Friday, 24 October 2014

Mgonjwa wa ebola azua taharuki


NA RODRICK MAKUNDI NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
WANANCHI wa Kata ya Shirimatunda katika Manispaa ya Moshi,  Kilimanjaro, wamepatwa na taharuki kutokana na taarifa za kuwepo  mgonjwa anayedhaniwa kuwa na ebola.
Mgonjwa huyo, ambaye amelazwa katika zahanati iliyoko kwenye kata hiyo, amesababisha huduma kusitishwa na zahanati kufungwa kwa muda huku wagonjwa waliokuwa wakipatiwa matibabu wakihamishiwa katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata.
Habari zaidi zimeeleza kuwa mgonjwa huyo, aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambapo alisafirishwa hadi kwenye zahanati hiyo baada ya kudai kusikia maumivu makali ya kichwa.
Taarifa hizo zilisema mgonjwa huyo (jina halikufahamika), anayedaiwa ni mzaliwa wa Marangu wilayani Moshi, mwenye makazi yake Dar es Salaam, ameendelea kutibiwa hospitalini hapo na wataalamu wa afya walioko katika zahanati hiyo.
Tayari wataalamu wamechukua sampuli kutoka kwa mgonjwa huyo kwa ajili ya vipimo ili kujiridhisha huku huduma zingine za matibabu zikiendelea kutolewa kwa mgonjwa huyo anayedaiwa kusafiri kutoka nchini Senegal.
Hata hivyo, waandishi wa habari waliofika eneo la tukio walishuhudia watoa huduma za afya katika zahanati hiyo, wakiingia na kutoka ndani ya jengo alikolazwa mgonjwa huyo, ingawa baadhi yao hawakuwa na mavazi rasmi ya kujikinga.
Jopo la wataalamu wa afya likiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Mtumwa Mwako, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Moshi, Dk. Christopher Mtamakaya, na watendaji wengine akiwemo Mkurugenzi wa Manispaa, Shaban Mtarambe, walikutana kwa dharura katika zahanati hiyo.
Mtarambe alipoulizwa kuhusu hali hiyo, alisema hawezi kuzungumza kwa maelezo kuwa suala hilo ni la kitaalamu zaidi linalohitaji wataalamu husika kulizungumzia.
Jitihada za kumpata Dk. Mwako, kutolea ufafanuzi suala hilo hazikuzaa matunda.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigongoni, Juma Sambeke, alithibitisha kuwepo kwa mgonjwa huyo baada ya kupokea taarifa kutoka viongozi wa wenzake.
Alisema licha ya mgonjwa kufikishwa kwenye zahanati hiyo, uongozi wa kijiji haukuwa na taarifa huku akipokea majibu kutoka ngazi ya manispaa kuwa suala hilo linaratibiwa na mkoa.
Diwani wa Kata ya Shirimatunda, Felix Mushi, alilaumu uongozi wa manispaa kwa uamuzi wake wa kutenga eneo hilo kwa ajili ya wagonjwa wanaohisiwa kuwa na ebola.
Alisema eneo hilo limezungukwa na huduma zote za kijamii, ambapo baadhi ya wazazi wamekuwa na shaka na kuwazuia watoto wao kwenda shuleni.
Zahanati hiyo inakadiriwa kutoa huduma kwa zaidi ya wagonjwa 5,000 kwa mwezi, ambapo takribani wagonjwa 100 walihamishiwa katika ofisi za Ofisa Mtendaji Kata, wakiwemo wale wanaofika kwa ajili ya chanjo ya surua na rubella.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru