NA CHARLES MGANGA, DODOMA
MWENYEKITI wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, amepongezwa kwa kutumia busara kuongoza vikao.
Samia Suluhu Hassan, alitoa pongezi jana, baada ya kurejesha fomu kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Bunge.
Alisema wajumbe waliamua kumchagua Kificho kutokana na uzoefu alionao.
Samia, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alisema kuongoza vikao wakati hakuna kanuni kulihitaji mtu mwenye uwezo mkubwa.
“Wajumbe walizingatia uzoefu, ukongwe na busara katika kuongoza shughuli za Bunge ndiyo sababu Kificho alipata fursa.
“Amefanya kazi kubwa iliyohitaji mtu wa aina yake, ambaye ni makini na mwenye uvumilivu,” alisema.
Samia amewashauri wajumbe kuzingatia kanuni wakati wa vikao kwa sababu ndiyo msingi wa uendeshaji shughuli bungeni.
“Kwa kufanya hivyo tutatekeleza kazi kwa uadilifu ili mwishowe tupate katiba bora,” alisema.
Wajumbe juzi walimchagua Samuel Sitta kwa kura 487 kuwa Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge hilo.
Sitta na makamu wake wanatarajiwa kuapishwa na Katibu wa Bunge kabla ya kuanza rasmi vikao kupitia Rasimu ya Katiba.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru