Monday 27 October 2014

Mwandosya: Fedha si kigezo cha Urais


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya, amesema fedha si kigezo cha mtu kuteuliwa kuwania nafasi ya urais na kwamba, imani iliyojenga haina mashiko.
Amesema suala hilo limekuwa likimtatanisha na kueleza kuwa kiongozi huchaguliwa kutokana na uadilifu na uwezo wake na si kigezo cha fedha kama baadhi ya makada walivyojenga imani hiyo.
Profesa Mwandosya, ambaye ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwakani, alisema imani hiyo inakwenda kinyume na matarajio ya wananchi na misingi ambayo vyama vya siasa havikuichagua.
Aliyasema hayo mjini hapa jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Mbeya.
“Fedha ili iweje …kwamba utawanunua wajumbe, utawapa thamani wajumbe, utasema mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa thamani yake ni sh.200,000 wa NEC sh.500,000 na yule wa Kamati Kuu ni sh.milioni moja.
“Hicho ni kiburi na sifahamu makada wenye imani hiyo potofu wanaipata kutoka wapi… halafu inakuwaje baada ya kuteuliwa,” alihoji Profesa Mwandosya.
Alisema kwa mshahara wake tangu alipoteuliwa, posho za safari za ndani na nje ya nchi, kamwe hana uwezo wa kumpa kila mjumbe  sh. 200,000.
”Sasa hizi fedha zingine wenzetu hawa wanazipata wapi na kama wanazikopa, watazirudisha namna gani? Kama wanafanya biashara, watawezaje kuwatumikia wananchi wakati wana mambo yao mengine pembeni,” alisema.
Alisema vitabu vya dini vinasema kamwe mtu hawezi kuwatumikia mabwana wawili, hivyo kuchanganya siasa na mambo mengine ni tatizo na kuwanyima haki wananchi.
Alisema hao wenye uwezo huo kifedha, wamekuwa wanawaona wengine wanaohoji hali hiyo, kuwa wanasiasa za kizamani, lakini kwake ni afadhali kuendelea na siasa za kizamani, kuliko siasa za kumrubuni mwananchi kwa uongozi kupatikana kwa njia ya fedha.
“Fedha ambazo utazirudisha namna gani, zimetoka wapi na kwa sababu gani? Kwa kweli hili ni jambo, ambalo nitaendelea kulizungumza tu, kama Mwenyezi Mungu akinijalia kufika popote pale, nitakuwa kwa sababu nina upendo, nataka kuwatumikia wananchi, lakini si sababu nina fedha,” alisema Mwandosya. 

Urais ni zaidi ya hapo
Katika hatua nyingine, Profesa Mwandosya amesema ndani ya CCM, hawateui mtu kwa ajili ya kuwa rais tu, bali wanamtarajia kuwa Mwenyekiti wa Taifa.
Alisema makada wengi wamekuwa wakilisahau hilo na kwamba, lazima wajiulize mtu wanayemtaka anaweza kudumisha fikra za waasisi, Hayati Julius Nyerere na Amani Karume?
Alisema urais ni mfumo unaoendana na dhamana na heshima na jukumu kubwa, hasa ikichukuliwa kuwa kuna utaratibu ndani ya CCM.
Kwa mujibu wa Profesa Mwandosya, kumsaidia mwananchi kimaendeleo,  kwa kupiga hatua ni jukumu kubwa, ambalo analiona linatetemesha, lakini ni lazima mmoja wao aende akaifanye hiyo kazi.
Alisema Mwalimu Nyerere, aliwahi kusema viongozi wazuri na bora hawajitangazi kwa sababu wanaona uzito wa dhamana iliyopo mbele yao.
“Hawajitangazi ila kuna watu wanawajua viongozi wanaofaa kuwaongoza.
“Fulani tunamfahamu anaweza akatutoa hapa, na kutuongoza kupigania kijiji chetu. Kwa mfano ataongoza majeshi yetu kupigana na kijiji kingine na haiwezekani mtu ajitokeze na kusema atafanya kila njia ili achaguliwe,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa hilo ni suala gumu sana ambalo hata ndani ya Chama, ni lazima waanze kufikiria iwapo hii demokrasia waliyonayo (CCM), ifike kiasi ambacho kila mtu kwa sababu ana uhuru, basi anaweza akasema anataka kwenda Magogoni.
Alisema mwakani, taifa litaingia kwenye hatua ya kufanya mabadiliko ya uongozi, ambapo kila chama kina mchakato wake, na CCM nacho kina utaratibu wake.
“Mwakani ndio uchaguzi, lakini dira na maelekezo bado hayajatoka, basi ni dhahiri mwananchi na mwana-CCM ana ruksa ya kugombea nafasi yoyote ikiwemo urais,” alisema Profesa Mwandosya.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru