Tuesday 25 June 2013

Kampuni za simu zai-beep serikali


Na Hamis Shimye
MSIMAMO wa serikali kuzibana kampuni za simu kulipa kodi ya mapato, umechukua sura mpya, baada ya Umoja wa Wamiliki wa Simu za Mkononi Tanzania (Moat) kutunisha misuli.
Moat imesisitiza uamuzi wa kupandisha gharama za simu kwa watumiaji uko pale pale na kwamba, utaanza Jumatatu ijayo.
Kwa upande wake, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema itatekeleza kwa vitendo uamuzi wa serikali katika ukusanyaji kodi kwenye kampuni hizo, ambazo zinatajwa kupata faida kubwa huku zikilipa kodi kiduchu.
TRA imesema itaanza kazi ya kukusanya kodi kikamilifu Jumatatu, ikiwa ni miongoni mwa mambo yaliyopitishwa na Bunge katika bajeti ya serikali kwa mwaka 2013/2014.
Akizungumza kwa simu jana, Mkurugenzi wa Huduma za Elimu wa TRA, Richard Kayombo, alisema wao ni watekelezaji wa sheria.
“Jukumu letu ni kukusanya kodi na si vinginevyo, hivyo iwapo serikali na Bunge zimeridhia na kupitisha, hakuna shida kwa upande wetu kwa kuwa ndiyo jukumu letu,’’ alisema.
Alisema TRA kwa sasa haiwezi kusema chochote kwa kuwa bado haijapewa au kutaarifiwa kuhusu kiwango cha kodi cha kukusanya, kwani bajeti ya serikali bado haijaanza kutumika.
“Mwaka wa fedha unaisha Juni 30, mwaka huu, hivyo natarajia Julai Mosi kila kitu kitajulikana,’’ alisema.
Serikali katiba bajeti iliyopitishwa na Bunge juzi, imependekeza kuzitoza kodi kampuni hizo kwa asilimia 14, badala ya asilimia 12 ya awali.
Kwa upande wake, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema haihusiki na kodi, bali utoaji leseni.
Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando, alisema msimamo wa kampuni hizo ni kuongeza gharama kwa watumiaji simu.
Kwa nyakati tofauti, wabunge na serikali wamesema kuongeza gharama za matumizi ya simu kunalenga kuendelea kuwanyonya wananchi.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alisema juzi kuwa, kampuni hizo zinatumia gharama ndogo kujiendesha, hivyo serikali inatarajia gharama zishuke zaidi na si kuongezeka.
Alisema gharama za uendeshaji za kampuni hizo zimepungua kutokana na kutumia mkongo wa mawasiliano wa taifa.
Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene, akijibu hoja za wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2013/2014, alisema suala la kampuni za simu kutokulipa kodi stahili limekuwa kilio cha muda mrefu.
Alisema serikali itaanza kuzibana kampuni hizo ili zilipe kodi na mapato stahili, pia kuwashirikisha Watanzania katika umiliki wake.
Katika kufanya hivyo, alisema serikali itaweka mtambo maalumu wa kufuatilia miamala yote ya kampuni hizo na kuziingiza katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru