Thursday, 13 March 2014

Balozi Lusinde: Serikali tatu zitavunja Muungano


Na Epson Luhwago, Dodoma
MWANASIASA mkongwe nchini, Balozi Job Lusinde, amesema hakubaliani na wazo la kuwa na serikali tatu kwa kuwa kuwepo kwa muundo huo ni kuuvunja Muungano.
Sambamba na kutoa msimamo huo, ameelezea siri ya Tanganyika na Zanzibar kuungana na aliyeshawishi kuwepo kwa Muungano huo.
Akizungumza nyumbani kwake mjini hapa jana, Balozi Lusinde, alisema licha ya kwamba yeye ni muumi wa serikali moja, anapendelea mfumo wa sasa wa serikali mbili uendelee.
Balozi Lusinde ambaye alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa katika serikali ya kwanza ya Tanganyika, alisemakuwepo kwa serikali tatu kutasababisha taifa la Tanzania kusambaratika. 
“Hii hoja ya kuwepo kwa serikali tatu ni tamaa ya watu wachache kutak madaraka, jambo ambalo ni la ubinafsi zaidi na halileti umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania,” alisema.
Aliongeza kuwa Watanzania hawana budi kuzingatia maneno ya mwasisi wa taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliyesema “kwa mtu yeyote mwenye akili timamu lazima afikirie serikali moja na si tatu kama ana nia ya kuulinda Muungano.”
“Hata mimi ninasisitiza kwa kuwa na serikali tatu ni fujo, kwa sababu kutakuwa na gharama kubwa kuziendesha, halafu kila serikali itakuwa na wimbo wake wa taifa, bendera yake na itifaki zake zitakuwa ngumu,” alisema.
Kwa mujibu wa Lusinde, mjadala kuhusu Muungano wa serikali tatu umeanza kuwagawa Watanzania katika makundi, hivyo kuhatarisha amani na umoja wa Watanzania. 
Kutokana na hilo, alisema kuna hatari kubwa ya kulisambaratisha taifa na kusisitiza kuwa hata mchakato wa katiba mpya unaoendelea hivi sasa unapaswa kuwaongoza Watanzania kwenye umoja na si kuleta mifarakano.
“Tusifike mahali watu wakaanza kuleta mambo ya kutuvuruga Watanzania ambao wengi wetu walizaliwa Tanzania. Isifike mahali watu wakawaza mambo ya Tanganyika au Zanzibar. Hata ndani ya bunge la katiba, wajumbe wajadili mambo ambayo yatatupatia katiba ambayo itaendelea kuwaunganisha watu na si kuwagawa,” alisema.
Kuhusu chimbuko la kuungana, Balozi Lusinde, alisema aliyeshawishi si Mwalimu Nyerere bali ni Hayati Abeid Amani Karume. 
Alisema Karume alimfuata Nyerere na kutaka nchi hizo ziungane na kuwa nchi moja na serikali moja, kwa yeye (Karume) kuwa makamu wa rais na Nyerere kuwa rais.
Alisema baada ya wazo hilo, Nyerere aliitisha kikao cha mawaziri na kuzungumzia jambo hilo kuamua kwamba kuwepo kwa serikali moja kungeimeza Zanzibar ambayo wakati huo ilikuwa na miezi mitatu tu tangu kupata uhuru wake kupitia Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Balozi Lusinde alitoa tathmini yake kuwa Muungano huo ambao Aprili 26, mwaka huu utatimiza miaka 50, umekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa shabaha za kuanzishwa kwake zimefanikiwa.
Alizitaja shabaha hizo kuwa ni kudumisha umoja miongoni mwa wananchi wa pande hizo, kuimarisha uchumi, kuimarisha usalama na mwingiliano wa kijamii uliokuwepo kabla ya kuungana.

AKERWA NA TABIA ZA WAJUMBE
Balozi Lusinde, alielezea kukerwa na nidhamu mbaya ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Alisema tabia ya baadhi ya wajumbe hao kutoleana lugha ya maudhi imewafanya wapoteze heshima mbele ya jamii.
Alisema ameshangazwa na hatua ya baadhi yao kutokumheshimu mwenyekiti wa muda wa bunge na hata wengine kutaka kurushiana ngumi. 
“Inashangaza kuona kuwa watu ambao wameaminiwa na Watanzania milioni 45 katika mchakato wa katiba mpya, wanashindwa kuwa na heshima.
“Bunge si mahali pa kutoa lugha za kihuni, pale ni mahali pa heshima, si pa kuropoka ropoka tu. Heshima imeondoka, wanapaswa kufuata kanuni,” alisema.
Kiongozi huyo mkongwe, alisema wajumbe wanapaswa kuelekeza maoni yao kwenye kiti na si kushambuliana kama walivyokuwa wakifanya wakati wa mchakato wa kujadili na kupitisha kanuni za bunge hilo. 
Sambamba na kusitikitishwa na tabia hizo, Balozi Lusinde aliwaasa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuzingatia maslahi ya taifa badala ya vyama na makundi wanayowakilisha.
Alisema iwapo maslahi binafsi yatatangulizwa, kuna hatari ya kupatikana kwa katiba yenye mlengo wa kundi au chama fulani badala ya ile ambayo Watanzania wanaitarajia.  

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru