Wednesday 26 June 2013

Ongezeko dawa za kulevya laogofya


Na Theodos Mgomba, Dodoma
KASI ya ongezeko la dawa za kulevya nchini imeanza kuitisha serikali, ambayo imesema ikiachwa inaweza kuendelea kuleta athari kubwa.
Imesema wafanyabiashara wa dawa za kulevya ni watu hatari na kwamba, wanaweza kuingilia misingi ya kiutawala, hivyo Watanzania hawana budi kuipiga vita kwa nguvu zote.
Kauli hiyo imetolewa jana mjini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kwa niaba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kwenye maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani.
Katika hotuba hiyo, Pinda amesema miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.
Alisema iwapo biashara hiyo haitadhibitiwa kikamilifu na kuachwa ikaendelea moja ya athari zitakazojitokeza ni kuingiliwa kwa misingi ya utawala na ongezeko kubwa la rushwa.
Pinda alisema wafanyabiashara wa dawa za kulevya baadhi wamekuwa wakiwatumia watendaji wa serikali katika kufanikisha mambo hayo haramu.
Waziri mkuu alisema kushamiri kwa biashara hiyo kunaongeza mtandao wa fedha haramu na kusababisha mfumuko wa bei, hatua itakayoongeza umasikini kwa wananchi wa kawaida.
“Biashara hii ni hatari, inapaswa kupigwa vita. Ikiachwa itaendelea kuleta athari kubwa na wananchi watashindwa kumudu huduma za kijamii, kama vile elimu na afya. Uwezo wa serikali katika kutoa huduma muhimu unaweza kupungua kutokana na biashara hii haramu,” alisema.
Alisema Watanzania wengi wamekuwa wakijihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi, hali inayoharibu taswira ya nchi kimataifa.
Waziri mkuu alitoa mfano kuwa, katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012, watuhumiwa 10,799 walitiwa mbaroni kwa kujihusisha na biashara hiyo nchini.
Katika kipindi hicho, alisema  Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na baadhi wamefungwa.
“Hali hii inaharibu taswira ya nchi kimataifa, Watanzania wasio na hatia wanapata usumbufu na kuwekewa masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali kutokana na sifa mbaya.
“Wachache wanafanya wengi wanapata usumbufu na kushindwa kutumia fursa za kibiashara zilizoko katika nchi za nje,” alisema.
Kuhusu ukamataji wa dawa hizo, alisema kumekuwa na juhudi kubwa zinazofanywa na vyombo vya dola na kwamba, kiwango kinachokamatwa ni kikubwa.
Hatua hiyo alisema inatokana na ulinzi mkali katika mipaka na maeneo mengine ya kuingia nchini, ambapo kuanzia mwaka 2010 hali imekuwa mbaya kuliko miaka ya nyuma.
Ukamataji mkubwa umekuwa ukifanyika eneo la kimataifa katika Bahari ya Hindi, ambako dawa hizo zimekuwa zikiingizwa kwa meli kubwa, ikiwa ni moja ya mbinu zinazotumiwa na wafanyabiashara.
Alisema kilo 914 za dawa za kulevya aina ya heroin zilikamatwa na kikosi kazi cha kuzuia uharamia, hali iliyodhihirisha kuwa kasi ya uingizaji wa dawa hizo ni kubwa.
Kwa upande wake, Kamishna wa Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo, alisema tume imekuwa na changamoto kubwa katika kudhibiti wafanyabiashara wa dawa hizo.
Alisema licha ya kudhibiti watu hao, pia imegundulika kuwa bangi imekuwa ikilimwa katika kila mkoa nchini.
Shekiondo alisema kitendo hicho kinahamasisha vijana wengi wa umri mdogo kuanza kuitumia kutokana na kulimwa katika mashamba na nyingine jirani na makazi ya watu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru