- Wawakilishi Z’bar wasisitiza ni serikali mbili
- Waponda maoni ya BLW kwenda kwa Warioba
- Sheni apigilia msumari, waraka feki wakwama
Na
waandishi wetu
WAJUMBE
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Baraza la Wawakilishi, wamedai wao si
sehemu ya maoni yaliyowasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pia,
wameponda mchezo mchafu wa baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar kusambaza waraka
kudai msimamo wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW) unaunga mkono mfumo wa
serikali tatu kuwa, hawautambui na kuwa umetengenezwa na wajanja wachache kwa
maslahi binafsi si ya taifa.
Kwa
mujibu wa wawakilishi hao, wao msimamo wao ni serikali mbili na si tatu kama
waraka uliotolewa na kusambazwa na watu wasiojulikana unavyodai.
Akizungumza
na waandishi wa habari bungeni jana, katika ukumbi wa Pius Msekwa, Katibu wa
Kamati ya Wawakilishi wa CCM Zanzibar, Salmin Awadh Salmin, alisema wao
hawakuhusishwa katika kutoa maoni hayo.
Salmin
alisema licha ya Baraza la Wawakilishi kupata nafasi ya kutoa maoni kama
taasisi, ni viongozi wachache waliobeba jukumu hilo bila kuwahusisha wengine
hivyo, maoni hayo si msimamo wa baraza bali ni kikundi cha wachache.
Alisema
utoaji maoni hayo ulifanyika kwa siri bila kutolewa taarifa kwa viongozi,
wakiwemo wa kamati ya uongozi.
Katibu
huyo alisema taarifa na maoni yaliyotolewa kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi
hayakuwa na baraka au kuvishirikisha vikao husika, hivyo kubeba maoni binafsi
ya viongozi waliohusika.
“Hatukuwahi kukutana au kuamua kuwasilisha maoni hayo, tunatambua labda walikuwa na nia njema kiasi cha kusahau hata utaratibu.
“Sisi wawakilishi wa CCM tutaendelea kusimamia na kutekeleza Ilani, kanuni na miongozo ya Chama na kama Chama msimamo wetu ni serikali mbili,’’ alisema.
Salmin
aliwatoa hofu viongozi na wanachama akisema wawakilishi wa CCM hawatakisaliti
Chama na wanachama wake.
Alisema
wao kama wana-CCM watasimamia maelekezo na miongozo kwa gharama yoyote,
wakiamini Muungano imara ni wa serikali mbili. Katibu huyo aliwaasa wananchi
kufuatilia kwa karibu mchakato wa katiba ili kubaini dhamira ya wapotoshaji wa
malengo mema ya waasisi wa taifa la Tanzania.
“Tunaendelea kuamini kwamba, bado miongozo ya CCM ni dira pana na yenye maono ya mbali,’’ alisema.
Habari
za kuamini zimesema kuwa, waraka huo ulisambazwa kwa lengo la kuvuruga Muungano
na kutoa nafasi kwa wachache kutaka kuitawala Zanzibar kwa maslahi binafsi.
Pia,
waraka huo umedaiwa uliandikwa na watu wachache waliojifungia na kuwa maoni
yaliyomo huko hayajawahi kujadiliwa wala kupendekezwa na mjumbe wa wowote wa
BLW.
Juzi,
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Sheni, alisema msimamo wa serikali mbili ndio
unaokubali kwa wengi.
Pia,
amesema kutokana na matakwa hayo ya wananchi, wamekubaliana kuendelea na mfumo
wa serikali mbili yaani ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Alisema
uamuzi huo wa serikali mbili ulifikiwa baada ya kushauriana kati ya pande zote
mbili na kwamba, chokochoko zinazoibuliwa na watu wachache kamwe hazina tija
kwa watanzania.
UVCCM
yambana Maalim Seif
Umoja
wa Vijana wa CCM (UVCCM) Zanzibar, umekitaka chama cha CUF kumbana Makamu wa
Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad, kujiuzulu wadhifa huo.
Umesema
kelele za CUF kumtaka Dk. Sheni
kubatilisha uteuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC),
Salim Jecha Salim na kuvunja sekreteriete yake, hauna mashiko na waanza kwanza
kumbana Maalim Seif.
Naibu
Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, alisema Maalim Seif naye
ameteuliwa na Dk. Sheni hivyo, CUF wanapaswa kupigia kelele uteuzi huo badala
ya Salim.
Alikuwa
akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Bustani huko Kiembesamaki wakati
akiwashukuru wapiga kura kwa kuipa ushindi wa kishindo CCM katika uchaguzi
mdogo wa jimbo hilo uliomalizika karibuni.
“Nimewasikia hawa jamaa zetu wanapiga kelele kutaka Salim na sekreterieti ya ZEC ivunjwe, madai yake ni ya kitoto na kipuuzi, CUF kama kimejipima na kuona kimeshindwa kabla ya mwaka 2015, kikae pembeni kwa kuwa madai yao hayana mashiko,” alisema.
Naye
Mwakilishi wa Kiembesamaki Mahmoud Thabit Kombo, aliwahakikishia wananchi kuwa
atafanya kila awezalo ili kukamilisha ahadi zote alizoahidi kabla ya mwaka
2015.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru