Tuesday 8 April 2014

Wachimbaji wadogo kumwagiwa mamilioni


NA MWANDISHI WETU

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini ya kukabidhi hundi za ruzuku ya dola za Marekani 500,000 kwa wachimbaji wadogo 11 waliokidhi vigezo.
Hafla ya utoaji wa hundi hizo kwa wachimbaji wadogo itafanyika katika Chuo cha Madini mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Waziri wa Nishati na Madini, Badra Masoud ilisema, waziri wa wizara hiyo, Profesa Sospeter Muhongo ataambatana na Naibu Waziri anayeshughulikia Madini, Stephen Masele.
Wengine ni watendaji kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA), ambao watashuhudia utoaji wa hundi hizo.
Ilisema ruzuku hiyo imetolewa na  Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ulio chini ya wizara hiyo.
Kutolewa kwa hundi hizo ni matokeo ya mkataba, ambao wizara hiyo iliingia na TIB ili benki hiyo iwe wakala wa kutoa mikopo na ruzuku kwa wachimbaji wadogo kwa niaba ya serikali.
Mkataba wa uendelezaji wa wachimbaji wadogo ulioingiwa kati ya TIB na serikali, unasisitiza ruzuku kutolewa kwa wachimbaji wadogo wenye sifa ili kuwawezesha kufanya shughuli zao za uzalishaji mali, wakiwemo wanawake wanaojishughulisha na utoaji huduma katika maeneo ya uchimbaji mdogo.
Wachimbaji wadogo 11 watakabidhiwa hundi hizo za ruzuku baada ya kukidhi vigezo vya kuwa na uzoefu wa uchimbaji mdogo usiupungua miaka tano na kuwa na leseni hai ya uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini pamoja na kuwa na ushahidi wa upatikanaji wa mashapo au mali ghafi inayohitajika kwa ajili ya mradi unaoombewa ruzuku.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru