- JK aridhia marekebisho mengine, posho kuendelea kuwa sh. 300,000
Na Mwandishi wetu
MJADALA
wa nyongeza ya posho kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, umefungwa rasmi
baada ya Ofisi ya Rais Ikulu, kusema kiwango cha posho kitaendelea kuwa sh.
300,000 kwa siku.
Pia,
imesema hakuna mbunge aliyeongezewa posho na kuwa, hakuna maombi
yaliyowasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete kuombwa kuaridhie nyongeza ya viwango
vya posho kutoka sh. 300,000 hadi 500,000.
Kutokana
na hatua hiyo, Ikulu imesema hakuna ongezeko lolote la posho za wajumbe ambalo,
Rais Kikwete ameliridhia na kutaka mjadala huo ufungwe kwa kuwa hauna tija wala
ukweli.
Hivi
karibuni baadhi ya wajumbe wa bunge hilo limbana Mwenyekiti wa Bunge, Pandu
Ameir Kificho wakidai posho ya sh. 300,000 wanayolipwa kwa siku ni ndogo na
hailingani na gharama za maisha ya Dodoma.
Madai
hayo yalimlazimu Pandu kuunda Kamati kwa ajili ya kufuatilia posho ambayo
iliundwa na wajumbe sita akiwemo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi.
Wengine
ni Mohammed Aboud Mohammed, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais Zanzibar, Paul Kimiti, Asha Bakari Makame, ambaye amewahi kushika
nyadhifa za uwaziri Zanzibar na Jenista Mhagama, ambaye pia ni Naibu Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Hata
hivyo, madai hayo yalizusha mjadala mkali kutokana na wananchi kupinga na
kuwatuhumu wabunge kujali maslahi yao mbele badala ya kazi waliyotumwa.
Pia,
baadhi ya wajumbe walipingana na wenzao kuhusu nyongeza hiyo na kueleza kuwa
kiasi wanacholipwa kwa siku ni kikubwa.
Taarifa
ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu kwa vyombo vya habari jana, imesema kuwa Rais
Kikwete hajapokea maombi kutoka kwa Uongozi wa Bunge kumwomba aridhie posho
mpya hivyo, wajumbe wote watalipwa sh. 300,000 kwa siku.
Imesema
kuwa kumekuwepo na habari nyingi, baadhi zenye kuchanganya umma kuhusu posho za
wajumbe wa Bunge la Katiba.
Imesema
kuwa taarifa zingine zimedai kuwa baadhi ya wafanyakazi nchini wamepanga
kuandamana iwapo Rais Kikwete, atakubaliana na maombi ya nyongeza ya posho
hizo.
‘’Mhe. Rais hajapata kupokea maombi yoyote kutoka kwa Uongozi wa Bunge ya kumwomba aridhie kuongezwa kwa posho ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kiwango cha sasa cha sh. 300,000 kwa siku hadi kufikia 500,000 ama 700,000 kama ambavyo imekuwa ikivumishwa.
‘’Mhe. Rais hajapata kupokea maombi ya nyongeza ya posho hiyo, hakuna ongezeko lolote la posho ambalo Mhe. Rais ameliidhinisha.
‘’Kwamba alichopokea Mhe. Rais ni maombi ya Uongozi wa Bunge wa kuomba Mhe. Rais aridhie kufanyika marekebisho katika kiwango cha malipo ya siku kwa wajumbe hao cha sh. 300,000 ili posho ya kikao iwe posho ya kujikimu na posho ya kujikimu iwe ndio posho ya kika,’’ ilisema taarifa hiyo.
Pia,
imeongeza kuwa Rais Kikwete amelikubali ombi hilo la kufanyika kwa marekebisho
katika mpangilio huo wa posho, lakini kiwango cha malipo ya kila siku
kitaendelea kuwa sh. 300,000 kwa siku.
WAJUMBE
WAJA JUU
Akizungumzia
hilo, mjumbe James Mbatia, ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema suala
la posho halina umuhimu katika katiba, bali cha muhimu ni kupata katiba bora.
Kwa upande
wake, mjumbe Issa Ameir Suleiman, alisema suala la posho limezuka kutoka kwa
baadhi ya wajumbe lakini halina nafasi.
Alisema
baadhi ya wajumbe katika maeneo yao hawapati kiwango hicho cha posho
wanapokwenda kwenye shughuli kama vile makongamano.
Naibu
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alisema serikali haina fedha za nyongeza kwa
posho za wajumbe na kwamba, anayeona sh. 300,000 haimtoshi ni vyema akafungasha
virago.
Alisema
serikali ina mambo mengi ya kufanya kwa ajili ya maendeleo ya watanzania na kwamba,
haiwezi kutumia mamilioni ya shilingi kulipa wajumbe wa bunge hilo.
‘’Kama taifa tuna matatizo mengi na mambo muhimu ya kufanya, hatuwezi kulipa wajumbe posho ya sh. 500,000 kwa siku, kama kuna aliyeona kiasi hicho hakimtoshi afungashe virago aondoke Dodoma,’’ alisema Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara).
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru