Tuesday 25 June 2013

MKURABITA yaonyesha njia ya maisha bora

na mwandishi wetu
MPANGO wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge nchini (MKURABITA), umeendelea kuwa mkombozi wa watanzania katika kufikia Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.
Hatua hiyo imetokana na kuendelea kugawa hati miliki za kimila kwa wananchi mbalimbali nchini ikiwa ni kuwawezesha kupata fursa za mikopo kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Mratibu wa MKURABITA Seraphia Mgembe, alisema hayo juzi wakati akitoa tathimini ya kazi ya kutoa hatimiliki hizo kwa wakulima wa chai katika wilaya za Mbinga, Mufindi na Njombe.
Kazi ya kutoa hatimiliki hizo ni mwendelezo katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo wiki mbili zilizopita wananchi wa wilaya ya Rungwe walikabidhiwa hati miliki za kimila.
Alisema maisha bora kwa kila Mtanzania hayawezi kupatikana kwa wananchi kukaa vijiweni ama kubweteka bila kufanya kazi na kusubiri serikali kufanya kila kitu.
Seraphia alisema jukumu la serikali ni kujenga mazingira bora kwa wananchi kuzalisha mali ikiwa ni pamoja na kutumia vizuri rasilimali walizonazo kama dhamana ya kupata mitaji.
“Tunaendelea kutoa hati miliki za kimila ili kuwezesha wananchi kupata mitaji kwa kutumia rasilimali walizonazo. Kazi inayoafuata ni kuendelea kuwajengea uwezo na jinsi ya kuzitumia kama dhamana,” alisema.
Alisema maendeleo ya kweli na ya haraka ni yale yanayotokana na matumizi ya rasilimali zinazowaunganisha wananchi na MKURABITA imekuwa kiunganishi muhimu baina yao na taasisi za fedha nchini.
Katika hatua nyingine, wakuu wa wilaya za Njombe, Sarah Dumba na Mufindi, Evarista Kalalu, waliipongeza MKURABITA kutokana na jitihada za kuhakikisha wakulima wa chai wanayamiliki rasmi mashamba ili kuwakomboa na umasikini.
Walisema kuwa awali wakulima hao walikuwa na utajiri, ambao haukuwafainisha zaidi ya kulima na kuuza mazao yao, lakini kwa sasa watakuwa wamiliki na pia watatumia hati miliki zao kukopa fedha kwenye taasisi za fedha. Jumla ya hatimiliki za kimila zimetolewa kwa wakulima wa chai.

MKUU wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba, akimkabidhi hati miliki ya kimila, mkazi wa kijiji cha Iwafi, Everina Jonas, wakati wa hafla fupi ya MKURABITA kukabidhi hati miliki za kimila kwa wakulima wa chai wa Rungwe, Mfindi na Njombe. Katikati ni Mratibu wa MKURABITA, Seraphia Mgembe. (Picha kwa hisani ya PPRA).

WANANCHI wakifurahi kukagawiwa hati miliki za kimila kutoka kwa mmoja wa maofisa wa MKURABITA

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru