Wednesday 23 April 2014

Hamad awafyatukia Maalim Seif, Lipumba



  • Awaita wasaliti wakubwa wa Watanzania
  • Afichua michezo michafu ya CUF bungeni
  • Kigwangala aeleza hatma ya Tanganyika
  • UKAWA wawakera Wazanzibar, walaani

NA THEODOS MGOMBA, DODODMA
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Hamad Rashid Mohamed juzi alimshukia Makamu wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad huku akimtuhumu ni kiongozi msaliti kwa Watanzania.

Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alielezwa kuwa ni kiongozi kigeugeu kwani sasa amegeuka na kutaka serikali ya Muungano wa mkataba wakati awali alikuwa muumini mkubwa wa serikali mbili.
“Tuwe macho na viongozi wanaobadilika badilika kama kinyonga kwani, mwaka 1992,  CUF walikuwa na msimamo wa  serikali tatu, juzi serikali ya mkataba, kila siku anabadilika,  ni kiongozi wa aina gani huyu?’’Alihoji.
Kwa mujibu wa Hamad, katika kipindi cha kudai katiba mpya,  CUF na vyama vingine viliandamana na kuleta machafuko Zanzibar.
“Watu waliingia katika maandamano na  kusababishiwa ulemavu na  wajane, na hata sehemu zingine  wanafunzi walikosa masomo na leo badala ya kuhakikisha katiba inapatikana, wanahatarisha amani na kutaka mapinduzi tena,”alisema.
“Hivi kati yangu na yeye, msaliti ni nani kwani wakati wakiwa wanatafuta serikali ya umoja wa kitaifa, walikutana sehemu mbalimbali ikiwemo Dodoma na kuafikiana namna ya kufanya serikali hiyo.

“Lakini nilishangaa wenzake watano, akiwemo Maalim Seif, walijifungia ndani, wakaja na masuala ya mkataba, kama ni usaliti, nani msaliti wa wenzake?’’ Alihoji Hamad.
Alisema walipokwenda kwenye kikao cha Halmashauri Kuu, ikapendekezwa Mwinyi (Rais Ali Hassan) agombee Urais na kwa vyovyote Maalim Seif awe Waziri Mkuu.
Huku akishangiliwa na wajumbe, Hamad alisema waliwahi kwenda kwa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1992 wakiwa saba, na aliwaambia kama kuna makosa amefanya ni kuitambua Biafra na kuwatambua wao, na aliwaagiza wahakikishe kuwa Muungano unabaki hai.
“Tushukuru tunaye Rais mstaarabu, mvumulivu, watu wanampa shinikizo siku saba, lakini anacheka tu, kwa wenzetu hili halitokei, utakuwa jela,” alisema  Hamad.


Akisisitiza zaidi, alisema Bunge linapaswa kufanya uamuzi kwamba ni theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na kutoka Zanzibar wakutane ili kuweza kupata katiba.
“Theluthi mbili pande zote tukae tutafute katiba, lakini inashangaza  leo, katiba inapatikana, hutaki, tukae tuhakikishe katiba inapatikana,” alisistiza Hamad.
“Hakuna sababu ya kutoka hapa bila katiba.
Wananchi wanasubiri, hapa hakuna UKAWA wala Upawa,’’ alisema.
Alisema tangu mwaka 1982, amekuwa akiishi 
Tanzania Bara na kwamba uhusiano wake na Bara si wa kawaida, ni wa kindugu wa damu.
“Wanashangaa nyie Watanzania ndio walimu wetu, lakini leo mmepata kichaa gani mnamsema vibaya Nyerere na Karume, kama ingekuwa ni kwetu, mgeipata habari yenu,” alisema.
Alisema kuna watu wanajinadi kuwatetea Wazanzibar kuwa wao ndio Wazanzibar  wa kweli bila wanzanzibar wenyewe kutaka, na kusema ni vyema  Watanzania kuwa macho na watu wa aina hiyo.

Naye Dk. Hamis Kigwangala amesema hakuna sababu kwa Bunge Maalumu la Katiba kuendelea kujadili mambo ya Muungano kwani hayakuwepo kwenye mabadiliko ya tume ya katiba.
Amesema mchakato wa kupata katiba mpya unaoendelea bungeni mjini Dodoma, si wa kuifufua Tanganyika.
Alisema baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wameugeuza mchakato huo na kuufanya kuwa wa kujadili Muungano.
Ameonya kuwa mchakato huo wa katiba si wa kubadilisha muundo wa Muungano na kwamba kuna mambo mengi yanapaswa kujadiliwa.
Dk. Kigwangala alisema hayo jana mjini Dar es Salaam kwenye mdahalo wa utafiti ulioandaliwa na Taasisi ya Twaweza.
Alisema mchakato wa katiba umegeuzwa na kuwa wa kubadili muundo wa Muungano, jambo ambalo halikuwemo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Dk. Kigwangala, ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa CCM, alisema iwapo suala hilo litaendelea, ni vyema likarejeshwa kwa wananchi.
Alisema pamoja na UKAWA kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, mchakato huo utaendelea mpaka mwisho.
“Ni bora UKAWA warejee bungeni tuendelee na mchakato, waonyeshe kutokerwa na lazima wafuate sheria,” alisema na kuongeza:“Muundo wa Muungano si ugali, sio maji na wala sio dawa kwa wananchi.” 
Alisema katika mchakato huo, si rahisi kukwepa makundi yenye mitazamo tofauti na jambo la busara ni kuvumiliana.

Jaji Warioba afunguka tena
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wameacha kuzungumzia maoni ya wananchi, badala yake wanazungumzia suala la serikali tatu.

Alisema kuna mambo ya msingi ndani ya rasimu ya katiba mpya, yanayowahusu wananchi moja kwa moja, lakini hadi sasa hayajazungumzwa.
“Badala ya kujadili mambo muhimu ya wananchi, wameng’ang’ania serikali tatu, kila kundi linaonyesha dhahiri linataka nini ndani ya rasimu ile.
“Waliowengi wanataka wapitishe katiba yao na wachache wanataka kuwakwamisha wengi ili katiba isipite,” alisema.
Alisema iwapo wajumbe wa Bunge Maalumu wataendelea kuvutana, upo uwezekano mkubwa wa kupata katiba, ambayo haitadumu miaka mingi kama iliyopo sasa.

Mtatiro ataka kura ya maoni
Naye mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Julius Mtatiro alisema ni vyema ikapigwa kura ya maoni ili wananchi waamue wanataka serikali ngapi.

Wanzanzibar waijia juu UKAWA
Mwenyekiti wa Umoja wa Wazanzibar waishio Dar es Salaam, Swalehe Omary amesema wameshitushwa na kuhuzunishwa na kitendo cha wabunge wa vyama vya upinzani kutoka NCCR, CUF na Chadema kutoka nje ya Bunge na kususia vikao bila ya sababu maalumu.
Alisema inashangaza kuona wabunge wanaacha kutumia fursa ya kutunga katiba ndani ya bunge,
badala yake wanatoka na kuzurura mitaani na wakiwa wameshilipwa mamilioni ya fedha.
Omary alisema kitendo cha UKAWA kutoka ndani ya Bunge ni usaliti na kwamba, wanakilaani na wanawataka wananchi wasiwaunge mkono.
“Tunaamini kuwa katiba mpya haiwezi kupatikana kwa maandamano na mikutano ya hadhara, tunawataka UKAWA warejee bungeni kuendelea na mchakato, waache visingizio,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru