Wednesday 16 April 2014

Seif: Hakuna anayetaka Muungano uvunjike


WILLIAM SHECHAMBO NA MUSSA YUSUPH
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad amewataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutopuuzia mawazo ya makundi yaliyopo katika bunge hilo kuhusu mfumo wa Serikali utakaofaa kuwemo kwenye katiba mpya.


Alisema mawazo ya muundo upi wa Serikali utakaofaa kuwepo kwenye katiba hiyo ni lazima ulenge katika kuimarisha Muungano uliopo baina ya Tanyanyika na Zanzibar.
Makamu huyo wa kwanza wa Rais alisema ni lazima wajumbe wafahamu kuwa, hakuna Mtanzania anayependa Muungano uliopo uvunjike baada ya kudumu kwa takribani miaka 50 ya mafanikio na kwamba rasimu ya pili ya katiba imethibitisha hilo kwa kuonyesha kuna idadi ndogo ya watu wasiopenda kabisa kuwepo kwa Muungano.
Maalim Seif alisema hayo jana alipokuwa akifungua Maonyesho ya Miaka 50 ya Muungano kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja,
Dar es Salaam jana, ambayo yamehusisha taasisi na idara za serikali zinazohusika na mambo ya Muungano.
Alisema ni vizuri kuepuka maamuzi yatakayovunja Muungano.
Maalim Seif alisema pia kuwa, ili kupata katiba bora, wajumbe wa bunge hilo wanapaswa kusikilizana kila mmoja na hoja yake, ambayo inatetea muundo wa serikali anayotaka na kisha kuichuja kwa kuzingatia maslahi ya Muungano kwa kuwa kuwepo kwa fikra tofauti katika eneo fulani ndio chanzo cha maendeleo.
Makamu wa Kwanza wa Rais alitumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi kufuatilia kwa ukaribu mijadala inayoendelea Bungeni na kuhakikisha wanatumia nafasi yao muhimu ya kupiga kura ya kupitisha katiba kwa kusimamia uwepo wa Muungano na si vinginevyo.
“Watanzania tunapaswa kuhakikisha tunaulinda na kuudumisha Muungano kwenye katiba ijayo kwa kupiga kura baada ya kutathmini mafanikio yake tuliyoyapata tangu mwaka 1964 mpaka sasa,” alisema.
Alisema hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia kuwepo kwa mchakato wa katiba mpya, ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, ni busara iliyojaa nia ya kizalendo, kwa kuwa alitoa nafasi ya kutathmini mustakabali wa Taifa kwa kipindi cha miaka 50 mingine ijayo ya Muungano.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru