Wednesday 19 June 2013

Mji wa Biharamulo kuwa halmashauri
MCHAKATO wa kuufanya mji wa Biharamulo, mkoani Kagera,  kuwa halmashauri ya mji mdogo unatarajiwa kukamilika Novemba, mwaka huu.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Aggrey Mwanri, alisema hayo alipojibu swali la Dk. Anthony Mbassa (Biharamulo -CHADEMA), aliyetaka kujua ni lini mchakato wa kuufanya mji huo kuwa halmashauri utakamilika.
Mwanri alisema mchakato huo utakamilika baada ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) wa Kagera kufanya kikao cha mwishoni mwa mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwanri, RCC itakutana kujadili masuala mbalimbali, ambapo moja ya ajenda ni suala la Halmashauri ya Mji wa Biharamulo. 
Alisema mchakato huo ulianza mwaka 2010, kwa kuanza kupima upya eneo la kiutawala, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kata mpya mbili ili kufanya idadi kufikia tano kama sheria inavyotaka.
Mwanri alisema suala hilo limechukua muda kutokana na wilaya ya Biharamulo kugawanywa na kuwa wilaya mbili za Biharamulo na Chato.
Naibu waziri alisema kisheria ili mji uweze kuwa na halmashauri unapaswa kuwa na watu 10,000 lakini Biharamulo imevuka kigezo hicho, kwani ina watu takriban 101,000.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru