Wednesday 21 August 2013

Wabunge waibua madudu Ardhi


NA KHADIJA MUSSA
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali imegundua madudu katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambapo viwanja 7,800 nchini havina wamiliki.
Kati ya viwanja hivyo, 160 vyenye thamani ya sh. milioni 500 viko Dar es Salaam.
Kutokana na hilo, kamati hiyo imemuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu katika wizara hiyo ili kujua undani wa viwanja hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, katika ofisi ndogo za Bunge, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe, alisema viwanja hivyo wamiliki wake hawajulikani licha ya kuweko katika orodha ya wizara.
Zitto alisema sababu nyingine ya kuomba ukaguzi maalumu ni kutofikiwa malengo yaliyowekwa na serikali ya kukusanya sh. bilioni 99 katika bajeti ya mwaka 2012/2013, ambapo zilikusanywa sh. bilioni 20 tu.
“Baada ya wizara kuona imeshindwa kufikia malengo katika ukusanyaji fedha, iliamua kuongeza kodi na bei ya viwanja jambo ambalo liliwaongezea wananchi mzigo,” alisema.
Kutokana na hilo, alisema kamati imeiagiza wizara kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kuanzisha mfumo wa kidijitali utakaowezesha hati zote kutolewa kama zilivyo leseni za udereva.
Zitto alisema kamati ina imani kupitia mfumo huo, ambao kila mmiliki atatambulika kupitia namba ya mlipakodi utawezesha kuondoa migogoro ya ardhi iliyoko sasa, ikiwemo ya hati tatu kutolewa kwa kiwanja kimoja.
Katika hatua nyingine, kamati imetaka maelezo kutoka Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, kutokana na kutotumika mfumo wa kielektroniki wa utoaji wa risiti za malipo yanayotokana na makosa ya madereva wa magari.
Imekiagiza kikosi hicho kuwasilisha taarifa mbele ya kikao cha kamati kitakachofanyika Septemba 10, mwaka huu, mjini Dodoma.
Zitto alisema muda umepita tangu mfumo huo uanzishwe na vifaa vya utekelezaji wa kazi kununuliwa na serikali, lakini askari wa kikosi hicho wanatumia mfumo wa kizamani kutoa stakabadhi.
Alisema kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kama mfumo huo ungetumika ungeiwezesha serikali kuingiza sh. bilioni 55, tofauti na ilivyo sasa ambapo wanakusanya sh. bilioni 15 kwa mwaka.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru