Wednesday 19 June 2013

Ulinzi ziara Obama waimarishwa

 

Na Mwandishi Wetu
ZIKIWA zimebaki wiki mbili kabla ya kuwasili kwa Rais wa Marekani, Barrack Obama, jiji la Dar es Salaam limeanza operesheni kubwa ya usafi ambayo imewakumba wasafisha viatu na wafanyabiashara ndogo ndogo katika maeneo ya Posta Mpya.
Kutokana na operesheni hiyo, zaidi ya watu 20 wamekamatwa baada ya kukutwa wakifanya shughuli zao katika maeneo yasiyoruhusiwa, huku ulinzi ukiimarishwa kwenye maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Kwa upande wa Manispaa ya Ilala, hususan maeneo yanayozunguka eneo la Ikulu, Posta Mpya na Posta ya Zamani na mitaa mbalimbali ya Kata ya Kivukoni, operesheni hiyo ilifanyika jana.
Mgambo wa manispaa, polisi jamii na askari polisi walishirikiana kuwaondoa watu hao hali iliyozua gumzo na manung’uniko miongoni mwa watu.
Rais Obama anatarajiwa kuwasili nchini Julai Mosi, mwaka huu, ikiwa ni ziara yake kwanza Barani Afrika baada ya kuchaguliwa kwa mara ya pili kuwa Rais wa Marekani.
Mbali ya Tanzania, Ras huyo atazitembelea pia nchi za Afrika Kusini na Nigeria.
Wakizungumza na Uhuru jana, baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam, walisema wanaamini operesheni hiyo inafanyika kwa ajili ya ujio wa Rais Obama.
Msemaji wa Manispaa ya Ilala Dar es Salaam, Tabu Shaibu, alisema manispaa hiyo iliamua kufanya usafi kwa kuwa suala la uchafu wa mazingira limekuwa kero ya muda mrefu.
Tabu alisema wameona ni muda muafaka wa kuhakikisha wanaimaliza hali hiyo kwa kufanya oparesheni hiyo.
Hata hivyo, alisema ujio wa Rais huyo pia inaweza kuwa moja ya sababu kati ya nyingi.
“Lakini kikubwa tunataka kuiweka Manispaa yetu katika hali ya usafi na usalama,” alisema Tabu.
Alisema usafi kwa mkoa wa Dar es Salaam ni moja ya mambo ambayo Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki, aliliagiza kwa watendaji wote kulisimamia.
Alisema mkuu huyo wa Mkoa aliagiza oparesheni hiyo ianzie Manispaa ya Ilala,  kata ya Kivukoni.
Akijibu madai ya baadhi ya wananchi waliodai kuwa oparesheni hiyo inatokana na ujio wa Rais Obama, Tabu alisema si kweli.
Bali alitoa wito kwa wafanya biashara hao kutambua kuwa licha ya kutafuta riziki, wanatakiwa kufanya biashara kwa kufuata utaratibu.
Akizungumzia baadhi ya watu wanaofanya kazi ya kusafisha viatu, alisema wamekuwa na tabia ya kufanya zaidi ya kazi hiyo.
Alisema wapo ambao huuza pombe na biashara nyingine haramu. Alitoa wito kwa wakazi wa jiji hilo badala ya kutoa visingizio.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru