Monday, 27 October 2014

Vigogo wa dawa za kulevya watoweka  • Wauza mahekalu, magari wakimbilia nje 
  • Mawakala wahaha, polisi wapigwa butwaa

LChikawe: Tutawanasa wote kimya kimya
NA MWANDISH WETU
SIKU chache baada ya kunaswa kwa watuhumiwa wanaotajwa kuwa ni vinara wa kusafirisha na kuingiza dawa za kulevya nchini, hali imeanza kuwa tete kwa vigogo wengine wa biashara hiyo.
Baadhi ya vigogo wakiwemo wafanyabiashara wakubwa nchini, wameanza kukimbia nje ya nchi kukwepa mkono wa sheria, huku wengine wakisubiri hali itulie ndipo wajitokeze.
Hatua hiyo inatokana na askari wa Kikosi Maalumu cha Kudhibiti Dawa za Kulevya kuendelea kuwasaka vinara wa biashara hiyo kimya kimya, ikiwa ni mkakati wa kusambaratisha mtandao wa biashara hiyo haramu nchini.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikosi hicho, zinasema kuwa operesheni hiyo imekuwa ikifanyika kwa usiri mkubwa, kiasi cha mamlaka zingine kutofahamu kinachoendelea.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kikosi hicho kilivamia nyumbani kwa Muharani Abdallah  Chonji (44), na kumtia mbaroni akiwa na wenzake wanne kwa tuhuma za kudaiwa kuwa ni kinara wa dawa hizo.
Kukamatwa kwa Chonji, ambaye tayari amepandishwa kizimbani kujibu mashitaka, kumezusha taharuki kubwa huku vigogo wengine wakijificha kukwepa mkono wa sheria.
Habari za kuaminina zinasema kuwa, tangu kutokea kwa tukio hilo, vijiwe vingi vinavyotumika kuuza dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, vimesimama kuendelea na biashara hiyo na vingine mawakala wake wakihama.
Kwa sasa, biashara hiyo hususan ile ya uchuuzi kwa watumiaji wa hali ya chini kabisa (mateja), imekuwa ikifanyika kwa usiri mkubwa tofauti na hapo awali, ambapo ilikuwa ikifanyika hadharani bila woga.
“Hali imekuwa mbaya, matajiri hawaonekani na simu wamezima tangu wanene walipokamatwa… hakuna vijiwe ambavyo vinafanya kazi hadi hapo hali itakapotulia ndipo inaweza kurejea tena.
“Wakubwa wengine wameshapanda pipa (ndege), wamekwenda kusikilizia nchi za watu hali itakuwaje ndipo tutajua kinachoendelea,” kilisema chanzo kimoja.
Chanzo hicho kimesema kuwa operesheni iliyoanzishwa ni tofauti na zilizowahi kufanyika na kwamba, ya sasa imetawaliwa na usiri mkubwa.
Pia, kimesema kuwa askari wanaotumika ni wageni na wamekuwa wakisimamia maadili kwani, hata wanaporubuniwa kwa fedha, wamekuwa wakali.
Habari za kuaminika zinaeleza kuwa, kikosi kinachoendesha operesheni hiyo, kinahusisha askari maalumu wapya, wakiwemo maofisa usalama wa taifa.
Kimesema kuwa siku ya tukio la kwenda kukamatwa kwa Chonji na wenzake, kikosi hicho kiliweka mikakati yake kisha kuomba msaada wa askari polisi wa kituo kimoja.
Hata hivyo, askari wa kituo hicho waliokuwepo kwenye msafara huo hawakufahamu mhusika anayekwenda kukamatwa, badala yake walielezwa kuwa ni jambazi.
“Hawa makamanda walivamia pale bila askari ambao wamezoeleka kufahamu kinachofanyika. Walidai wanakwenda kukamata jambazi, lakini waliposimama nyumbani kwa mtuhumiwa, walishtuka na hawakuweza kufanya lolote zaidi ya kutoa ushirikiano ili kutimiza lengo hilo,” kilisema chanzo hicho.
Hatua hiyo inatokana na madai kuwa, askari polisi wengi wanafahamu mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini na kwamba, inapopangwa mikakati ya kuwatia mbaroni, huwabonyeza ili kutoroka, hivyo kufanya kazi hiyo kuwa ngumu.
Chidi Benz kupanda kortini
Kukamatwa kwa msaani nyota wa hip hop, Rashid Benzino (Chid Benz), kumezidisha hali ya hatari kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Chid Benz anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia leo kujibu mashitaka ya kukutwa na dawa za kulevya.
Msaani huyo alikamatwa na dawa hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, ambapo alikutwa na kete 14 za heroin na misokoto miwili ya bangi.
Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, amewaonya vijana kuacha kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Alisema kukamatwa kwa Chid Benz, ambaye alikuwa na nafasi kubwa ya kuiepusha jamii na biashara hiyo haramu, ni fursa nyingine ya vijana kujifunza na kujiepusha na dawa za kulevya.
Serikali yaonya
Akizungumza na Uhuru jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema hiyo ni operesheni maalumu na kamwe haitakuwa upepo wa mpito, hivyo itakuwa endelevu.
Alisema serikali imeibuka na mbinu mpya za kukabiliana na vinara wa dawa za kulevya na kwamba, vita hiyo itakuwa ya kudumu na hakuna atakayepona.
Aliwataka vijana kukaa mbali na kutojihusisha na vinara wa dawa za kulevya kwani kufanya hivyo ni kujitafutia matatizo.
“Hii mikakati dhidi ya hawa vinara wa dawa za kulevya haitasimama na tumekuja kivingine kabisa…miaka ya nyuma walikuwa wanawatumia vijana wetu kuwaibia taarifa, lakini sasa wataona vumbi tu,” alisema.
Hata hivyo, alionya kuwa vigogo wa dawa hizo  wanaokimbilia nje ya nchi ili kukwepa mkono wa sheria, kamwe hawatakuwa salama kwa kuwa watasakwa kimya kimya na kutiwa mbaroni popote walipo.
Bila kuweka hadharani mikakati hiyo, Chikawe alisema serikali imejipanga kikamilifu na itaendelea kubana njia zote zinazotumika kuingiza dawa hizo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru