VIONGOZI wa vijiji wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, hivyo kuwa chanzo cha migogoro kati ya wakulima na wafugaji wametangaziwa kiama.
Wanadaiwa kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji na kugawa ardhi holela bila kuwashirikisha wananchi, hivyo kuibua migogoro.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kihangaiko, Madesa na Pongwe Msungura, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alitaka wananchi wasiwachague watu wa aina hiyo katika uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu.
Nape alisema CCM haiko tayari kuona wakulima wakinyanyaswa na watu waliowachagua.
Alisema migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa mikubwa katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Mbeya na mingine ya Kanda ya Ziwa, hivyo ni lazima serikali ichukue hatua.
“Haiwezekani wakulima wateseke kwa kupoteza nguvu kwenye kilimo halafu wafugaji walishe mifugo yao na kutumia fedha kumaliza kesi.” alisema.
Alisema suluhisho ni kuweka mipaka ya ardhi kwa kuzingatia idadi ya watu na si mifugo.
Nape aliahidi kushirikiana na mbunge kuhakikisha serikali inamaliza migogoro ya wakulima na wafugaji.
Mkulima Matogolwa Chamburi, alisema mwishoni mwa mwaka jana, shamba lake la mahindi liliharibiwa na ng’ombe na alipojaribu kupambana na mfugaji alishambuliwa.
Alisema alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Mbwewe, lakini mkuu wa kituo alimtaka wakakubaliane na mfugaji ili wamalize kesi kwa kuwa itakuwa usumbufu.
Matogolwa alisema baada ya mvutano alilipwa sh. 40,000 na kulazimishwa kufuta kesi licha ya kutumia sh. 30,000 za nauli ya pikipiki kwenda na kurudi Pongwe.
Akizungumza kwa nyakati tofauti, mgombea ubunge wa CCM katika uchaguzi mdogo jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, alisema suluhisho la migogoro hiyo ni kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi.
Tuesday, 25 March 2014
Kiama cha wala rushwa chaja
07:32
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru