Wednesday 19 June 2013

Wafanyabiashara walanguzi kukiona

SULUHU ya kudumu juu ya ulanguzi wa wafanyabiashara wanaonunua mazao ya wakulima kwa ujazo uliozidi kipimo (lumbesa), itapatikana hivi karibuni baada ya serikali kuanzisha sheria ili kuwadhibiti.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Gregory Teu, alisema jana kuwa, chini ya sheria itakayowasilishwa katika mkutano ujao wa Bunge, watakaoendelea na tabia hiyo watapata adhabu kali.
Teu alisema hayo alipojibu swali la Mchungaji Luckson Mwanjale (Mbeya Vijijini -CCM), aliyehoji serikali inatoa tamko gani juu ya wizi huo, unaofanywa na wafanyabiashara.
Alisema wananchi wamekuwa wakiendelea kuwa masikini kutokana na kuuza mazao kwa mtindo wa lumbesa, hivyo serikali imeamua kutunga sheria kali itakayowabana wafanyabiashara.
“Naomba niwaeleze wakulima na wafanyabiashara kuwa, hakuna sheria inayowataka wakulima kupima mazao kwenye lumbesa. Nawaagiza wafanyabiashara kuacha mara moja mtindo huo wa kuwashurutisha wakulima kutumia lumbesa,” alisema.
Kuhusu kukithiri tabia hiyo, Teu alisema kunatokana na adhabu ndogo wanayopewa wafanyabiashara hao ya faini ya sh. 10,000 wanapobainika kufanya hivyo.
Alisema chini ya sheria mpya, serikali imeazimia wanaoendekeza tabia hiyo watatozwa faini ya sh. milioni 100 ama kifungo cha miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja.
“Kwa atakayefanya hivyo kwa mara ya pili atatozwa faini ya sh. milioni 200 ama kifungo cha miaka saba jela au vyote kwa pamoja,” alisema.
Alisisitiza wakulima ni lazima waendelee kupima mazao kwa uzito wa kilo 100 kwa gunia,  ambao unatakiwa kisheria na kwamba, anayefanya kinyume cha hapo ajue ni makosa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru