Wednesday 14 August 2013

Nape: Madiwani Bukoba bado halali


NA SELINA WILSON
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema bado kinawatambua madiwani wanane wa Manispaa ya Bukoba, waliotangazwa kuvuliwa uanachama.
Kwa mujibu wa Chama, uamuzi wa kuwavua uanachama hauna baraka za vikao vya ngazi ya juu vya CCM.

Chama kimewataka madiwani hao waendelee kufanya kazi na kwamba, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, itakutana Agosti 23, mwaka huu, mjini Dodoma, kujadili suala hilo na mambo mengine.
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera, kutangaza kuwavua uanachama madiwani hao.
Madiwani waliovuliwa uanachama ni Yusuph Ngaiza wa kata ya Kashai, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba, na Samwel Ruangisa wa kata ya Kitendagulo, aliyewahi kuwa meya na mkuu wa kwanza wa mkoa wa Kagera.
Wengine ni Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Deusdedith Mutakyawa (Nyanga), Richard Gaspal (Miembeni), Naibu Meya Alexander Ngalinda (Buhembe),  Dauda Kalumuna (Ijuganyondo) na Robert Katunzi (Hamugembe).
Nape alisema kwa mujibu wa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM walio kwenye vyombo vya dola, hususan wabunge na madiwani, uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Mkoa si wa mwisho.
“Uamuzi huo unapaswa kupata baraka za Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, ndipo utekelezwe, na hilo ni kwa mujibu wa Mwongozo wa CCM ulitolewa Juni 22, mwaka 2010,” alisema.
Alisema mwongozo huo umeelekeza uamuzi wowote wa adhabu unaogusa viongozi wa CCM wenye madaraka kwenye serikali, wakiwemo wabunge na madiwani ni lazima upitishwe na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama.
Nape alisema madiwani waliosimamishwa bado ni halali wa CCM, na wanapaswa kuendelea na kazi kama kawaida wakisubiri kikao cha Kamati Kuu.
Aliwataka wananchi wa Manispaa ya Bukoba na kata husika, wanachama na viongozi wa CCM kuwa watulivu katika kipindi ambacho suala hilo linashughulikiwa na vikao vya kitaifa.
Kwa mujibu wa Nape, wamepokea barua za madiwani hao za kukata rufani kupinga uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Mkoa kwa msingi wa madai ya kukiukwa utaratibu katika kufikia uamuzi huo.
Madiwani hao walikata rufani kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kupinga uamuzi huo, muda mfupi baada ya kutangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera, Avelin Mushi.
Katika barua ya rufani, ambayo Uhuru ina nakala yake, madiwani hao wanasema wanapinga kuvuliwa uanachama na kuondolewa nyadhifa zao kwa kuwa utaratibu haukufuatwa.
“Sisi madiwani wanane wa CCM kwa pamoja tunapinga uamuzi uliofikiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya mkoa kwa sababu kanuni, utaratibu na katiba ya Chama  havikufuatwa.
“Kwa hali hiyo, tunaleta malalamiko yetu mbele yako ili uliangalie suala hilo kwa umakini kwa maslahi ya Chama chetu, serikali, wanachama na wananchi waliotupa dhamana ya nafasi hizi,” ilieleza barua hiyo iliyowasilishwa kwa Kinana.
Juzi Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Kagera, katika kikao kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Chama mkoani humo, Costancia Buhiye, kilipitisha uamuzi wa kuwafutia dhamana ya uanachama na kuwaondolea nyadhifa zao madiwani hao.
Kwa mujibu wa Mushi, hatua hiyo ilitokana na kupuuza ushauri uliotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Mushi, alisema uamuzi huo unatokana na Chama kujali maslahi ya wananchi, tofauti na ya watu binafsi na kwamba, ulitokana na mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa  hiyo, Dk. Anatoli Amani.
Rais Kikwete akiwa ziarani mkoani Kagera hivi karibuni, alitoa agizo kwa wana-CCM hao kutoendelea na mgogoro huo. Mushi alisema vikao vya Chama vimekuwa vikifanyika kwa kufuata kanuni na utaratibu.
Hata hivyo, alisema licha ya kuitwa kwenye vikao hivyo, wanachama hao wamekuwa wakikaidi, na  wakionywa kuhusu kuihujumu serikali ya CCM kwa kushirikiana na madiwani wa kambi ya upinzani kwa kutotekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi.
Katika mgogoro ndani ya manispaa, Kagasheki anapinga ujenzi wa soko jipya mjini Bukoba akidai haukufuata uamuzi wa vikao vya baraza la madiwani wakati Dk. Amani akisisitiza ujenzi umepitishwa na vikao vya baraza.
Mgogoro huo uliibuka baada ya uongozi wa manispaa kutangaza utekelezaji wa miradi mbalimbali, ukiwemo wa ujenzi wa soko jipya na la kisasa na upimaji wa viwanja 5,000.
Uamuzi huo wa kutimuliwa kwa madiwani wanane ulipokelewa kwa hisia tofauti na wananchi wa manispaa hiyo wakiwemo wanachama wa CCM ambao baadhi yao waliungana  na madiwani hao kusikitikia uamuzi huo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru