Na Cecilia Jeremiah
WAZAZI na walezi wametakiwa kuacha kuwaozesha watoto wao kwa tamaa za fedha mara wanapomaliza masomo yao.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa, wakati akiwahutubia wazazi na wanafunzi wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mtanga.
Alisema si sahihi kwa wazazi kupokea fedha na kuwaoza watoto wao, kwani kufanya hivyo ni kukatisha malengo yao.
Mbunge huyo alisema mbali na kuwaozesha wakiwa wamemaliza masomo yao, pia kuna wengine ambao wamekuwa wakifanya hivyo hata kwa wanafunzi wanaofeli mitihani yao.
“ Kuna baadhi ya wazazi, mtoto akifeli ndio tiketi ya kumwozesha, hapana… huyu ana uwezo wa kuendelea na masomo ya ziada na baadaye kufanya vizuri pia,” alisema.
Alisema hivi sasa hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa kike inajengwa ili kuwasaidia wale wanaokaa mbali na shule kutopata shida.
Marombwa alibainisha wengi, wengi waliobainika kuwa na mimba walikuwa wakidanganywa njiani na wengine kutofika shule.
Hata hivyo alisema, jitihada zinafanywa kufikisha maji katika hosteli hiyo ili wanafunzi waanze kuitumia.
Aliahidi kulipa ada ya mhula wa kwanza kwa wanafunzi wote wanakaochaguliwa kwenda kidato cha tano shuleni hapo.
“Idadi ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne ni 18, wasichana wanne wavulana 14, hawakufika idadi ya kupewa kituo cha mtihani hapa Mtanga hivyo wataenda kufanya mitihani yao Muhoro, hawa nitawalipia gharama za malazi,” alisema.
Mkuu wa Shule ya Mtanga, Gynogret Nwakyambiki, alisema shule yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya kutokuwa na maabara.
Sunday, 26 October 2014
Msiwaozeshe mabinti wadogo-Marombwa
07:41
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru