Friday 9 August 2013

Atakayefukuzwa kupoteza ubunge


SUALA la wabunge wanaotimuliwa na vyama vyao limechukua nafasi kubwa katika mjadala wa Rasimu ya Katiba Mpya, mjini Kibaha, huku wengi wakipendekeza wabunge hao wapoteze ubunge.
Wakichangia ibara ya 123 ya rasimu hiyo, wajumbe wa Baraza la Katiba la Halmashauri ya Mji wa Kibaha, walisema mbunge aliyedhaminiwa na chama akifukuzwa na kuvuliwa uanachama, ubunge wake nao unapaswa kukoma.
Mjumbe kutoka kata ya Kongowe, Slom Bagumesh, alisema hatua hiyo itasaidia kujenga nidhamu kwa wabunge wanaotokana na vyama, lakini wakiendelea na ubunge haitakuwa sawa.
“Hivi mtu aliyepeperusha bendera ya chama fulani, anakwenda bungeni badala ya kutetea wananchi anakitukana chama kilichompeleka pale, akifukuzwa hakuna sababu ya kubaki na ubunge,” alisema.
Mjumbe mwingine kutoka kata ya Tumbi, Rajabu Makala, alisema kifungu cha pili cha ibara ya 123, kinapaswa kuboreshwa badala ya kubaki na ubunge, kitamke atakuwa amepoteza ubunge, mbunge atakayefukuzwa na chama chake.
Alisema wabunge wanaotokana na vyama wanapaswa kuheshimu katiba na kanuni za vyama vyao, na endapo akizivunja na akifukuzwa na kuvuliwa uanachama apoteze ubunge.
“Tunasema huyo abaki na ubunge atakuwa anamwakilisha nani, kama waliompeleka wamemtimua inabidi ufanyike uchaguzi mdogo,” alisema.
Mjumbe mwingine alisema kifungu cha tatu cha ibara hiyo, ambacho kinatamka mbunge akijiondoa mwenyewe kwenye chama, atapoteza sifa ya kuwa mbunge, kiondolewe na kibaki kifungu cha pili.
Wajumbe wengine walitaka katiba ieleze endapo ataondolewa kwa mizengwe aweze kwenda kupinga mahakamani.
Hata hivyo, mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema kifungu hicho kiliwekwa kutokana na maoni ya wananchi kwamba, ili kukwepa gharama za uchaguzi mdogo, pasiwe na uchaguzi wa mara kwa mara.
Alisema kama maoni ya kutaka uchaguzi mdogo urejeshwe yatajitokeza, tume itachukua maoni ya wengi.
Wajumbe wengine waliunga mkono rasimu hiyo kwamba, endapo mbunge atakoma ubunge kutokana na kifo au sababu yoyote, chama chake kiteue mtu aliyefuata katika orodha ya kura za ndani ya chama isipokuwa kwa mbunge huru uchaguzi ufanyike.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru