Friday 28 June 2013

Vyama vya siasa mtegoni

Na Theodos Mgomba, Dodoma
SERIKALI imesema itachukua hatua kali kumaliza njama zinazofanywa na kundi la watu wachache, wanaopandikiza chuki za kisiasa na kidini nchini, hivyo kuvuruga amani na utulivu.
Imesema vyama vya siasa vitakavyobainika kuhusika na uvunjifu wa amani vitachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa mujibu wa sheria.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema hayo bungeni jana, alipotoa hotuba ya kuahirisha Bunge.
Alisema hatua hizo zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo, bila kujali hadhi na nafasi yake katika jamii.
Waziri Mkuu Pinda alisema kuna dalili za kuwepo vikundi vya watu wachache wasioitakia mema Tanzania, kwa kupandikiza chuki za kisiasa na kidini miongoni mwa wananchi.
Alisema pia vimekuwa vikileta mauaji na mapigano miongoni mwa wananchi.Sina shaka kuwa fujo, vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani, ikiwemo mashambulio ya mabomu Arusha na vurugu za Mtwara ni sehemu ya mikakati hiyo mibovu,’’ alisema.
Waziri mkuu aliwasihi viongozi wa serikali, kisiasa, kidini na wananchi kwa jumla, kila mmoja kwa nafasi yake kuwajibika ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa kisiwa cha amaTuendelee na mshikamano wa kukataa vitendo vya uvunjifu wa amani katika nchi yetu, kila mtu mwenye taarifa za kuwezesha kukamatwa kwa watu wanaohatarisha amani azitoe kwa vyombo vya dola na zitafanyiwa kazi kwa umakini kwa maslahi ya taifa,’’ alisema.

Pinda alisema katika kuhakikisha amani inadumishwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imewakutanisha viongozi wote wa vyama vya siasa na Jeshi la Polisi.

Alisema lengo la mkutano huo ni kueleza dhima ya polisi na vyama vya siasa katika kukua kwa demokrasia na amani nchini.

Kwa mujibu wa Pinda, katika mazungumzo hayo, viongozi wa vyama vya siasa walilaani tabia ya baadhi ya vyama kujihusisha katika kuvunja amani.

Alisema hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya vurugu yanayohusishwa na vyama vya siasa, huku sheria ya vyama vya siasa na kanuni zake zinakataza vyama kujihusisha na vurugu, kuigawa nchi kwa udini, ukabila rangi au aina yoyote ya ubaguzi, ambayo itasababisha amani kutoweka.

Pinda alisema sheria hiyo pia ipo wazi kuwa, chama kitakachobainika kufanya hayo kitafutwa kwa mujibu wa sheria.

“Nawakumbusha viongozi wenzangu wa kisiasa kuwa, demokrasia si kufuta vyama au kuvuruga amani ya nchi, bali ni kuwa na sera nzuri zinazowaunganisha Watanzania na kudumisha amani.

“Nawaomba wanasiasa na viongozi wenzangu, tusijaribu kuweka nchi yetu rehani kwa kuhamasisha kwa njia moja au nyingine wananchi kuvuruga amani. Tuwafundishe kupendana, kuvumiliana na kusaidiana,’’ alisema.

Katika hatua nyingine, waziri mkuu alisema serikali imeendelea kuwaondoa madarakani viongozi wasio waadilifu katika vyama vya ushirika, kutokana na kukithiri vitendo vya wizi, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Alisema vitendo hivyo vimesababisha baadhi ya vyama kuiingia kwenye migogoro na madeni makubwa, kutokana na hasara za mara kwa mara zinazosababisha wanachama kukata tamaa kuhusu ushirika.

Pinda alisema viongozi hao pia wametozwa fidia ili kurejesha fedha zilizofujwa na kwamba, utaratibu wa kuchukua hatua zaidi za kijinai unaandaliwa.

Waziri mkuu alisema serikali itaunda timu imara ya ukaguzi, ikihusisha wakaguzi kutoka katika halmashauri.

Bunge limeahirishwa hadi Agosti 26, mwaka huu, litakapokutana katika mkutano wa 12.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru