Wednesday 19 June 2013

Serikali yazionya NGO

SERIKALI imeyaonya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO), kuacha kueneza propaganda za uchochezi kuhusu utafiti wa madini ya urani katika Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida.
Onyo hilo lilitolewa jana,  bungeni mjini hapa, na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, alipojibu swali la nyongeza la Kapteni John Chiligati (Manyoni Mashariki - CCM).
Chiligati alitaka kujua kauli ya serikali kuhusu NGO zinazopita kueneza ujumbe kwa wananchi kupinga mradi wa uchimbaji urani katika vijiji vya Manyoni na Bahi, mkoani Dodoma.
Masele alisema serikali ina taarifa kuhusu asasi hizo, ambazo zimekuwa zikieneza ujumbe wa chuki kwa wananchi kuwa, watafukuzwa iwapo itagundulika kuna madini katika maeneo hayo.     
Naibu waziri alisema NGO hizo zinafanya propaganda kupitia ufadhili wa baadhi ya mataifa ya nje, ambayo yamekuwa yakiwania uchimbaji wa madini hayo adhimu duniani.
“NGO hizi zinacheza ngoma ambayo inapigwa na mataifa ya nje, ambayo yanawania kupata nafasi ya kupata madini haya yanayogombewa duniani. Hii yote inatokana na ukweli kwamba, urani ni madini ya kimkakati,” alisema.
Kuhusu maendeleo ya utafiti wa madini hayo unaofanywa na kampuni ya URANEX, Masele alisema unaonyesha wilayani Manyoni kuna kiasi kikubwa cha urani kinachofikia ratili milioni 29.
Alisema licha ya kiwango hicho kutosha kuanza shughuli ya uchimbaji, kampuni hiyo inaendelea kufanya utafiti wa kimaabara ili kutenganisha urani katika udongo wa mfinyanzi.
Masele aliwaasa wananchi wa Manyoni kutokuwa na hofu kuwa watafukuzwa kwenye maeneo yao uchimbaji utakapoanza.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru