NA MWANDISHI WETU, BEIJING
“NINGEPENDA Rais ajaye baada yangu awe bora kuliko mimi.” Ni kauli ya Rais Jakaya Kikwete kwa mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao nchini.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi mjini hapa, alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na wawakilishi hao wa Afrika na kuwaeleza hali ilivyo Afrika kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kilichomsukuma Rais kuzungumzia mustakabali huo wa uongozi wa taifa, ni swali aliloulizwa na mwakilishi wa Nigeria, Sola Onadije, ambaye mbali na kuupongeza utaratibu wa uongozi wa Tanzania, alitaka kujua kama ana wazo la kuongeza muda wa kuendelea kuwa madarakani.
“Kipindi changu cha pili cha uongozi kinamalizika mwakani. Nafarijika kusema nitastaafu nikiwa nimeridhika kabisa na nikijivunia pia juhudi zangu chanya nilizozifanya wakati wa uongozi wangu,” alisema.
Aliwataka wawakilishi hao wa Afrika kuondoa mawazoni uwezekano wa yeye kuwania madaraka wakati muhula wake utakapomalizika na kusema atajisikia furaha sana atakapokuwa anakabidhi ‘kijiti’ kwa Rais ajaye.
“Urais ni kazi ngumu. Nawashangaa wenye misuli ya kuendelea nao kwa kipindi kirefu,” alisema na kuongeza kuwa kuna uzuri wa kuwa na ukomo wa madaraka.
Alisema ukomo huo unatoa fursa kwa nchi kupata kiongozi mpya, mwenye mawazo mapya na njia mpya za kufikiria kusukuma mbele ajenda za kitaifa.
“Wakati kipindi changu kitakapomalizika, nitapenda kubaki shambani nikilima na kumwachia mwingine aendeleze kazi tuliyokwishaianza. Natamani ajaye awe bora kuliko mimi,” alisema.
Naibu Kiongozi wa Mabalozi hao anayetoka Mauritius, Paul Chong Leung, aliupongeza uongozi wa JK na mchango wake katika kuleta amani na utulivu Tanznia na Afrika kwa jumla na kutolea mfano wa juhudi za hivi karibuni za upatanishi wa mahasimu wa Sudan Kusini.
Friday, 24 October 2014
JK azungumzia Rais ajaye
01:03
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru