Na furaha omary
WASHITAKIWA 11 katika kesi ya kuporomoka jengo la ghorofa 16 kwenye mtaa wa Indira Gandhi, Dar es Salaam, wamepelekwa rumande baada ya kubadilishiwa hati ya mashitaka.
Pamoja na mmiliki wa jengo hilo, Raza Ladha (68), waliokuwa nje kwa dhamana wakikabiliwa na mashitaka ya kuua bila kukusudia watu 24 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana walibadilishiwa mashitaka na kuwa ya kuua kwa kukusudia.
Katika kesi hiyo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime ameongezwa.
Wengine ni mhandisi wa jengo hilo, Goodluck Mmbanga (35), Mkaguzi wa jengo Willbrod Mugyabuso (42) na Diwani wa kata ya Goba, Ibrahim Kissoky (59), ambaye ni mfanyabiashara, anayemiliki kampuni ya Lucky Construction ya Dar es Salaam iliyojenga jengo hilo.
Wamo pia Mhandisi Mohamed Abdulkarim (61), Mhandisi wa Manispaa ya Ilala Charles Ogare (48), Mhandisi Mshauri Zonazea Oushoudada (60), anayemiliki Kampuni ya Sou Consultancy Co. Ltd, ambayo ilikuwa ikisimamia ujenzi wa jengo hilo, Msanifu Majengo Vedasto Nzikoruhale (59) na Mwandaaji Michoro ya Majengo Michael Hema (59).
Msajili Msaidizi wa Bodi ya Wasanifu na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Albert Mnuo (56) na Ofisa Mtekelezaji Mkuu wa AQRB, Joseph Ringo (43).
Walibadilishiwa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka na kusomewa 27 ya kuwaua kwa makusudi watu 27. Hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Wakili wa Serikali Mkuu Bernard Kongola, aliiomba mahakama kubadilisha hati ya mashitaka na kumuongeza Fuime na mashitaka kutoka kuua bila kukusudia na kuwa kuuwa kwa kukusudia.
Fuime aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kuua watu wanne kutokana na kuporomoka kwa jengo hilo, Machi 29, mwaka jana, asubuhi alifutiwa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando.
Hatua hiyo ilitokana na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yake.
Baadhi ya washitakiwa walionekana kupigwa butwaa waliposomewa mashitaka mapya. Kesi itatajwa Machi 26, mwaka huu.
Thursday, 13 March 2014
Mapya yaibuka kesi ya kuporomoka jengo
01:09
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru