Tuesday 20 August 2013

UDSM kutoa Shahada ya Sayansi ya Hali ya Hewa


NA RACHEL KYALA
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), imefanikisha kuanzisha kozi ya Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Hali ya Hewa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agness Kijazi, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam.
Dk. Agness alisema mchango wa TMA katika kufanikisha uanzishwaji wa shahada hiyo ni kushiriki katika uandaaji wa mitaala ya kufundishia na kutoa wataalamu wa kufundisha kozi mbalimbali chuoni hapo.
Alisema mamlaka itatoa nafasi ya mafunzo ya vitendo kwa wanachuo, ikiwemo kufanya mazoezi ya kazi kwa mwaka mmoja kwa wahitimu, na kuhakikisha Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), linatambua uanzishwaji wa kozi hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema kuanzishwa kwa mafunzo hayo nchini ni moja ya utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete, na fursa kwa idadi kubwa ya Watanzania, wageni na wafanyakazi wa mamlaka kujiunga na masomo katika taaluma ya hali ya hewa kwa gharama nafuu.
“Kwa upande wa mamlaka, mafunzo hayo yatasaidia kuokoa gharama kubwa ya kati ya sh. milioni 15 na sh. milioni 25 kwa mwaka iliyokuwa ikitumika kusomesha mtaalamu mmoja nje ya nchi, sasa itagharimu sh. milioni moja tu kwa mwaka,” alisema.
Dk. Agness alitoa wito kwa wanafunzi, hususan wa kike kufanya vyema kwenye masomo ya Fizikia na Hesabu ili kukidhi vigezo vya kujiunga na masomo hayo.
Alisema hivi sasa mamlaka ina idadi ndogo ya wafanyakazi wanawake, ambao ni 125  ikilinganishwa na wanaume 449.
Wakati huo huo, alisema TMA imepanua wigo wa ushirikiano na vyombo vya habari, hususan redio za kijamii ili kutoa taarifa za hali ya hewa kwa wakati, zikiwemo za kila siku, za msimu na za tahadhari ya majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi.
Dk. Agness alisema mamlaka imeboresha viwango vya utoaji  taarifa za hali ya hewa kwa asilimia 80, ambapo imezindua njia kadhaa za usambazaji habari, ikiwemo mitandao ya simu za mkononi kwa makundi maalumu, wakiwemo wakulima na wavuvi.
Naye mtaalamu wa hali ya hewa wa mamlaka hiyo, Ladislaus Chang’a, alisema idadi ya watu wanaotumia utabiri wa hali ya hewa kwenye shughuli mbalimbali, hususan wakulima inaongezeka kila mwaka.
Kutokana na hilo, alisema watapata taarifa kutoka serikali za mitaa, kupitia kwa maofisa ugani, ambao watawashauri namna ya kuzitumia ili kuleta kilimo chenye tija.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru