NA MWANDISHI MAALUMU, ZANZIBAR
WAKUU wa mikoa na wilaya wametakiwa kuisoma mara kwa mara na kuielewa katiba pamoja na sheria nyingine za nchi.
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni, alitoa agizo na kusema wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku, wanapaswa kuzingatia katiba na sheria.
Alitoa agizo hilo jana, alipokuwa akifungua mkutano elekezi kwa wakuu wa mikoa na wilaya za Zanzibar.
Alizitaja baadhi ya sheria ambazo wakuu hao wanapaswa kuzielewa na kuzitekeleza kila siku ni pamoja na Sheria Namba 1 ya Mwaka 1998 ya Tawala za Mikoa, Sheria Namba 3 ya Baraza la Manispaa ya Mwaka 1995 na Sheria Namba 2 ya mwaka 2011 ya Utumishi wa Umma.
Aliwataka pia kuheshimu kiapo cha uaminifu wanachokula kabla ya kukabidhiwa dhamana zao na kuwakumbusha kuwa kiapo hicho ni jukumu walilochukua katika maisha yao duniani na mbinguni.
Dk. Sheni aliwataka wakuu wa mikoa kuelewa kuwa ndio watendaji wakuu katika mikoa yao na kuwakumbusha mabadiliko ya kumi ya katiba ya Zanzibar, ambayo yanaeleza kuwa wakuu wa mikoa na wilaya ni watendaji wa serikali, tofauti na ilivyokuwa kabla ya mabadiliko hayo.
Alisema ni vigumu shughuli za serikali kutekelezwa katika ngazi hizo, bila ya kuwepo kwao, hivyo wanapaswa kuelewa uzito wa majukumu yao katika kuleta maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi katika mikoa na wilaya zao.
Hata hivyo, alibainisha kuwa kazi za mikoa na wilaya si za kuratibu shughuli za serikali kuu pekee, bali mikoa na wilaya inapaswa kuwa na dira na kupanga mipango yake ya maendeleo kwa kuzingatia changamoto, vipaumbele, mazingira na mahitaji ya mkoa na wilaya husika.
Sunday, 26 October 2014
Dk. Sheni: Someni katiba na kuzielewa sheria
07:42
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru