Tuesday 20 August 2013

Jalini kinga badala ya tiba –Dk. Sheni


Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imetoa wito kwa wataalamu wa afya kutoka China, kuangalia kwa kina suala la kinga ya maradhi badala ya tiba wanapokuwa nchini.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni, alitoa rai hiyo alipozungumza na timu ya wataalamu 25 wa afya kutoka Jamhuri ya Watu wa China, waliomtembelea Ikulu, juzi.
Wataalamu hao, wakiwemo madaktari bingwa waliwasili nchini Juni, mwaka huu, na wanatarajiwa kukaa nchini kwa miaka miwili. Wanatoka jimbo la Jiangsu na wamekuwa wanakwenda Zanzibar kufanya kazi tangu mwaka 1964.
“Msijishughulishe tu kutoa huduma za tiba, badala yake muangalie pia suala la kinga ambalo ni muhimu katika kuimarisha afya za wananchi,” alisema.
Dk. Sheni alivitaka vyombo vya habari, vikiwemo vya serikali kuelimisha jamii kuhusu kinga ya maradhi.
Alisema wataalamu hao wana umuhimu wa kipekee, kwa kuwa licha ya kutoa tiba pia wanatekeleza mipango maalumu ya kusimamia ujenzi wa kituo cha uchunguzi wa maradhi ya njia ya chakula katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, Unguja.
Pia ujenzi wa kituo cha kuhudumia wagonjwa waliopata ajali katika hospitali ya Abdalla Mzee Pemba.
“Vituo hivyo ni vipaumbele kwetu kwa kuwa vitapunguza gharama kwa serikali ya kuwapeleka wagonjwa nje ya Zanzibar kwa matibabu, wakati mwingine hata kwa uchunguzi,” alisema.
Dk. Sheni alisema hivi sasa wagonjwa wengi wenye matatizo ya njia ya chakula hulazimika kupelekwa Dar es Salaam au hata nje ya nchi, hivyo kukamilika kwa kituo hicho kutakuwa faraja kwa serikali na wananchi.
Kuhusu kituo cha watu wanaopata ajali cha Pemba, alisema ni muhimu kwa kuwa zimekuwepo ajali nyingi, hususan wakati wa msimu wa uchumaji karafuu.
Dk. Sheni aliwahakikishia wataalamu hao kuwa serikali itafanya kila jitihada ili kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi.
Kwa upande wao, wataalamu hao walisema wamejizatiti katika kuwahudumia wananchi ili kutoa mchango wao ipasavyo katika kuimarisha afya nchini.
Kiongozi wa wataalamu hao, Dk. Lui Ya Ping, alisema watafanya kazi kwa bidii ili kutimiza wajibu wao.
Alisema mpango kazi wao umewasilishwa kwa Wizara ya Afya, hospitali na kwa viongozi wao walioko China.
Dk. Lui alisema ujumbe kutoka Idara ya Afya ya Jimbo la Jiangsu utawasili nchini Novemba, mwaka huu, kuangalia utekelezaji wa ujenzi wa vituo vilivyoelezwa katika mpango huo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru