Tuesday 1 April 2014

Ujangili wapungua kwa asilimia 58

  •  Sarakikya: Tutaendelea kuwabana majangili
NA LILIAN JOEL, ARUSHA

VITENDO vya ujangili vimepungua kwa asilimia 58, lakini idadi ya meno ya tembo yanayokamatwa imeongezeka kutokana na kukamatwa meno yaliyowindwa siku zilizopita.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, Paul Sarakikya, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya ujangili katika kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu.
Sarakikya alisema katika kipindi cha hicho, siku za doria zilikuwa 30,372 na zilifanyika katika Mapori ya Akiba, Hifadhi zote za Taifa, Mapori Tengefu pamoja na Mamlaka ya Ngorongoro.
Alisema katika kipindi husika, mizoga ya tembo 39 ilipatikana ndani na nje ya hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema meno ya tembo wazima 171 na vipande 22 vya meno ya tembo vilikamatwa. Alisema meno 302 ya tembo pia yalikamatwa yakiwa yameshachakatwa.  
“Jumla ya meno yote yaliyokamatwa yalikuwa na kilo 662.62, ambapo mengine yalikuwa yameshaanza kuchakaa kutokana na majangili kuyafukia aridhini kwa muda mrefu wakati wakitafuta soko,” alisema.
Aidha, ng’ombe 2,663  na misumeno na mbao 745 vilikamatwa na kuongeza kuwa, kesi 124 zenye watuhumiwa 544 waliojihusisha na vitendo vya ujangili, zilifunguliwa kwenye mahakama mbalimbali nchini.
Kaimu Mkurugenzi alisema kesi 38 kati ya hizo zenye watuhumiwa 113, zinaendelea na zingine 62 zenye jumla ya watuhumiwa 85 ziliishia kwa watuhumiwa kulipa faini ya sh. milioni 25.5.
Alisema katika kipindi cha doria ya miezi hiyo, idara hiyo iliweza kukamata kilo 1,111 za wanyama mbalimbali zikiwemo silaha nzito zinazotumika kuwinda wanyama.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru