Tuesday 25 June 2013

Sugu mbaroni kwa kumtukana Pinda


Na Theodos Mgomba, Dodoma
MBUNGE wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amekamatwa na polisi na kuhojiwa akituhumiwa kumtusi Waziri Mkuu Mizengo Pinda, katika mtandao wa kijamii.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema jana kuwa, mbunge huyo wa CHADEMA alikamatwa saa nane mchana akitoka bungeni na kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi, ambako alihojiwa kwa saa mbili na nusu.
Alisema Sugu alikamatwa baada ya kunaswa akimtukana waziri mkuu kuhusu utendaji wake wa kazi.
Mbunge huyo anatuhumiwa kumtusi waziri mkuu kutokana na kauli aliyoitoa hivi karibuni bungeni wakati wa maswali ya papo kwa hapo.
Pinda alivitaka vyombo vya dola, likiwemo Jeshi la Polisi kutowavumilia watu wanaotishia amani na utulivu nchini.
Kamanda alisema Sugu alidhaminiwa saa 10.30 jioni na mbunge wenzake wa CHADEMA, Tundu Lissu na mwalimu wa Shule ya Sekondari Viwandani.
Alisema mbunge huyo ametakiwa kufika tena polisi kesho saa tatu asubuhi kwa ajili ya kuendelea kuhojiwa.
Misime alisema polisi itaendelea kuchukua hatua kwa kadri itakavyoona inafaa, ikiwemo kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.
Alisema polisi haitasita kumkamata mtu yeyote anayepandikiza mbegu za chuki, zinazoweza kusababisha kuvunjika amani na utulivu nchini.
Kamanda amewataka wanaotumia mitandao hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Hivi sasa kumezuka tabia ya baadhi ya wanasiasa kutumia mitandao ya kijamii kuwachafua viongozi wa serikali, hivyo kujenga chuki kati ya wananchi, serikali na viongozi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru