Tuesday 20 August 2013

Warioba: Hatuhitaji malumbano


Na Hamis Shimye
MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, amesema tume haiko katika malumbano na wanasiasa dhidi ya Rasimu ya Katiba.
Amesema tume iko kwa ajili ya kupata muafaka wa mambo yanayotakiwa yawemo ndani ya katiba mpya.

Jaji Warioba amesema anashangazwa na mikutano ya hadhara inayofanywa na baadhi ya vyama vya siasa, ikidaiwa kuwa ni mabaraza ya katiba, kwa kuwa huu si muda wa kupokea maoni yao.
Alisema hayo jana, alipofungua mkutano wa kitaifa wa baraza la katiba la tasnia ya habari ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Katika mkutano huo, Jaji Warioba alikuwa mgeni rasmi. Aliwataka waandishi wa habari kuijadili kwa umakini na kupendekeza mambo mazuri kwa maslahi ya wananchi.
Alisema waandishi wanapochangia katika rasimu hiyo, wajadili mambo muhimu kuhusu taifa, kwa kuwa kutasaidia kupatikana rasimu bora ya habari itakayolinda maslahi ya taifa.
“Hatupokei maoni, muda wa kupokea maoni ulishakwisha na tume kufanya kazi ya kuchambua maoni hayo, sasa tuna rasimu na kinachotakiwa ni kuijadili kwa kujenga muafaka na si malumbano,’’ alisema.
Alisema waandishi wanapaswa kuchangia kwa umakini ili kusaidia kupatikana katiba bora, kwa kuwa hiyo ndiyo fursa yao na wasingoje kulalamika baadaye.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, rasimu ina mambo mengi ya kujadiliwa, kama vile ardhi, elimu na uchumi, ambayo yanamgusa moja kwa moja mwananchi wa kipato cha chini, ambaye katiba mpya itakuwa mkombozi wake.
Alisema katiba ni jambo la msingi na si la mifarakano, kwa kuwa jamii yote inataka katiba mpya, hivyo waache watu wasikilizwe ili kupatikana kwa mawazo ya pamoja.
Mwenyekiti huyo alisema vyombo vya habari vinapaswa kuwa makini na kuhakikisha habari zinalenga kuielimisha jamii kuhusu rasimu iliyopo na kuachana na habari za kujadili sehemu ndogo ya mgawanyo wa madaraka.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru