Na Mwandishi wetu.
ASKARI Polisi wa Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo, Dar es Salaam, wanadaiwa kumpiga hadi kufa dereva bodaboda, Salehe Said.
Said (18), mkazi wa Magomeni Kagera, alifariki dunia Machi 23, mwaka huu, saa saba usiku katika Hospitali ya Mwananyamala, ambapo awali akiwa na wenzake watano walifikishwa kituoni hapo na dereva teksi.
Inadaiwa dereva huyo wa teksi, alimfikisha Said na wenzake katika kituo hicho kutokana na kutokea mgogoro wa kugombea abiria katika kituo hicho cha mabasi.
Kwa mujibu wa baba mlezi wa marehemu, Leonard Mkomo, baada ya mwanawe kufikishwa kituoni hapo, alihoji sababu ya kufikishwa na ndipo askari polisi wakaanza kumshambulia kwa kipigo.
Alisema mara baada ya kipigo hicho, hali ya mwanawe ilianza kuwa mbaya na ndipo akapelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu na kufariki dunia siku hiyo hiyo saa saba usiku.
“Baada ya kifo hicho mwenzake na marehemu waliokuwa wakishikiliwa kituoni hapo waliachiwa, jambo ambalo linatia shaka na kusisitiza kuwa polisi walitumia nguvu kubwa katika kukabiliana na tukio hilo,’’alisema.Mkomo alisema familia inafuatilia tukio hilo, na wapo katika mpango wa kuonana na Mkuu wa Polisi Mkoa maalum Kinondoni, Camillius Wambura kumweleza hali halisi kuhusiana na tukio hilo.
“Kwa sasa bado hatujapata ushirikiano wowote kutoka polisi, tunatarajia kuonana na Mkuu wa polisi Kinondoni aweze kutusaidia juu ya tukio hili” alisema.Pia, alisema familia bado haijafikia uamuzi wa kumzika marehemu kwa kuwa wanafanya uchunguzi wa mwili wa marehemu ili kupata uthibitisho zaidi na baadae wataandaa taratibu za mazishi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru