taasisi za umma 319 kufanya manunuzi ya kandarasi za ujenzi, vifaa na huduma, kwa mwaka wa fedha 2011/12.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dk. Ramadhani Mlinga, alisema kiwango cha uzingatiaji wa sheria, kimekuwa kikikuwa
kutoka asilimia 39, 2006/2007 mpaka  asilimia 73, 2009/2010.
Hata hivyo, alisema mwaka 2010/2011, kiliporomoka kwa asilimia 68.
Dk. Mlinga, alisema pamoja na mafanikio hayo, PPRA inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya kuendeleza utaratibu wa kuzipatia mafunzo taasisi za umma, hususan serikali za mitaa kuhusu sheria, kanuni na utaratibu wa manunuzi ya umma.
Nyingine aliitaja kuwa ni ya kujiimarisha  kimuundo kwa kuajiri watumishi wa
kutosha na wenye ujuzi.
Akizungumzia warsha hiyo, alisema imelenga kuwawezesha wajumbe wa Bodi kuelewa wajibu wao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru