Friday 9 August 2013

Watalii wamwagiwa tindikali Zanzibar




Na waandishi wetu
WATALII wawili raia wa Uingereza, wamejeruhiwa baada ya watu wasiojulikana kuwamwagia tindikali wakiwa matembezini eneo la Shangani, mjini Unguja, Zanzibar.
Habari za kuaminika zinasema watalii hao walikuwa wanakwenda kula katika hoteli ya Pagoda, na walipatwa na mkasa huo saa moja usiku.
Tukio hilo ni mwendelezo wa matukio kadhaa ya watu kumwagiwa tindikali, wakiwemo viongozi wa dini na wafanyabiashara.
Watalii hao, Katie Gee na Kristie Trup, wana umri wa miaka 18, ambao ni walimu wa kujitolea katika Kituo Maalumu cha Sober House, kinachowasaidia waathirika wa dawa za kulevya.
Katie na Kristie waliwasili Zanzibar wiki mbili zilizopita kupitia Shirika lisilo la Kiserikali la Art In Tanzania.
Rais Jakaya Kikwete,  amewatembelea watalii hao katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam, ambako walipelekwa baada ya tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamishna wa Jeshi la Polisi Mussa Ali Mussa, alisema wameanza uchunguzi ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa.
“Tumeanza uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwahoji watu mbalimbali, wakiwemo wanaotembeza watalii Zanzibar,’’ alisema.
Alisema ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote, yakiwemo ya Mji Mkongwe, hususan wakati huu, ambao waumini wa dini ya Kiislamu wanasherehekea sikukuu ya Idd el Fitri.
Kamishna Mussa alisema wamefungua vituo vidogo vya polisi kwenye maeneo yote yatakayokuwa na mikusanyiko na askari wameongezwa kulinda usalama mitaani.

CCM YAONYA, YALAANI
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimelaani tukio hilo, ambalo kimesema imepokea taarifa zake kwa masikitiko.
Imesema walimu hao walikuwa msaada mkubwa kwa taifa, kutokana na kujitolea kufundisha Shule ya Mtakatifu Monica, katika Kanisa la Anglikana, Zanzibar.
Taarifa ya Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Itikadi na Uenezi, Zanzibar, Waride Bakari Jabu, alisema unyama huo kamwe haupaswi kufumbiwa macho, kwani ni kinyume cha haki za binadamu.
“CCM inalaani unyama huu na vitendo vya watu kumwagiwa tindikali, tunavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina, kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wote,’’ alisema.
Waride, katika taarifa kwa vyombo vya habari jana, alisema mfululizo wa matukio ya watu kumwagiwa tindikali ni jambo la hatari.

SANYA: NI UNYAMA
Mbunge wa Mji Mkongwe, Muhammad Ibrahimu Sanya, alisema tukio hilo ni la kinyama na halipaswi kufumbiwa macho.
Ameliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha linakuwa makini na watu wanaoendesha unyama huo, na kuchukua hatua kwa wakati stahili.
“Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi haraka na lihakikishe waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria. Ni tukio la kijinga na la kinyama, binadamu hawezi kufanya hivi kwa mwenzake,” alisema.
Sanya alisema hilo ni tukio la utovu wa nidhamu na kwamba, matukio ya aina hiyo hayapaswi kufumbiwa macho, kwani yanalipaka tope taifa.
HOFU YATANDA
Tukio hilo limeanza kuwatisha wadau wa utalii, wakihofia kupungua kwa watalii.
Ofisa wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, ambaye hakupenda kuandikwa jina gazetini, alisema tukio hilo linaweza kuzorotesha maendeleo, hususan katika sekta ya utalii.
Alisema linaweza pia kuwatisha raia wa Uingereza, ambao wanaweza kusitisha kutembelea Zanzibar.
Zanzibar hupokea watalii wengi kutoka nchi za Ulaya, ikiwemo Uingereza na Italia.
Tukio hilo ni la tatu katika kipindi cha miezi mitatu, ambapo Mei 23, mwaka huu, Sheha wa Shehia ya Tomondo, Zanzibar, Mohammed Omar Said, alimwagiwa tindikali na watu wasiofahamika.
Julai 14, mwaka huu, Sheikh wa Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, Said Makamba, alimwagiwa tindikali.
Mmoja wa wamiliki wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad, alimwagiwa tindikali Julai 19, mwaka huu, eneo la Msasani, Dar es Salaam.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru