NA MARIAM MZIWANDA
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuwasilisha mikataba yote ya gesi ambayo haijafanyiwa ukaguzi.
Pia imeagiza kuwasilishwa kwa taarifa za mapitio ya mikataba hiyo kesho kwa Katibu wa Bunge baada ya saa za kazi ili ifanyiwe ukaguzi kubaini utekelezaji wa miradi.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema hayo jana wakati wajumbe wa kamati hiyo walipokutana na uongozi wa TPDC.
Alisema TPDC lazima iwasilishe mikataba yake isiyokaguliwa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo ni 19 na kuondoa saba iliyokaguliwa kati ya 26 ya gesi iliyopo.
Alisema shirika hilo limekuwa likipiga chenga kuwasilisha mikataba ya gesi na mapitio yake hivyo, kukiuka sheria katika kuiwezesha kamati kutekeleza kazi yake.
“Tunaiagiza TPDC kesho wawasilishe mikataba ya gesi na watapangiwa siku ya kuja ili ijadiliwe na kukaguliwa kwa kina. Kamati ndiyo wananchi hivyo inafanya kazi kisheria. Kuinyima taarifa za mikataba ni kuvunja sheria,“ alisema.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Katibu wa Kamati PAC, Eric Maseke, alisema sheria mama inayotoa mamlaka kwa kamati za Bunge inaelekeza ofisi yeyote ya umma kupitia kwa maofisa wake wanapotakiwa kutoa nyaraka za serikali.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Michael Mwanda, aliomba radhi kwa kamati hiyo kutokana na kutokea kutofautiana kati ya uongozi wake na kamati hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, James Andilile, aliieleza kamati hiyo kuwa iwapo wanahitaji nyaraka za mikataba wawasiliane na Wizara ya Nishati na Madini kwa kuwa imewasilishwa huko.
Monday, 27 October 2014
PAC yataka mikataba ya gesi
08:48
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru